Spare: Kitabu cha Harry kitakachozua balaa Uingereza-2

Muktasari:

  • Familia ya kifalme ya Uingereza sasa imejiandaa kwa uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na mwana mfalme, Prince Harry, wakionywa kinaweza kuwa bomu kwa Ufalme wa Uingereza, huku mawakili wa Ikulu wakijiweka tayari kusubiri uzinduzi wake uliopangwa kufanyika Januari 10 mwakani.

Familia ya kifalme ya Uingereza sasa imejiandaa kwa uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na mwana mfalme, Prince Harry, wakionywa kinaweza kuwa bomu kwa Ufalme wa Uingereza, huku mawakili wa Ikulu wakijiweka tayari kusubiri uzinduzi wake uliopangwa kufanyika Januari 10 mwakani.

Taarifa ya uzinduzi wa kitabu hicho kiitwacho Spare ilitolewa Alhamisi iliyopita.

Wanafamilia wa familia ya ufalme wa Uingereza hawakuarifiwa kuhusu ujio wa kitabu hicho, ambacho kitakuwa na toleo la lugha ya Kihispania.

Awali kitabu hicho ilikuwa kizinduliwe mwishoni mwa mwaka huu kuwahi msimu wa mapumziko wa sikukuu za mwisho wa mwaka, ikiwamo Krismasi ambapo kingepata soko kubwa, badala yake kitazinduliwa Januari.

Inasemekana kuahirishwa kwa uzinduzi huo ni kwa sababu ya heshima kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth na mabadiliko hayo ya dakika za mwisho yalifanywa na Prince Harry mwenyewe.

Wachapishaji wa kitabu hicho, Penguin Random House wameweka wazi kuwa Harry hatakwepa mada nyeti kama vile uamuzi wa familia kumtia moyo yeye na kaka yake mkubwa Prince William kutembea nyuma ya jeneza la mama yao, Diana.

Walisema Harry anaweza pia kufichua ni mshiriki gani wa kifalme ambaye alitoa maoni ya ubaguzi wa rangi juu ya rangi ya ngozi ya mtoto wake, ambaye alikuwa hajazaliwa wakati huo, Archie, au kuangazia uhusiano wake mbaya na baba yake ambaye sasa ni Mfalme wa Uingereza na nyakati ngumu na za shida kati yake na kaka yake, Prince William.

Yaliyomo kwenye kitabu cha Harry yana uwezekano mkubwa wa kufanywa siri ya hali ya juu na wasaidizi wa Ikulu. Maofisa wa Jumba la Buckingham wamefichua kuwa hakuna washiriki wa familia ya kifalme waliopewa nafasi ya kujua kinachoendelea kabla haijatangazwa hadharani.

Wakati mpango wa uchapishaji ulipotangazwa Julai mwaka jana, ni Malkia pekee aliyepewa onyo la mapema. Kitabu hicho kitakuwa na barua fupi inayoelezea kuwa kitabu hicho kiliandikwa kabla ya kifo cha Malkia Elizabeth huko Balmoral Septemba 8 mwaka huu.

Msemaji wa Mfalme alikataa kutoa maoni juzi usiku alipoombwa kufanya hivyo. Kaya ya Kifalme imeonywa kwamba kitabu hicho chenye kurasa 416, kinachotarajiwa kuuzwa kwa Pauni 28 za Uingereza ni muhimu kwa kila mtu na wanakiogopa.

Jamaa wa Harry wanaweza kukabiliwa na vichwa vya habari vya magazeti ikiwa Harry atachagua kutafakari mambo yenye utata ya maisha ya kifalme, tangu miongo iliyopita.

Gazeti ‘Daily Mail’ la Uingereza limeambiwa kwamba Harry, ambaye amerekodi kwa sauti sehemu ya kitabu hicho, hakuiambia familia yake mapema juu ya jina hilo na kwamba litaonekana kama utata na uchochezi katika duru za kifalme. Chanzo kingine kililiambia gazeti la ‘Daily Mirror’ kuwa “Jina lenyewe linaonyesha shambulio lingine la makabiliano dhidi ya familia ya kifalme, baada ya kudai kutaka faragha. Wanasheria wa Buckingham bila shaka watakuwa katika hali ya kusubiri kuona kilichomo ndani yake.

“Ikiwa madai ya awali ya Harry katika mahojiano mengi aliyofanya katika vituo vya runinga hayatakuwa na mabadiliko, hii itakuwa nyuklia. Bila kujali maudhui, ambayo bila shaka yatakuwa ya kulipuka, kutakuwa na nafasi ndogo ya kufanya kama chombo cha upatanisho kwa Harry na (mkewe) Meghan”.

Harry aliripotiwa kulipwa kitita cha Dola 20 milioni (wastani wa Sh46.6 bilioni) kwa kitabu hicho kama sehemu ya mkataba wa mauzo.

Tangazo la kuzinduliwa kwa kitabu hicho lilikuja kama mshangao baada ya miezi kadhaa ya uvumi, ambapo wachapishaji Penguin Random House walisema: ‘Spare inawarudisha wasomaji mara moja kwenye mojawapo ya picha zilizoungua sana za karne ya 20, wavulana wawili, wana mfalme wawili, wakitembea nyuma ya jeneza la mama yao, huku ulimwengu ukitazama kwa huzuni na hofu. Wana wa mfalme hao walikuwa na umri wa miaka 12 na 15 wakati wa mazishi ya mama yao yaliyofanyika Jumamosi ya Septemba 6, 1997 na Harry ameweka wazi kuwa alidhani ni kitu ambacho hakuna mtoto anapaswa kushurutishwa afanye.

Kitapatikana kwa Kiingereza nchini Uingereza, Ayalandi, Australia, New Zealand, India, Afrika Kusini na Canada, huku kitabu hicho pia kikichapishwa katika lugha 15 za ziada, zikiwamo za Kihispania, Kiitaliano, Kijerumani na Kichina.

Juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Random House, Markus Dohle, alisema: “Tuna heshima kubwa kwa kuchapisha simulizi ya wazi na yenye hisia za Prince Harry kwa ajili ya wasomaji kila mahali. “Anasimulia safari binafsi ya kusisimua kutoka katika hali ya kuwa na kiwewe hadi uponyaji, ambayo inazungumza na nguvu ya upendo na itawatia moyo mamilioni ya watu duniani kote”.

Maelezo katika kitabu hicho yanaonekana kuwa mabaya zaidi kuliko Harry alivyokielezea kitabu hicho Julai mwaka jana. Kisha, akasema: “Ninaandika haya si kama mwana mkuu niliyezaliwa bali mtu aliyekua”. Mark Borkowski, mwandishi na mtaalamu wa utangazaji, alisema kulikuwa na wakati mwingi wa kuhariri kitabu hicho kati ya kifo cha Malkia mapema Septemba na tarehe ya uchapishaji kabla ya kutangaza kinazinduliwa lini.

Wachambuzi wa mambo wameona kuwa kitabu hicho kinaweza kuitia doa familia ya kifalme ya Uingereza kiasi kwamba Mfalme Charles anaweza kulipiza kisasi kwa kutompa mwanaye huyo na mkwewe vyeo vya kifalme, na hata kuondoa majina yao ya Duke na Duchess wa Sussex.

Harry alionywa kwamba kisasi cha Sussex kitajibiwa, kwa hivyo kutakuwa na Krismasi yenye wasiwasi kati ya familia ya Kifalme huko Sandringham, kwani wanatarajia mabaya zaidi. Kwa Mfalme mpya, Charles, bado anapanga kutawazwa kwake, na huenda hii inakuja wakati mbaya zaidi wa mtanziko katika familia.

Mhudumu mmoja wa ndani wa jumba la kifalme alisema: “Tangazo la kwanza lilikuwa jambo la kushtua sana. “Sasa tumetumia muda mrefu kusubiri kuona kilichomo ndani yake na kusema ukweli, tunataka haya yaishe kila mtu asonge mbele”.