Wanne warejea duniani baada ya kuishi anga za juu siku 168

Wanne warejea duniani baada ya kuishi anga za juu siku 168

Muktasari:

  • Chombo cha kampuni ya utafiti wa anga za juu ya SpaceX, kilichobeba wanaanga wanne kimerejea duniani na kutua Florida jana Jumapili asubuhi, ikiwa ni mara ya kwanza kutua usiku baharini.

Washington, Marekani. Chombo cha kampuni ya utafiti wa anga za juu ya SpaceX, kilichobeba wanaanga wanne kimerejea duniani na kutua Florida jana Jumapili asubuhi, ikiwa ni mara ya kwanza kutua usiku baharini.

Wanaanga hao wameripotiwa kuwa wanaendelea vizuri kiafya baada ya kurejea duniani baada ya kuwa katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) kwa miezi sita, taasisi ya NASA ilisema.

Wanne warejea duniani baada ya kuishi anga za juu siku 168

Chombo hicho kilitua saa 8:56 usiku katika ghuba ya Mexico nje ya Panama City baada ya kusafiri kwa saa sita-na-nusu kutoka ISS, picha za usiku zilizotolewa na NASA zinaonyesha.

Timu zilizokuwa katika meli ya Navigator zilikivuta chombo hicho na kukipakia melini kwa karibu saa moka-na-nusu baadaye. Kwa NASA, hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha anga za juu kutua usiku tangu wanaanga waliokuwa katika chombo cha Apollo 8 walipotua Bahari ya Pacific Desemba 27, 1968.

Kamanda Michael Hopkins alikuwa wa kwanza kushuka baada ya mlango wa chombo hicho mithili ya yai kufunguliwa, akijaribu kunyanyua miguu melini, na muda mfupi baadaye kufuatiwa na mwanaanga mwenzake wa NASA, Victor Glover.

"Kwa niaba ya wanaanga na familia zetu, tunataka tuseme tu asante ... Ni kitu cha kufurahisha kwa kile tunachoweza kufanikisha wakati watu wakishirikiana. Wote mnaibadili dunia. Hongera. Ni kitu kizuri kurejea," Hopkins alisema katika ujumbe wa NASA uliotumwa Twitter.

Mwanaanga wa NASA, Shannon Walker na Mjapani Soichi Noguchi ni watu wengine waliokuwa katika chombo hicho.

Maili milioni 71
Wanaanga hao wanne walienda anga za juu Novemba mwaka jana wakiwa katika mpango wa kwanza kamilifu wa kikazi katika kituo cha ISS wakitumia chombo kilichotengenezwa na kampuni ya SpaceX inayomilikiwa na Elon Musk. SpaceX imekuwa mshirika ambaye NASA inaonekana kupenda kufanya naye usafirishaji wa kibiashara kwenda anga za juu.

Wanaanga hao walisafiri maili milioni 71.2 (sawa na kilomita milioni 114.6) ndani ya siku 168 walizokuwa katika mzingo wa dunia (zikiwemo siku 167 walizokuwa katika kituo hicho cha anga za juu), NASA ilisema.

Wanne warejea duniani baada ya kuishi anga za juu siku 168


Baada ya uchunguzi wa kiafya, wanaanga hao wanne walitarajiwa kusafirishwa kwa helikopta kwenda Pensacola kwa ajili ya kupanda ndege ya kuwapeleka Houston kuungana tena na familia zao na marafiki, NASA ilisema.

Kabla ya safari yao, wanaanga wawili wa Kimarekani walifanya majaribio ya kwenda ISS mwezi Mei na kuishi huko kwa miezi miwili.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kuanzisha safari ya kwenda ISS kutokea ardhi ya Marekani tangu mwaka 2011. Pia ilikuwa ni safari ya kwanza iliyojumuisha wanaanga kuendeshwa na kampuni binafsi, tofauti na za NASA.