Wito na maandamano ya wapinzani yanavyoitikisa Afrika

Maandamano yaliyowahi kutokea Afrika Kusini, picha na BBC

Muktasari:

  • Mbali na wito na maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa azimio la umoja ambaye ni waziri mkuu wa zamani na mpinzani mkubwa wa Rais William Ruto, Raila Odinga kuwataka wafuasi wake kufanya maandamano kuelekea Ikulu ya Kenya kwa ajili ya kumtaka Ruto ajiuzulu katika nchi nyingine ya Afrika Kusini, Nigeria na Tunisia pia kuna vuguvugu hilo linalotishia amani ya nchi hizo.

Mbali na wito na maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa azimio la umoja ambaye ni waziri mkuu wa zamani na mpinzani mkubwa wa Rais William Ruto, Raila Odinga kuwataka wafuasi wake kufanya maandamano kuelekea Ikulu ya Kenya kwa ajili ya kumtaka Ruto ajiuzulu katika nchi nyingine ya Afrika Kusini, Nigeria na Tunisia pia kuna vuguvugu hilo linalowakosesha usingizi watawala wa nchi hizo.

Nchini Kenya, kiongozi huyo wa upinzani amekua akiitia tumbo joto serikali inayoongozwa na Ruto tangu kumalizika kwa uchaguzi mwaka jana, baada ya tume kumtangaza William Ruto kuwa ndiye mshindi hata baada ya kesi kwenda mahakamani.

Hivi karibuni Raila amekuwa akifanya mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini humo akiwapa maagizo wafuasi wake kutotumia bidhaa zinazozalishwa na kampuni zenye uhusiano na serikali kama vile mayai.

Haikuishia hapo Raila aliamua kuitisha maandamano kwenda Ikulu hapo siku ya Jumatatu Machi 20, baada ya madai yake kuwa Ruto ameshindwa kushusha gharama za maisha na hafai kuendelea kuwa Rais wa nchi hiyo.

“Kuanzia leo Wakenya wanaweza kugoma, au kuandamana na kuenda katika nyumba yoyote ya serikali kupelekea malalamishi yao," alisema Raila alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

Japokuwa kauli yake Raila imepata upinzani kutoka kwa watu mbalimbali kama Wakili maarufu wa masuala ya katiba PLO Lumumba aliyemshutumu Raila kuwa mpango wake huo ni uhaini na ni jaribio la kuipindua serikali lakini Raila amekaza msimamo wake.

Lumumba akionyesha wasiwasi wake wakati akifanya mahojiano kwenye kipindi cha JK Live cha Citizen Tv alisema kuwa iwapo Raila na wafuasi wake watatekeleza vitisho vyao vya kuvunja Ikulu, basi mambo yataka mabaya zaidi.

“Kama kutakuwa na maandamano mnamo Machi 20 na Mungu apishe mbali kundi hilo la watu kufanikiwa kuingia Ikulu na iwapo mtu atapigwa risasi na kuuawa na kukitokea mkanyagano, kutatokea umwagaji damu na Kenya haitakuwa sawa tena, nini kitatokea tarehe 21? Mwisho ni upi?"

Huko Afrika Kusini kiongozi wa chama cha, The Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema ameitisha maandamano kote nchini siku ya kesho Jumatatu Machi 20 akiishinikiza serikali ya Rais Cyril Ramaphosa kung’oka madarakani kwa kile kinachodaiwa kushindwa kudhibiti mgao wa umeme uliogeuka janga katika nchi hiyo.

Februari 9 mwaka huu Ramaphosa alitangaza janga la kitaifa kutokana na uhaba wa umeme nchini humo, akisema unaleta tishio taifa hilo lililoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika.

Katika hotuba yake ya kila mwaka aliyoitoa bungeni siku ya Alhamisi, Ramaphosa alikiri kuwa wako kwenye mzozo mkubwa wa kinishati huku akiulaumu ufisadi.

Katika hotuba hiyo ilishuhudiwa upinzani mkubwa dhidi ya wabunge wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) waliovuruga shughuli kwa zaidi ya dakika 45 huku wengine wakijaribu kupanda jukwaani.

Malema alisema wakati akiongea na waandishi wa habari kuwa ataitisha maandamano licha ya vikwazo vilivyopo kwasababu ni haki yao ya kikatiba, kuongezeka kwa uhalifu na ukosefu mkubwa wa ajira, na mgao wa umeme ni miongoni mwa baadhi ya sababu za kuitisha maandamano nchini humo.

Nchini Tunisia kuna vuguvugu ambapo utawala wa Rais Kais Saied hauna amani huku upinzani ukipanga zaidi kufanya maandamano dhidi ya utawala wake.

Upinzani umekataa kutambua uhalali wa bunge lililoapishwa hivi majuzi, Mamia ya wafuasi wa upinzani nchini Tunisia wamekaidi katazo la maandamano na wanataka kuachiliwa kwa watu mashuhuri zaidi ya 20 ambao wamekamatwa katika wiki za hivi karibuni.

Saied alivunja bunge lililochaguliwa mwaka 2021 na kuanza kufanya mabadiliko ya kiholela kwa mfumo wa kisiasa lakini uchaguzi wa wabunge wa Desemba mwaka jana ulionyesha uungwaji mkono mdogo wa umma kwa mabadiliko yake.

Mnamo Machi 4 na 5, maelfu ya Watunisia waliingia barabarani dhidi ya serikali ya Rais Kais Saied, waandamanaji hao yaliyondaliwa na vyama viwili wa upinzani, kikiongozwa na kile cha Ennahdha na National Salvation Front, walikuwa wakipinga ongezeko la majaribio ya serikali ya kunyamazisha upinzani kwa vitisho vya kukamatwa na kushindwa kwake kushughulikia masuala ya msingi ya kiuchumi ya watu.

Makundi makubwa ya kisiasa na jumuiya ya wafanyakazi wanapinga mabadiliko hayo ambayo Saeid ana mpango wa kuyatekeleza, huku wengi wanabashiri mapinduzi ya kidemokrasia.

Mbali na changamoto za kisiasa, baada ya kiongozi huyo kulifuta bunge na kubadilisha katiba, ili kuwa na madaraka makubwa, raia wa Tunisia pia wameendelea kulalamilkia hali ngumu ya kiuchumi, wakati huu watu wakikosa mahitaji ya msingi.

Kwingineko huko Nigeria viongozi wa upinzani bado wako kwenye vuguvuvgu la kupinga matokeo yaliyoshuhudia Bola Tinubu wa chama cha All Progressives Congress (APC) akitangazwa mshindi wa urais.

Kiongozi wa upinzani nchini Nigeria Atiku Abubakar ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais uliofanyika Februari 25, tayari amefanya maandamano na wafuasi wake kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Peter Obi wa Chama cha Labour, ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo, pia amekataa matokeo hayo, na kusema anaenda mahakamani kuwathibitishia Wanigeria kwamba alishinda kinyang'anyiro cha urais.