Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifo vya Ebola Congo vyazidi 100, tahadhari ikitolewa

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo ulitangazwa Mei 15, 2026, ingawa wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo ulianza kusambaa kabla ya kugunduliwa rasmi, hali iliyofanya juhudi za kuudhibiti kuwa ngumu zaidi.

Congo. Zaidi ya watu 100 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja tangu mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zitangaze mlipuko wa ugonjwa huo mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Marekani (AP), likinukuu mamlaka za afya nchini Congo, hali ya ugonjwa huo inaendelea kutia wasiwasi huku juhudi za kuudhibiti zikiongezwa.

AP imeeleza changamoto mbalimbali zinaendelea kuathiri mapambano dhidi ya ugonjwa huo, zikiwamo mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya, mashaka ya wananchi kuhusu ugonjwa huo pamoja na mapigano ya makundi yenye silaha katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya hali ya ugonjwa huo iliyotolewa Jumatatu ya Juni 8,2026  usiku, wagonjwa 550 wamethibitishwa kuambukizwa Ebola hadi kufikia Jumapili, huku watu 101 wakifariki dunia na wengine 19 wakipona.

Mlipuko huo umejikita zaidi katika Mkoa wa Ituri mashariki mwa Congo, ambao unachangia zaidi ya asilimia 90 ya matukio yote yaliyoripotiwa.

Matukio mengine yameripotiwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku ugonjwa huo ukiripotiwa pia kuvuka mpaka na kuingia nchini Uganda.

Mamlaka za afya zinaamini idadi halisi ya wagonjwa itakuwa kubwa zaidi kutokana na kuchelewa kugunduliwa kwa mlipuko huo pamoja na changamoto za ufuatiliaji wa watu waliokutana na waathirika. Ingawa kiwango cha ufuatiliaji kimeimarika hivi karibuni, bado kipo katika asilimia 64.

Mlipuko huo unasababishwa na virusi adimu vya Bundibugyo, aina ya Ebola ambayo hadi sasa haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa.

Hali hiyo ni tofauti na aina ya virusi vya Zaire Ebola vilivyohusika katika milipuko mingi ya awali nchini humo na ambavyo vina chanjo pamoja na matibabu yaliyothibitishwa.

Mwendesha bodaboda mmoja, Justin Abekani, ameiambia AP kuwa mamlaka zimepiga marufuku kubeba abiria wawili kwa wakati mmoja.

“Tumepigwa marufuku kubeba wateja wawili kwenye pikipiki moja. Sasa tunaruhusiwa kubeba mteja mmoja tu,” amesema.

Licha ya hatua hizo, bado kuna maeneo ambayo wananchi wanaonyesha mashaka na kupuuza kanuni za afya zilizowekwa.

Baadhi ya walionusurika katika mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018 nchini Congo wameonya kurudiwa kwa makosa ya zamani kunaweza kusababisha vifo vingi ambavyo vingezuilika.

Wakati huohuo, wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu, wakikabiliwa na uhaba wa malipo, uchovu mkubwa na mashambulizi kutoka kwa baadhi ya wananchi.

Kwa mujibu wa AP, mapigano yanayoendelea kati ya makundi ya waasi katika baadhi ya maeneo yamewazuia wahudumu hao kufikia jamii zinazohitaji huduma za haraka za afya.

Kwa miaka mingi, mashariki mwa Congo imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi mbalimbali ya waasi na wanamgambo, baadhi yao yakidaiwa kuwa na uhusiano na mataifa ya nje au kundi la itikadi kali la Islamic State.


Maandamano Kenya

Wakati hali ikiwa hivyo nchini Congo, Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limeripoti polisi nchini Kenya wamewatawanya kwa mabomu ya machozi waandamanaji katika eneo la Nanyuki waliokuwa wakipinga ujenzi wa kituo cha kuwahifadhi wagonjwa wa Ebola kutoka Marekani.

Makundi ya waandamanaji waliokuwa wakipeperusha bendera za Kenya na kubeba jeneza lililoandikwa neno ‘Ebola’ yalitaka Serikali kufuta mpango huo mara moja.

Maandamano hayo yanafuatia mengine yaliyofanyika wiki iliyopita ambapo watu wawili walifariki dunia baada ya kupigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakiyatawanya.

Mpango wa Marekani wa kuanzisha kituo hicho umeibua hofu miongoni mwa wananchi kuhusu uwezekano wa maambukizi kuvuka mipaka, pamoja na kile kinachodaiwa kuwa ukosefu wa uwazi kutoka serikalini kuhusu shughuli zitakazofanyika katika kituo hicho.

Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru kusitishwa kwa uzinduzi wa kituo hicho baada ya wanaharakati wa haki za binadamu kufungua kesi wakidai mradi huo unaweka afya ya umma hatarini.

Kwa mujibu wa mpango huo, kituo chenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50 kitakuwa na wataalamu wa afya kutoka Marekani na kitatumika kuwahudumia Wamarekani watakaoathirika na mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais wa Kenya, William Ruto, ametetea mpango huo akisema alipokea ombi rasmi kutoka Marekani la kuanzisha kituo hicho na kulikataa ingekuwa kitendo kisicho cha kibinadamu.