Watu 141 wafa baada ya daraja kuporomoka India

Muktasari:

Watu 141 wamefariki dunia baada ya daraja linalotumiwa na waenda kwa miguu kuvunjika katika jimbo la magharibi la Gujarat nchini India.

Dar es Salaam. Watu 141 wamefariki dunia baada ya daraja linalotumiwa na waenda kwa miguu kuvunjika katika jimbo la magharibi la Gujarat nchini India.

Vyombo vya habari vya kimataifa vmeripoti kuwa mamia ya watu waliotumbukia katika mto Macchu ulioko kwenye mji wa Morbi walikuwa wakipiga kelele kuomba msaada huku wengine wakining'inia kwenye kingo za daraja lililokuwa likizama mtoni.

Waziri wa Kazi na Ajira kwenye jimbo hilo la Gujarat Brijesh Merja amesema kuwa zaidi ya watu 80 wameokolewa, katika daraja hilo ambalo wakati likipasuka kulikuwa na watu 400.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya daraja hilo kufunguliwa tena, kufuatia ukarabati uliokuwa ukifanywa.

Daraja hilo lililojengwa katika karne ya 19, lina urefu wa mita 230 na ni maarufu kama kivutio cha utalii katika eneo hilo.

Tarifa zinasema kuwa kulitokea mtafaruku watu wakijaribu kujiokoa baada ya kutumbukia mtoni na wengine kukwamba katika kingo za daraja hilo refu kwenda juu, wakati giza likiingia.

Juhudi za uokoaji zimefanyika usiku kucha. Bado chanzo cha kuvujika kwa ajali hiyo hazijafahamika, lakini mamlaka za eneo hilo zinasema msongamano wa watu katika daraja hilo wakati huu wa msimu wa sikukukuu ya Diwali inaweza pia kuwa sababu.