Wanaharakati 20 wa chama cha siasa Kongo wauawa

Muktasari:

  • Washambuliaji wenye silaha nchini Kongo, wamewaua wanaharaki 20 wa masuala ya kisiasa mjini Lubumbashi.

Dar es Salaam. Zaidi ya wanaharakati 20 wa masuala ya kisiasa wameuawa katika mji wa Lubumbashi Kusini Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, vyama vyao na makundi ya kiraia yakieleza mauaji hayo kufanywa na washambuliaji wenye silaha.

“Baadhi ya makomandoo wameua zaidi ya watu 25 kwa risasi na wengine kuwazamisha kwenye maji,” amesema Bertin Tchoz, kiongozi wa shirika la kiraia la amani na usalama katika Wilaya ya Haut-Katanga mjini Lubumbashi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), watu waliopoteza maisha ni wanachama wa Muungano wa Kitaifa wa Wanaharakati wa Shirikisho la Kongo (UNAFEC).

Kiongozi wa UNAFEC, Jean Umba Lungange amesema mashambulizi  hayo yalitokea Ijumaa ya wiki iliyopita baada ya watu waliovalia sare za kijeshi kuwakuta wanachama wao kwenye mkutano wa hadhara na kuanza kuwafyatulia risasi.

"Wengine walipigwa risasi na wengine walizamishwa kwenye Mto Naviundu, mpaka sasa miili iliyopatikana ni 21 bado mingine,” ameeleza kiongozi huyo mbele ya waandishi wa habari.

Tayari meya wa eneo hilo, Martin Kazembe ameshaanzisha uchunguzi kubaini waliohusika na matukio hayo.

UNAFEC ni mwanachama wa Jukwaa la Muungano wa Kitaifa ulioanzishwa na Rais Felix Tshisekedi. Muungano huo umekumbwa na migogoro tangu mwasisi wake Gabriel Kyungu kupoteza maisha mwaka 2021.

Ongezeko la mashambulizi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha zaidi ya vifo vya watu zaidi ya 700 kwenye mikono ya wanamgambo tangu Desemba mwaka jana.