Sudani hakukaliki

Kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Dagalo maarufu (Hemedti)

Muktasari:

  • Mapigano yameendelea nchini Sudan ikiwa ni muda mfupi tu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Sudan. Mapigano na mashambulio zaidi ya anga yameripotiwa nchini Sudan, ikiwa ni saa chache tu tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayo kwa siku saba, baina ya jeshi la Serikali na vikosi vya wanamgambo wa RSF.

Makubaliano hao mapya, yalitakiwa kuanza rasmi jana usiku; hata hivyo, bado hakuna utekelezaji wa makubaliano hayo.

Mapigano hayo yalianza wiki tano zilizopita, yakichochewa na mzozo wa madaraka kati ya viongozi wa jeshi la Serikali na Wanamgambo wa kikundi hicho cha RSF.

Majaribio ya awali yaliyolenga kuleta utulivu wa kudumu yameripotiwa kuyumba na kusababisha hofu ya mapigano kuendelea kwa muda mrefu.

Kulikuwa na matumaini mapya ya usitishaji wa vita hiyo kufuatia mazungumzo rasmi ambayo yalisimamiwa na nchi za Saudi Arabia na Marekani.

Kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Dagalo maarufu Hemedti, alirekodiwa katika ujumbe wa sauti akisema wanajeshi wake hawatarudi nyuma hadi pale watakapokamilisha mapinduzi nchini humo.

Mkazi wa Khartoum Moe Faddoul aliiambia BBC kwamba dakika chache baada ya makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano, kulitokea mashambulizi mawili ya anga magharibi mwa mji huo, ambako kuna kambi kuu ya jeshi la anga la nchi hiyo.

"Nyumba ilitikisika mahali ninapokaa," alisema, na kuongeza: “Kulikuwa pia na mapigano, lakini mapigano yalikuwa yamesitishwa,” Faddoul aliongeza.

Faddoul alisema kwamba wakazi wengi walikuwa wamekimbia, na hakukuwa na magari barabarani huku watu wachache tu walikuwa wakitembea kutafuta mahitaji muhimu.

Wakati huo huo, raia waliiambia Reuters kwamba walisikia ufyatuaji risasi katika miji ya Omdurman na Bahri, miji pacha ya Khartoum.

Mapigano yalizuka mjini Khartoum Aprili 15, kufuatia siku za mvutano kati ya Serikali na wanachama wa RSF na ndipo walipoanza kusambazwa nchini kote katika hatua ambayo jeshi liliona kama tishio.

Mzozo mkubwa ni kati ya Jenerali Dagalo na Mkuu wa Jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ambaye amekuwa kiongozi wa Sudan tangu Rais Omar al-Bashir alipopinduliwa mwaka 2019.

Mamia ya watu wameuawa katika mapigano hayo na Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali mbaya zaidi katika nchi hiyo ambayo tayari idadi kubwa ya watu wake wamekuwa wakitegemea misaada zaid hata kabla ya mzozo huo.

Taarifa kutoka vyanzoi mbalimbali vya habari vinabainisha kuwa, zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao tangu mapigano hayo kuanza.