Waziri Mkuu DRC ajiuzulu, Rais Tshisekedi kuunda serikali mpya

Muktasari:

  • Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilifanya uchaguzi Desemba 20, 2023 ambapo Rais Felix Tshisekedi alifanikiwa kushinda uchaguzi huo. Wabunge wengi kutoa kwenye muungano wake pia walichaguliwa kwenye uchaguzi huo uliolalamikiwa na wapinzani.

Kinshasa. Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean-Michel Sama Lukonde, amejiuzulu wadhifa huo, hivyo kusababisha kuvunjwa kwa ya nchi hiyo, Ofisi ya Rais imeeleza kwenye taarifa yake.

Waziri Mkuu huyo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais, Felix Tshisekedi Jumanne iliyopita zikiwa ni siku nane baada ya kuthibitishwa kwa mamlaka yake kama kiongozi wa shughuli za Serikali.

Hata hivyo katika barua yake ya kujiuzulu, amechagua kutumikia kama mbunge wa kawaida.

Ni takwa la kisheria nchini humo, ambapo mawaziri hawatakiwi kuwa wabunge, ikimaanisha kwamba mtu anapaswa kuchagua kubaki mbunge au kujiuzulu ili aitumikie serikali.

“Kujiuzulu kwake kumekubaliwa. Hata hivyo, Rais ameiomba Serikali (ya Lukonde) kuendelea kushughulikia masuala ya sasa hadi serikali mpya itakapoundwa,” Ofisi ya Rais ilisema.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Ikulu haikueleza sababu za Lukonde kujiuzulu wadhifa huo, wakati Taifa hilo likikabiliwa na mapigano katika eneo la Mashariki.

Lukonde aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo yenye utajiri wa madini Februari, 2021.

Baada ya kuchaguliwa tena Desemba 20, 2023, Rais Tshisekedi alimteua mwanasiasa huyo kwa lengo la kuunda Serikali ijayo.

Sama Lukonde (46), amekuwa madarakani kwa miaka mitatu. Aliteuliwa kuwa waziri mkuu Februari 15, 2021 baada ya muungano wa Rais wa zamani, Joseph Kabila na wa Félix Tshisekedi kuvunjika.

Kujiuzulu kwa Lukonde kunamaanisha kuwa Serikali yake yote sasa imevunjika, hivyo Rais Tshisekedi ana kazi ya kuunda mpya.

Jumla ya mawaziri 39 wa Serikali ya Congo walichaguliwa hivi karibuni kuwa wabunge. Watahudumu kwa miaka 5 ijayo. Hapo awali, Naibu Waziri Mkuu anayehusika na Uchumi na Naibu Waziri Mkuu anayesimamia utumishi wa umma waliwasilisha ombi la kujiuzulu.

Félix Tshisekedi anajiandaa kuunda serikali mpya kuanza muhula wake wa pili.

Hata hivyo, baadhi ya mawaziri waliojiuzulu huenda wakawa sehemu ya timu hiyo mpya kwa vile ni wabunge wengi katika muungano wa Rais Tshisekedi.

Tofauti katika muhula wake wa kwanza, alipolazimishwa kugawana madaraka na muungano wa Joseph Kabila, Tshisekedi hatarajiwi kupata upinzani mkali wakati huu.

Anatarajiwa kushinda zaidi ya viti 400 kati ya 500 katika Bunge la Kitaifa. chama cha mpinzani wake Moïse Katumbi kina wabunge takriban 20, wakati muungano wa Kabila ulisusia uchaguzi.

Martin Fayulu, ambaye alisusia uchaguzi, hana wabunge. Fayulu amewataka  wanachama wake kususia uchaguzi huo. Ilibidi abadili uamuzi wake, lakini aliendelea kutaka uchaguzi wa wabunge usogezwe mbele.