Chadema, ACT-Wazalendo wanapigana vita wakati mbaya

Muktasari:

  • Karne ya 20 (katikati), aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN), Jenerali Douglas MacArthur, alipendekeza kwa Serikali ya Marekani kuendeleza uchochezi kwenye vita ya Korea na China kama njia muhimu ya kuutokomeza ukomunisti.

Dar es Salaam. Karne ya 20 (katikati), aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN), Jenerali Douglas MacArthur, alipendekeza kwa Serikali ya Marekani kuendeleza uchochezi kwenye vita ya Korea na China kama njia muhimu ya kuutokomeza ukomunisti.

Hata hivyo, mbele ya jopo la wanadhimu wa majeshi ya Marekani, katika mkutano ambao ulihudhuriwa pia na aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Harry Truman, aliyekuwa kamanda Nyota-5 wa Jeshi la Marekani, hayati Omar Nelson Bradley alipingana na wazo hilo la kuchochea Vita ya Korea na China.

Bradley alisema kuwa uchochezi huo wa vita ya China na Korea ni “wrong war, at the wrong place, at the wrong time, and with the wrong enemy.” – “Vita batili, katika eneo batili, katika muda batili na dhidi ya adui batili.”

Kwamba nyakati hizo, Marekani kama baba wa ubepari, ilipaswa kujielekeza kupambana na Umoja wa Dola ya Kisovieti (USSR). Kujiingiza kwa Wachina na Wakorea, ilikuwa ni kupoteza rasilimali fedha, muda na watu, tena zaidi mafanikio yasingeonekana.

Si kwamba China na Korea hawakuwa maadui kwa Marekani, hapana, ila ni maadui wadogo. Katika vita unapaswa kuangalia mshindani wako hasa ni nani na kujiondoa kwenye kupambana na maadui wadogowadogo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa muda mrefu walipigana vita batili, katika eneo batili, katika muda batili na dhidi ya adui batili.

Walinyukana wao kwa wao kwelikweli. Walishindwa kutambua kuwa upo umuhimu wa kushirikiana dhidi ya adui yao. Kwamba wao wote ni wapinzani, kwa hiyo wanatakiwa kulenga shabaha zao kwa mtawala.

Wakapigana vita wao kwa wao kutafuta ukuu wa upinzani. Wakasahau kuwa upinzani wenye nguvu ndio unaweza kuiteteresha serikali. Hujuma na kuhujumiana wao kwa wao, kushambuliana wenyewe kwa wenyewe ni kuufanya upinzani upoteze nguvu ya kutosha.

Zitto na Mbowe walivurugana wakiwa chama kimoja (Chadema), kisha Zitto akavuliwa uongozi na baadaye akakihama chama hicho. Alipohamia ACT-Wazalendo, mapambano yanaendelea. Walifumuana kipindi Mwenyekiti wa CCM ni Jakaya Kikwete, wakawa na vipindi vya kuelewana na kupigana nyakati za Dk John Magufuli, sasa moto unawaka usukani ukiwa umeshikiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Zitto, vilevile ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Kwa mwavuli wa TCD, hivi karibuni akawasilisha ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la Mbowe na kulimaliza kwa njia ya maridhiano.

Kauli ya Zitto ikaibua zogo. Anashambuliwa kuwa hakutakiwa kumwombea Mbowe msamaha, kwani mashtaka dhidi yake ni ya kutengenezwa. Mwisho kabisa, dhamira na tafsiri ya alichokisema Zitto imekuwa tofauti kwenye masikio ya wana-Chadema, hususan mitandaoni.

Mbowe yupo mahabusu akishtakiwa kwa makosa ya ugaidi na kufadhili kikundi cha kihalifu kwa lengo la kudhuru viongozi. Wanasiasa wengi wanaamini hayo ni mashtaka ya kisiasa.

Je, upo ubaya mtu kuomba maridhiano? Kauli ya Zitto ililenga kujipatia umaarufu wa kisiasa? Na katika suala la Mbowe, mbaya ni nani?

Tatizo ni tafsiri. Pengine aliyoyasema Zitto mbele ya Rais Samia yangetamkwa na mwingine wala lisingekuwa jambo baya. Si ajabu kusingekuwa na malumbano mitandaoni ya Zitto na Chadema au ACT-Wazalendo dhidi ya Chadema.

Tatizo lipo pia kwa Zitto. Kukosa subira. Alipoanza kushambuliwa, naye akaibuka kujibu. Akamwingiza mpaka Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika. Ni rahisi kutambua kuwa lengo la Zitto kumtaja Mnyika ni kuonyesha kwamba alichokisema yeye kwa Rais Samia ndio ulikuwa msimamo wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Hata hivyo, Zitto angenyamaza bila kujibu chochote, pengine angesaidia kupunguza tafsiri ya ushindani wa vyama. Ikawa Chadema dhidi ya Zitto. Baina ya ACT-Wazalendo na Chadema. Ni vita batili. Adui batili. Na wakati ambao si sahihi.

Chadema na ACT-Wazalendo wanapitia mazingira yanayofanana kisiasa. Hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kisiasa na wote kilio chao ni Katiba Mpya. Utaona kwamba wala vyama hivyo si maadui. Isipokuwa wanachangia adui.

Watu wenye kuchangia adui huwa hawapigani wenyewe, bali wanajielekeza kwa adui. Hata kama hakuna kushirikiana lakini ukiwa Mashariki na wewe Magharibi halafu adui akiwa katikati, hapo ni kurusha mishale tu mpaka adui anachanganyikiwa.

Mshale ukimgonga kutoka Mashariki, akitimua mbio kuelekea Mashariki, mshale mwingine unamchoma mgongoni kutokea Magharibi. Anachanganyikiwa aende wapi? Mwisho adui anaishiwa nguvu.

Hii ndiyo sababu mara nyingi vyama tawala hutumia mbinu nyingi, ikiwemo za kijasusi au kimabavu ili wapinzani wasiwe imara. Vyama tawala huwa vinapenda kuwepo na nafasi (gape) kubwa ya kiushindani kati yao na wapinzani. Mshikamano wa upinzani huwa na athari kubwa kwa nchi na huwafanya watawala wapepesuke.

Kwa siasa za Afrika ni rahisi mno kusikia wapinzani wenye nguvu wakishutumiana kwa usaliti. NCCR-Mageuzi leo kingekuwa na nguvu ileile ya miaka ya 1990, sipati picha siasa za Tanzania zingekuwa na sura gani. Hata hivyo kiliuawa kwa wimbo wa kusalitiana.

Mtunzi wa wimbo “usaliti wa Zitto” hupati shida kumtambua. Mtunzi wa wimbo “Chadema ya Wachaga” au “Chadema Saccos ya Edwin Mtei na Mbowe” yupo. Ila waliokariri nyimbo ndiyo wakaziimba kwa bidii kubwa mithili ya msanii wa American Idol au Bongo Star Search. Wakasahau nyimbo zina watunzi wao na walitunga kwa sababu maalumu. Wakaziimba kama zao.

Watu hawajui kuwa mtu akiwa anataka kununua nyumba yenu ya urithi kwa bei nafuu au kama hapendi kuona mnavyoelewana na kushirikiana, anaweza kuwachonganisha kisha moto ukiwaka, ndipo unasikia “tuuze nyumba tugawane kila mtu afe na chake”, bila kujua kuwa ugomvi wenu ni mafanikio ya mchonganishi. Mara nyumba inachorwa “epuka matapeli nyumba hii haiuzwi.”

Vita ya Chadema na ACT inawanufaisha mno CCM. Wapinzani wanapogombana wao kwa wao, maana yake wanakuwa wanaushambulia upinzani, hivyo chama tawala kinajitanua kama siyo kujinafasi vizuri. Ni vita batili katika wakati mbaya.