Upinzani DRC kuandamana kesho wakati Rais Tshisekedi akiapishwa

Muktasari:
- Siku chache baada ya mahakama ya kikatiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumuidhinisha Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa urais katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni, viongozi watatu wa upinzani wameitisha maandamano nchi nzima kupinga matokeo ya uchaguzi.
DRC. Viongozi watatu wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameitisha maandamano nchi nzima kesho Jumamosi kupinga matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni, wakati Rais Felix Tshisekedi akitarajiwa kuapishwa kuwa Rais kwa muhula wa pili.
Tshisekedi alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita akishinda kwa asilimia 73 ya kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini humo, hata hivyo matokeo hayo yalipingwa na baadhi ya wagombea wa upinzani kwa kile walichodai ulikuwa na udanganyifu na kutaka urudiwe upya.
Wito wa maandamano hayo ulitolewa kwa pamoja katika mkutano na waandishi wa habari na Moise Katumbi, ambaye kwa mujibu wa matokeo rasmi, aliibuka mshindi wa pili kwa kupata asilimia 18, Martin Fayulu, aliyeibuka wa tatu akiwa na asilimia 5 na Anzuluni Bembe, aliyepata asilimia 1.
Wagombea hao wamedai kuwa kulikuwa na udanganyifu ikiwemo kuongezwa kwa kura bandia katika masanduku ya kura hata hivyo watatu hao walikataa kupinga matokeo kisheria kwenye mahakama ya kikatiba kufuatia chombo hichohicho kuidhinisha ushindi wa Tshisekedi.
Mnamo Desemba 31, mwaka jana tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo akishinda kiti hicho kwa mara ya pili mfululizo.