DAS awatolea uvivu watumishi wazembe Tanga

Muktasari:

  • Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amemtaka Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini kuwachukulia hatua watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

  

Tanga. Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amemtaka Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini kuwachukulia hatua watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Mnyema amesema hayo leo Alhamisi Juni 16, 2022 wakati akizungumza katika Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo walipokutana kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

"Itakuwa ni aibu kusubiri mimi nitoke mkoani nije hapa kuchukua hatua. Tuache kufanya kazi kwa mazoea kama tumelala maana yake hatutoshi na kama hutoshi maana yake utupishe.

"Kama Katibu Tawala siwezi kukubali kuharibu kibarua changu kwa ajili ya watu wachache," amesema.

Aidha, amewataka madiwani hao wakati wa kujadili wasikubali hoja zisizo na mashiko zibaki kwenye makabrasha yao ili waendelee kuweka imani kwa wananchi waliowachagua.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mussa Mwanyungu amesema  wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa upungufu wa watumishi wa afya pamoja na elimu hali ambayo inachangia ukosefu wa huduma bora.

Ametolea mfano wa uwepo wa zahanati sita ambazo hazina mtumishi hata mmoja na nyingine saba zina mtumishi mmoja mmoja pekee.

"Rais ana dhamira ya dhati kwa wananchi wake, anatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta za elimu na afya lakini changamoto kubwa iliyokuwepo ni uhaba wa watumishi ambao wanatishia utoaji wa huduma bora wa wananchi," amesema Mwenyekiti huyo.

Kutokana na hali, mwenyekiti huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kuwasaidia kumaliza changamoto ya watumishi Ili halmashauri hiyo iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wake.