Sudan yafuta chama cha Omar al-Bashir

Muktasari:

Mamlaka inayoongoza kipindi cha mpito nchini Sudan imepitisha Sheria ya kuvunja chama cha National Congress (NCP) cha rais aliyeng'olewa madarakani, Omar al-Bashir.

Khartoum. Mamlaka inayoongoza kipindi cha mpito nchini Sudan imepitisha Sheria ya kuvunja chama cha National Congress (NCP) cha rais aliyeng'olewa madarakani, Omar al-Bashir.

Vilevile mamlaka hiyo imeondoa sheria ya umma ambayo ilitumiwa kudhibiti mienendo mbalimbali ya wanawake katika kipindi cha Al Bashir.

Hatua zote zimejibu madai ya vuguvugu la waandamanaji ambayo yalilenga, na hatimaye kufanikiwa, kuuvunja utawala wa Rais Bashir baada ya kusaidiwa na jeshi.

Bashir alichukua madaraka 1989 kwa mapinduzi na kuongoza taifa hilo kwa miaka 30 hadi alipoondolewa kwa vuguvugu la maandamano Aprili mwaka huu.

Sudan kwa sasa inaongozwa na utawala unaojumuisha jeshi na Baraza la Kiraia pamoja na Baraza la Mawaziri la raia linaloongozwa na Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok.

Kuvunja chama cha Bashir

Imepitishwa sheria ambayo inasema kamati itaundwa kutekeleza suala la kuvunja chama cha NCP, hatua inayomaanisha kuwa mamlaka zinaweza kuhodhi mali za chama hicho.

Hii inafanyika ili waweze kurejesha utajiri ulioibwa," alisema Hamdok katika ujumbe wake wa Twitter.

Katika ujumbe huo Hamdok aliandika: "Sheria za umma pamoja na maadili ya umma zilitumiwa kama chombo cha unyonyaji, kuaibisha, ukiukaji wa haki za raia na ukiukaji wa hadhi ya watu.

"Ninatuma ujumbe wa heshima kwa vijana wa kike na kiume wa nchi yangu ambao wamepitia masaibu ya utekelezwaji wa sheria hizi."

Wanawake walikua mstari wa mbele katika vuguvugu lililomng'oa madarakani Bashir.

Kwa mujibu wa BBC, sheria hiyo pia inasema hakuna nembo yoyote ya utawala au chama itakayoruhusiwa kuhusika katika shughuli yoyote ya kisiasa kwa miaka 10.

Msemaji wa Muungano wa wasomi wa Sudan na kikundi cha waandamanaji kilichompindua Rais al-Bashir, ameiambia BBC kuwa huu ulikuwa ni wakati wa kihistoria.

"Huu ni wakati wa ahueni kwa sababu kila mtu nchini Sudan ameathiriwa vibaya na utawala kwa namna moja au nyingine," alisema msemaji Samahir Mubarak.

Wanaharakati wanasema chini ya sheria za ukandamizaji, zenye misingi ya ufafanuzi sheria ya Kiislamu (Sheria) , wanawake walikamatwa kwa kuhudhuria mikutano ya binafsi ya chama au kwa kuvaa suruali.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema maelfu ya wanawake walikamatwa na kupigwa kwa mienendo isiyofaa kila mwaka, na sheria zilitumiwa kiholela.