Wanajeshi 7 wauawa, wengine 18 wajeruhiwa Somalia

Muktasari:
- Wanajeshi 7 wadaiwa kuuawa na wengine 18 kujeruhiwa na wanamgambo wa Al Shabaab baada ya mabomu yaliliyotegwa ndani ya magari mawili kulipuka.
Somalia. Takribani wanajeshi saba wanadaiwa kuuawa na wengine 18 kujeruhiwa na wanamgambo wa Al-Shabaab baada ya mabomu yaliyotegwa ndani ya magari mawili kulipuka.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sauti ya Amerika (VOA), Naibu Gavana wa eneo la Gedo, Osman Haji, amesema wanajeshi hao wameuawa jana Juni 21, 2023 nje ya kambi ya mafunzo ya kijeshi katika mji wa Bardhere, Kusini mwa Somalia.
Mkuu wa Wilaya ya Bardhere, Mohamed Yusuf amesema vikosi vya usalama vya mkoa, vilizuia mabomu ya kujitoa muhanga yaliyokuwepo kwenye gari kuelekea kambi ya ulinzi.
“Tulikuwa tumepata taarifa za kiusalama kuhusu uwezekano wa mashambulizi na kuzuia magari ya kujitoa muhanga kufikia eneo hilo,” amesema Yusuf.
Ameendelea kueleza kuwa wanamgambo wenye itikadi kali wa Al-Shabaab wamedai kuhusika na shambulizi hilo wakisema maofisa wa Ethiopia na Somalia wanakutana katika kambi hilo.
“Tumelenga kambi hiyo kwa sababu maofisa wa Ethiopia na Somalia wamekuwa wakikutana huko,” ameeleza.
Hata hivyo mamlaka ya eneo hilo imekanusha madai hayo.
Machi 2023 shambulio kama hilo la bomu kutegwa ndani ya gari lililenga hoteli moja katika eneo hilo na kusababisha vifo vya wanajeshi kadhaa na wengine 10 kujeruhiwa.