Tanzania na Denmark zajadiliana ushirikiano

Muktasari:

Tanzania na Denmark zajadiliana ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, afya, biashara na uwekezaji.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Denmark zimekubaliana kushirikiana katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa mataifa hayo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichowakutanisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera ya Hali ya Hewa Duniani wa Denmark, Dan Jørgensen.

Mazungumzo yao waliyoyafanya leo Jumatano, Aprili 3, 2024 jijini Dar es Salaam kisha kuzungumza na waandishi wa habari. Waziri Makamba amesema hiyo si mara ya kwanza kwa mataifa hayo kushirikiana.

Amesema ushirikiano baina ya nchi hizo, ulishuhudiwa ukiota mizizi mwaka 2021, taifa hilo lilipoamua kufunga ubalozi na baadaye kubatilisha uamuzi huo.

“Kama mnakumbuka mwaka 2021 Serikali ya Denmark iliamua kufunga ubalozi wake nchini na mwaka jana ikabadilisha uamuzi huo na huyu ndio kiongozi wa kwanza tumempokea tangu uamuzi huo ulipofutwa, hii inaashiria kwamba Serikali yao bado inapenda kuwa Karibu na kushirikiana na sisi," amesema.

Kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na ujio wa waziri huyo Makamba amesema zipo za kibiashara zitakazoibuliwa na ushirikiano huo.

“Wenzetu wameendelea kwenye teknolojia hivyo kuna fursa ya kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali,” amesema.

Katika mkutano huo, Waziri Jørgensen alizungumza kwa kifupi hasa akiwashukuru waliohudhuria mkutano huo.

Imeandikwa na Ammar Masimba