Diamond naNandy waendeleza ubabe Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Huu ni mwaka wa pili mfululizo waimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz na Nandy wameendelea kuonyesha ubabe wao wa kimuziki ukanda wa Afrika Mashariki katika tuzo za African Muzik Magazine Awards (Afrimma).

Huu ni mwaka wa pili mfululizo waimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz na Nandy wameendelea kuonyesha ubabe wao wa kimuziki ukanda wa Afrika Mashariki katika tuzo za African Muzik Magazine Awards (Afrimma).

Wikiendi iliyopita Diamond alishinda tuzo ya Afrimma katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, huku Nandy akishinda kama Msanii Bora wa Kike kwa ukanda huo.

Mwaka jana Diamond na Nandy waliibuka washindi tena katika vipengele hivyo viwili, huku Zuchu akishinda kile cha Msanii Bora Chupukizi.

Diamond aliwazidi kete washindani wake ambao ni Eddy Kenzo (Uganda), The Ben (Rwanda), Khaligraph Jones (Kenya), Gildo Kassa (Ethiopia), Otile Brown (Kenya) na Meddy (Rwanda).

Kwa upande wake Nandy ameibuka mshindi mbele ya Zuchu (Tanzania), Nadia Mukami (Kenya), Vinka (Uganda), Sheebah Karungi (Uganda), Nikita Kering (Kenya), Knowless Butera (Rwanda) na Tanasha Donna (Kenya).

Hata hivyo, huu pia ni mwaka wa tatu mfululizo Nandy anapata tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, kwani mwaka jana alishinda kipengele hicho katika tuzo za All Africa Music Awards (Afrima) ikiwa ni mara ya pili baada ile aliyoshinda mwaka 2017.

Kizuri zaidi hiyo ni sawa na Diamond, kwani mwaka jana alishinda Afrima kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki. Hiyo ina maana kuwa kwa miaka miwili mfululizo katika tuzo za Afrimma na Afrima, Diamond na Nandy wametawala Afrika Mashariki katika kipengele hicho.

Ni wazi Nandy amekuja kupokea kijiti cha Vanessa Mdee ambaye aliwahi kushinda tuzo ya Afrima kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki kwa miaka miwili mfululizo, hiyo ilikuwa ni mwaka 2014 na 2015.

Katika miaka hiyo ambayo Vanessa amechukua tuzo hizo alikuwa akishinda pamoja na Diamond, ambaye mwaka 2015 alishinda tuzo tatu kwenye vipengele vya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, Msanii Bora wa Mwaka Afrika na Wimbo Bora wa Mwaka kupitia wimbo wake ‘Nasema Nawe’.

Tuzo za Afrima zilianza Desemba 2014 huko Nigeria kisha baadaye kufanyika Ghana, wana jumla ya vipengele 37, waandaaji wanashirikiana na Umoja wa Afrika (AU), lengo likiwa ni kuutangaza na kuupa thamani muziki wa bara hilo. Pia tuzo za Afrimma zilianza Julai 2014 Texas, Marekani kwa ajili ya kuwatunza wasanii, watangazaji, Djs na wengineo kutoka kiwanda cha burudani.