BQ: Ushindi Top 100 umetuongezea wateja, kukuza biashara ya kampuni

Muktasari:

Mwaka 2011 kampuni ya ukandarasi ya BQ ilishiriki mashindano ya kwanza ya kampuni za kati (Top 100) na kuibuka mshindi wa jumla na hadi sasa imeshapata zaidi ya miradi 40 iliyoitekeleza kwa ufanisi na kuongeza mapato yake zaidi ya mara tano.

Bila kujua kitakachotokea wakati inashiriki mashindano ya kwanza ya kampuni za kati (Top 100) mwaka 2011, kampuni ya BQ Contractors inasema mapato yake kwa mwaka yameongezeka zaidi ya mara tano ndani ya miaka saba iliyopita.

Kampuni hiyo ya ukandarasi iliibuka mshindi wa jumla mwaka huo wakati na mpaka sasa imeshapata zaidi ya miradi 40 iliyoitekeleza kwa ufanisi hivyo kuongeza wingi wa mapato yake.

Mmiliki na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, John Bura anasema baada ya kuwa mshindi mwaka 2011 wamekuwa na mafanikio makubwa yanayowatia moyo.

Anasema wakati wanashiriki hakufikiria kama kampuni hiyo ingeibuka mshindi wa jumla kutokana na usiri uliopo katika mchakato wa kumpata mshindi na anaiona chapa ya Top 100 kama jambo muhimu katika ukuzaji wa biashara na si tuzo ambayo kila mtu anaweza kuipata kwa urahisi.

“Nina ushahidi juu ya manufaa ya ushiriki katika shindano hili, mara baada ya ushindi miradi mingi ilikuja na tumekuwa hatukosi walau zabuni mbili kubwa kwa mwaka,” anasema Bura.

Mafanikio hayo, anasema yalianza kuonekana siku chache baada ya shindano pale kampuni ya Puma ilipotangaza zabuni ya kujenga bomba la mafuta kutoka bandarini hadi yalipo matanki yao (depot).

Ingawa kampuni nyingi za ndani na nje ziliomba zabuni hiyo na bei ya BQ Contractors ikaonekana ni kubwa, lakini waliombwa wapunguze kwani Puma walitaka kufanya kazi na mshindi wa Top 100.

Huo ulikuwa mwanzo tu. Siku chache baadaye kampuni hiyo ilipata zabuni ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kusambaza mabomba ya gesi kutoka Ubungo kwenda viwandani maeneo ya Mikocheni na nyumba 70. Ulikuwa ni mkataba wa Dola 3.5 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh7.87 bilioni).

Licha ya TPDC, kampuni hiyo pia ilipata kazi ya kujenga bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi kilipo kiwanda cha saruji cha Dangote, umbali wa kilomita tatu. Ni mradi uliogharimu Dola 3.72 milioni (zaidi ya Sh8.37 bilioni) na ulikamilika Septemba.

Mradi mwingine ambao BQ waliupata baada ya ushindi wa Top 100 ni mkataba wa miaka miwili wa kufanya matengenezo ya mitambo ya kampuni ya Pan African Energy (Songas) na hivi karibuni wakajenga kambi za Ilala, Soga na Ngerengere zinazotumiwa na mkandarasi anayejenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Cheti cha ISO

Licha ya miradi hiyo zaidi ya 40 iliyopata kampuni hiyo iliyojikita kwenye uhandisi wa mafuta na gesi imepewa cheti cha ubora wa kimataifa ISO 9001:2015 hivyo kuongeza imani ya wateja wengi.

“Kupata hiki cheti ulikuwa ni mpango wetu na sio rahisi kupata hii ithibati inaweza kuchukua hata miaka miwili,” anasema Bura.

Mhandisi huyo anasema licha ya mafuta na gesi huwa wanafanya kazi nyingine kama ujenzi wa barabara na majengo pamoja na miundombinu ya umeme. Kutokana na shughuli wanazofanya, anasema wanatarajia kukua kwa walau asilimia 25 kwa mwaka kutoka ukuaji wa asilimia 20 sasa hivi.

“Miradi ya mafuta na gesi ni michache na ina ushindani mkubwa, wenye nayo wana imani kubwa na kampuni za kigeni kuliko za ndani. Kidogo baada ya Top 100 tulianza kuaminika na kushirikishwa katika miradi hiyo,” anasema Bura.

Kabla ya mwaka 2011, kampuni hiyo ilikuwa na chini ya wafanyakazi 30 lakini hivi sasa inao zaidi ya 200 wakiwamo 70 wa kudumu.

Hivi sasa, Bura anasema kampuni inatarajia kuongeza zaidi rasilimali watu wakiwamo wanaohitimu mafunzo ya uhandisi ili kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana nchini na kuongeza ufanisi.

Mipango ya baadaye

BQ inapanga kubadili muundo wake wa umiliki kutoka kuwa kampuni ya familia na kuwa ya umma kwa lengo la kuongeza uwazi katika masuala ya fedha na kujenga imani zaidi kwa wateja wake.

Bura anasema kampuni inatarajia kuendelea kujiimarisha kwa kumiliki vifaa vyake kwani vya kukodi huwapunguzia faida na wakati mwingine kuimaliza kabisa. Kutokana na changamoto ya mtaji iliyopo, anasema BQ itaendelea kutafuta wabia wenye mtaji mkubwa ili wafanye kazi kwa pamoja ukiwa ni mkakati wa kuhakikisha kampuni inashiriki katika miradi mikubwa.

Mpango huo anasema utaisaidia kampuni hiyo kukabiliana na changamoto kubwa ya ukosefu wa mtaji wa kutosha kuweza kutekeleza miradi mikubwa wenye faida zaidi.

Kuhusu miradi, kampuni hiyo inaamini itaendelea kushinda zabuni mbalimbali kutokana na uaminifu wake katika kazi zilizopita