Waziri wa Mambo ya Ndani afariki ajali ya helikopta Ukraine

Muktasari:

  • Watu 18 wamefariki dunia kwa ajali ya Helkopta nchini Ukraine, huku Waziri wa Mambo ndani nchini humo akiwa miongoni mwa waliofariki pamoja na watoto wawili na maafisa wakuu kadhaa wa wizara hiyo.

Dar es Salaam. Watu 18 akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine na watoto wawili pamoja na maafisa wengine wakuu wa wizara wamefariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wamepanda kuanguka nje ya mji mkuu wa Kyiv nchini humo.

 Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘Aljazeera’ wameeleza kwamba taarifa hiyo ilithibitishwa na Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo, Igor Klymenko, ambapo alisema, “Miongoni mwa waliofariki ni maafisa wakuu kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Ndani akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Denys Monastyrsky.”

Waziri Monastyrskyi aliteuliwa chini ya Zelenskyy mwaka 2021 na alikuwa mtu muhimu katika baraza la mawaziri.
Monastyrsky, ambaye alikuwa anahusika na masuala ya polisi na usalama ndani ya Ukraine, ndiye afisa mkuu wa Ukraine aliyekufa tangu vita kuanza.
Gavana wa Mkoa wa Kyiv amesema kwamba helikopta ilianguka karibu na kitalu na jengo la makazi leo Januari 18.
Hata hivyo walieleza kwamba watoto wawili walikuwa miongoni mwa waliofariki na 10 kati yao wanapatiwa matibabu.

Wakati hatua za uokoaji zikiendelea mke wa Rais wa Ukraine, Olena Zelenska amewataka wajumbe katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos kufanya zaidi kusaidia kumaliza vita, wakati huo Rais Volodymyr Zelenskyy akitarajia kuzungumza katika kongamano hilo.