Spika Afrika Kusini ajiuzulu kwa kashfa ya rushwa

Muktasari:

Licha ya kujiuzulu, Spika Nosiviwe Mapisa-Nqakula amekanusha tuhuma hizo, akisema amejiuzulu kupisha uchunguzi.

Johannesburg. Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejiuzulu nafasi hiyo baada ya Polisi kuvamia nyumbani kwake kufanya uchunguzi.

Mapisa-Nqakula anatuhumiwa kuomba rushwa ili kutoa kandarasi wakati akiwa waziri wa ulinzi.

Hata hivyo, amekanusha tuhuma hizo, akisema kujiuzulu kwake hakumaanishi kwamba amekiri kosa.

Amesema, kutokana na umakini wa uchunguzi, asingeweza kuendelea na wadhifa wake.

Mapisa-Nqakula (67) ambaye ni miongoni mwa wapigania uhuru wa kupinga ubaguzi wa rangi, alichaguliwa kuwa spika mwaka 2021.

Kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Ulinzi kwa miaka saba.

Wiki iliyopita wanasheria wa Mapisa Nqakula walifungua kesi mahakamani wakiomba kupinga kukamatwa kwake wakisema kutavunja heshima yake.

Jumanne iliyopita, majaji walikataa maombi hayo kwa msingi kwamba suala hilo halikuwa muhimu na hawakueleza kuhusu kukamatwa kwake ambako kulikuwa bado hakujatekelezwa.

Mapisa Nqakula anatuhumiwa kudai fedha zinazofikia dola 120,000 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ili kumpa zabuni ya kusafirisha vifaa vya kijeshi kutoka nchi nyingine za Afrika kuja nchini Afrika Kusini, gazeti la Business Day limeripoti.

Kujiuzulu huko kumekuja ukiwa umebaki mwezi mmoja kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo, ambao baadhi ya watu wanaamini utakuwa mgumu kwa chama tawala cha African National Congress (ANC).

Chama hicho ambacho kiko madarakani tangu mwaka mwaka 1994, kimekumbwa na tuhuma nyingi za rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma na ndio imekuwa ajenda kuu ya uchaguzi.