Wanajeshi wa Israel waliouawa vita na Hamas wafikia 600
Muktasari:
- Tangu kuanza kwa vita kati Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas, tayari wanajeshi 600 wamekwishauawa.
Israel. Jeshi la Israel limesema tangu kuanza kwa vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas kutoka Palestina baada ya uvamizi wa Oktoba 7 mwaka jana, wanajeshi wake 600 wameuawa.
Idadi hiyo inafuatia kifo cha Nadav Cohen (20) aliyeuawa mwisho wa wiki hii huko Ukanda wa Gaza. Mashirika ya Habari ya AFP na Al Jazeera yameripoti.
Hayo yanajiri zikiwa zimetimia siku 178 tangu kuanza kwa mapigano hayo yaliyosababisha vifo zaidi ya 32,000 kwa upande wa Wapalestina na majeruhi kadhaa huku Israel ikidai kuwaua zaidi ya wapiganaji 10,000.
Wakati huohuo, Jeshi la Israel limejiondoa katika Hospitali ya al-Shifa iliyopo Gaza baada ya kuivamia tangu Machi 18. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema wagonjwa 21 wamefariki dunia tangu Israel ilipoanza kuzingira kituo hicho.
Hata hivyo, mashambulizi ya angani yameikumba tena Gaza huku mazungumzo kuhusu mapatano yakitarajiwa kuanza tena mjini Cairo, kwa mujibu wa televisheni ya Misri. Lakini si Israel wala Hamas walioonyesha matumaini.
Katika hatua nyingine ili kusaidia kupunguza mateso ya watu zaidi ya milioni 2.4 wa Gaza, meli ya misaada inaenda kutoa misaada ikitoka Kisiwa cha Kupro katika Bahari ya Mediterania, ikiwa na tani 400 za chakula.