‘Carbetocin’ yatajwa suluhisho kupunguza vifo vya wajawazito

Musoma. Serikali imeshauriwa kuingiza aina mpya ya dawa ‘Carbetocin HS’ kwenye orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu (STG/NEMLIT) ili kupunguza vifo vya wajawazito vinavyoweza kuzuilika hasa vile vitokanavyo na kuvuja damu nyingi.
Kuvuja damu baada ya kujifungua (PPH) humfanya mama kupoteza zaidi ya milimita 500 au 1,000 za damu ndani ya saa 24 za baada ya mtoto kuzaliwa ambayo bado inachangia idadi kubwa ya vifo.
Dawa ambazo zimekuwa zikitumika na zipo katika orodha ya taifa ya dawa muhimu kwa miaka mingi ni Oxytocin na misoprostol ambazo hata hivyo, wataalamu hao wamesema zina ufanisi mdogo na kushauri mbinu bora zinazoibukia za kimataifa katika kudhibiti vifo hivyo.
Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Wanawake na Madaktari wa Uzazi Tanzania (AGOTA) walikutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari kujadiliana njia bunifu za kupunguza vifo vya wajawazito nchini kwa kujadili hatua stahiki za kuchukua.
Pendekezo lililotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kupambana na changamoto hiyo kati ya 2023 na 2030 ni aina hiyo ya dawa iliyotengenezwa baada ya kugundua juhudi za kimataifa za kukabiliana na PPH hazijafanikiwa katika muongo mmoja uliopita.
Dawa hiyo mpya Carbetocin (HSC) na tranexamic acid (TXA) ambazo zimegunduliwa kuwa na ufanisi kupambana na kuvuja kwa damu.
Mkurugenzi Msaidizi, seksheni ya afya ya uzazi na mama, idara ya afya ya uzazi, mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Mzee Nassoro alisema dawa hizo bado hazijaingia kwenye mwongozo.
"Serikali lazima ijiridhishe kwanza katika upatikanaji wake, bei na iwapo kuna uwezekano wa kupatikana kirahisi, uhifadhi wake utakuwaje na iwapo tutaweza kugharamia ununuaji na kama kitakua pia na dawa mbadala wa hiyo," alisema Dk Mzee.
Wakati Serikali ikitoa msimamo huo, nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa ni pamoja na Tanzania bado zinakabiliwa na changamoto katika kubadili miongozo yao ya kitaifa na orodha za dawa muhimu ili kujumuisha dawa hizo zinazopendekezwa na WHO.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na uzazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Lilian Mnabwiru, alisema, udaktari unabadilika na ipo haja ya kuboresha jinsi tunavyowatibu wagonjwa.
“Kwa miaka mingi, tumekuwa tukitegemea matumizi ya dawa za uterotonic kama vile Oxytocin lakini katika miaka ya hivi karibuni WHO ilipendekeza matumizi ya Carbetocin ambayo inaweza kuhimili joto na matumizi ya tranexamic acid (TXA). Haya yanahitaji kujumuishwa katika miongozo ya kitaifa ili kuharakisha juhudi za kupunguza vifo vya uzazi,” alisema.
Katika mada aliyoitoa Dk Mnabwiru aliangazia sababu nyingine kubwa za vifo vya uzazi nchini Tanzania pamoja na kutokwa na damu nyingi. Wao ni pamoja na eclampsia, maambukizi ya njia ya uzazi ya mwanamke na utoaji mimba.
Makamu wa Rais wa AGOTA, Dk Chetan Ramaiya alisema ipo haja ya uboreshaji wa mwongozo uliopo kwa kufuata kanuni bora mpya zenye matokeo.
"Lakini kuna nafasi ya kuboresha. Ni muhimu kama nchi, tukaboresha miongozo yetu ya matibabu ili kuendana na dawa mpya za kuokoa maisha na afua ambazo zimeonyesha ufanisi katika kupunguza vifo vya uzazi,” alisema.
Dk Ramaiya alisema kupitishwa kwa kanuni bora kama inavyoshauriwa kutasaidia juhudi zinazoendelea katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali na mbinu nyinginezo pamoja na uwekezaji wa serikali na ushirikiano na wataalamu wa afya ya uzazi katika kudhibiti vifo.
Vifo vya uzazi vimeendelea kuwa juu nchini Tanzania, huku takwimu za mwaka 2017 zikionyesha kuwa vifo 524 bado vinatokea kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa, huku wengi wao wakichangiwa na matatizo yanayohusiana na kuvuja damu nyingi.
Januari mwaka huu WHO ilitoa makadirio ya kimataifa ya MMR na kwa Tanzania sasa ni vifo 238/100000 na kikomo cha chini ni 174/100000 na kikomo cha juu ni 381/100000, hali inayoonyesha kuwa vifo vimekuwa vikipungua kwa kasi lakini polepole kwa miaka.
Hata hivyo, ni hadi pale Utafiti mpya wa Demografia na Afya Tanzania utakapotolewa ndipo takwimu halisi kuhusu vifo vya uzazi nchini Tanzania inaweza kufichuliwa.
Rais wa AGOTA Dk Yahaya Kapona alisema dawa mpya iliyopendekezwa (carbetocin) ni dawa ya kuokoa maisha ambayo inaweza kusaidia kupunguza matatizo makubwa ya PPH ambayo hupoteza maisha ya akina mama wengi nchini Tanzania.
"Ni dawa nzuri sana ambayo inaweza kukata damu ndani ya dakika chache baada ya mgonjwa kupewa," alisema.
Dk Kapona alisema ingawa dawa hiyo mpya ni ya gharama kubwa ikilinganishwa na dawa za kawaida zinazotumika kama vile oxytocin na misoprostol, kuna fursa kwa hospitali za umma kuinunua kwa bei ya ruzuku kwa msaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa.
Mwanzilishi mwenza wa RESEARCHCOM, shirika la mawasiliano la utafiti, Dk Syriacus Buguzi alisema vyombo vya habari na waandishi wa habari wana jukumu la kutekeleza katika kuhabarisha umma na watunga sera kuhusu sayansi ya matibabu inayoendelea kuhusu afya ya uzazi.
Kwa mujibu wa Dk Mzee, alisema wamekuwa wakipambana na hilo kwa kutoa dawa za madini chuma kwa wajawazito na minyoo katika umri wote wa mimba.
Na baada ya kujifungua mwongozo unasema kinamama wote wapate dawa za kuwafanya wasitoke damu nyingi ndani ya dakika moja baada ya kujifungua.
"Dawa ya kwanza apewe oxitocine kama hamna inabidi apewe misoprotol akiendelea kutokwa anapewa moja iliyokuwepo kama hamna atapewa misoprotol au kama amepewa hizo dawa damu zinaendelea kutoka lazima apewe zaidi ya moja pamoja na mambo mengine.