Siri ya kunyongwa bila hatia

Muktasari:

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Angola, Pitta Groz amethibitisha Serikali yake imetoa hati ya kukamatwa Isabel dos Santos, binti wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jose Eduardo dos Santos.


Lisbon. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Angola, Pitta Groz amethibitisha Serikali yake imetoa hati ya kukamatwa Isabel dos Santos, binti wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jose Eduardo dos Santos.

Isabel aliwahi kutangazwa na jarida la biashara la Marekani la Forbes kuwa mwanamke tajiri Afrika mwenye mali inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 3.5 (sawa na Sh8.05 trilioni).

Groz alisema Serikali ya Angola inashirikiana na Shirika la Polisi la Jinai la Kimataifa (Interpol) linalounganisha nchi 190, kumkamata Isabel dos Santos.

Jitihada za kumkamata Isabel zimekuja baada ya miaka mingi ya uchunguzi uliokuwa ukifanywa na mamlaka ya Angola kutokana na ufisadi alioufanya wakati baba yake, Jose Eduardo dos Santos akiwa madarakani.

Jose Eduardo dos Santos alitawala Angola kwa miaka 38 kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 2017. Alifariki dunia Julai 8, 2022, Barcelona nchini Hispania na alizikwa Luanda, Angola, Agosti 28, 2022.

Wakati wa utawala wake aliandamwa na shutuma za rushwa na upendeleo kwa familia yake.

Baada ya Jose Eduardo dos Santos kuondoka madarakani, Joao Lourenco alichukua madaraka ya nchi. Kabla ya kuchukua mamlaka ya nchi, Lourenco alikuwa Waziri wa Ulinzi kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.

Kuingia kwa Lourenco madarakani alianza kushughulikia vitendo vya rushwa vya Serikali iliyopita, ikiwamo familia ya mtangulizi wake. Mwaka 2020 mtoto wa dos Santos, José Filomeno dos Santos alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa ubadhirifu wa fedha za umma Dola5 milioni za Marekani (sawa na Sh11 bilioni). Hata hivyo, aliendelea kuwa huru baada ya kukata rufaa.

Kesi za Isabel

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Groz alisema Isabel kwa miaka mingi amekuwa akichunguzwa na ofisi yake kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Idadi kubwa ya wananchi wa Angola ambao ni masikini na wanaishi chini ya Dola 1.90 za Marekani kwa siku (Sh4,200).

Groz alisema Januari 2020, Isabel alifunguliwa mashitaka ya utakatishaji wa fedha, ushawishi wa kibiashara haramu, uongozi mbaya na utengenezaji wa nyaraka bandia ambayo ni miongoni mwa makosa ya uhujumu uchumi aliyoyafanya wakati akiongoza Kampuni ya Mafuta ya Sonangol inayomilikiwa na Serikali.

Alisema licha ya kufunguliwa kwa mashitaka hayo, Isabel haishi Angola, makazi yake yako maeneo mbalimbali duniani, ikiwamo London Uingereza na Dubai, Falme za Kiarabu.

Groz alisema Isabela amekuwa hajibu barua anazoandikiwa akitakiwa kujibu hoja zilizotumwa kwa wakili wake, kwenye makazi yake ya Luanda, Angola na Uholanzi ilikosemekana ndio alikuwa akiishi. Hata hivyo, Isabel alilieleza Gazeti la The New York Times kwa njia ya simu kuwa wakati wote yuko tayari kuwasiliana na mamlaka ya Angola.

Alisema yeye na timu yake ya wanasheria hawajapokea notisi yoyote ya kukamatwa na hajaiona kwenye mtandao wa Interpol.

“Anuani zangu zinajulikana, nilipo panafahamika. Mimi sio mkimbizi na sijajificha kumkimbia yeyote,” alisema Isabel huku akiongeza kwamba anaishi London, Uingereza.

Isabel alisema shutuma dhidi yake zina msukumo wa kisiasa. Alisema kama kuna notisi ya kukamatwa iliyotolewa, atakuwa tayari kwenda mahakamani kutoa ushahidi kwa kuwa hajaiba mali za Serikali na kampuni zake ziko kihalali na zimetokana na mikopo ya benki.

Alisema uchunguzi na shutuma dhidi yake ni msukumo wa kisiasa wa Rais Lourenço. “Ananiona kama ni tishio kisiasa na mgombea mzuri wa nafasi ya urais hapo baadaye,” alisema.

Alisema hata tuhuma dhidi ya rushwa na upendelezo ni kutaka kuharibu sifa ya baba yake, dos Santos, ambaye ameitawala nchi hiyo tangu watawala wa kikoloni.

Isabel mara kwa mara amepuuza madai kuwa familia ya Rais ilipewa nafasi zaidi kuliko raia wengine kudhibiti uchumi na masuala ya kisiasa ili kuhakikisha familia hiyo inaendelea kutawala.

Binti huyo alikuwa anasimamia shirika la mafuta la Taifa na kampuni kubwa zaidi ya kutoa huduma za simu na sasa anadhibiti benki kubwa nchini Angola ya BFA.

Isabel anaendesha biashara kubwa akiwa na kampuni nchini Angola na Ureno na anamiliki hisa katika Kampuni ya Nos SGPS.

Familia na elimu

Isabel alizaliwa Baku, Azerbaijan (wakati ule Jamhuri katika Umoja wa Kisovyeti) akiwa binti wa kwanza wa dos Santos (baadaye Rais wa Angola) na mkewe wa kwanza, Tatiana Kukanova wa Urusi, ambaye alikutana naye wakati wa masomo katika Umoja wa Kisovyeti.

Alihudhuria shule ya wasichana huko Kent, Cobham Hall. Alisoma uhandisi wa umeme katika Chuo cha King’s London.

Huko alikutana na Sindika Dokolo ambaye kwa sasa ndiye mumewe raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC). Sindika Dokolo ni mtoto wa milionea kutoka Kinshasa mwenye mke raia wa Denmark.

Biashara za Isabel

Mwaka 1997, alianza biashara ya kwanza, akifungua Club ya Miami Beach, moja ya vilabu vya kwanza vya usiku na mikahawa ya pwani kwenye Kisiwa cha Luanda.

Juni 2016, aliteuliwa na baba yake (Rais dos Santos) kuwa mwenyekiti wa Sonangol, Kampuni ya Mafuta ya Serikali ya Angola.

Miezi miwili baada ya Rais Joao Lourenco kuapishwa kuchukua madaraka ya nchi alimwachisha kazi Isabel.