Dk Mwinyi anavyojifungulia ukarasa mpya wa historia

Wednesday November 25 2020
mwinyi1 pic
By Mwandishi Wetu

Kwa kawaida hapa nyumbani na nje linapoundwa baraza jipya la mawaziri baada ya uchaguzi, watu hutarajia mabadiliko ya mpangilio wa wizara na viongozi wake.

Lakini baraza jipya la mawaziri lililotangazwa wiki iliyopita na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ni la aina yake katika historia ya Visiwani tokea kufanyika mapinduzi mwaka 1964.

Baraza jipya lina vijana na wengi, tafauti na hali ilivyokuwa katika miaka ya nyuma ambapo wazee ndiyo walitamalaki. Pia, baraza jipya lina mawaziri wanawake wanne sawa na asilimia 31. Wizara mbili zipo wazi kwa maelezo kwamba zimetengwa kwa chama cha ACT Wazalendo kama kitaridhia kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Karibu mawaziri wote isipokuwa wanne walizaliwa kabla ya mapinduzi ya 1964. Rais Mwinyi naye yumo katika kundi, azaliwa mwaka 1966 pia Makamu wake wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla naye bado kijana sana. Hivyo, muundo wa Baraza unatafsiriwa kama mtihani kwa vijana wa Zanzibar, ambao kama wenzao wa Bara na nchi nyingi za Afrika, wamekuwa wakilalamika kwa miaka mingi kuwa wanabanwa kupewa nafasi za juu za uongozi.

Kinachosubiriwa ni kuona vipi Baraza hili lililotawaliwa na vijana litafanya kazi ukilinganisha na yaliyopita ambayo mawaziri wengi walikuwa wenye umri mkubwa.

Kwa kuzingatia maelezo ya Rais Mwinyi baada ya kuwaapisha mawaziri hao, wametwishwa mzigo mzito na sasa wanapaswa waubebe wenyewe na hakuna mwanya wa kumtwisha mpagazi.

Advertisement

Dk Mwinyi aliwaambia atakayeshindwa kuwajibika kuutumikia umma, kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali na kuondoa uonevu, ajue atawekwa pembeni.

Katika kuwaonyesha maovu aliyoyagundua katika sekta mbalimbali muda mfupi tangu aingie madarakani, Dk Mwinyi alielezea madudu aliyoyaona na kulazimika kuwatimua baadhi ya viongozi wa serikali na mashirika ya umma.

Katika hili, Rais alisema kweli tupu, kwa sababu ukitazama kwa kina orodha ya madhila yanayofanywa na baadhi ya viongozi huko serikalini wakiwamo baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, ni mengi na kama lengo ni kuwa na serikali yenye weledi, haya lazima yamulikwe na wahusika wafagiwe bila kuwaonea muhali.

Serikali ya Zanzibar sasa ni lazima ikaenda na ari ya Rais Mwinyi ya kutooneana haya pale watendaji wanapokwenda kinyume na matakwa ya kiongozi wao mkuu.

Kila anayekumbatia rushwa, anayetumia vibaya fedha za serikali, uzembe au uonevu achukuliwe hatua za kisheria kama ilivyo kwa wizi wa nazi, viazi na maandazi au wanaovunja nyumba na kuiba luninga, nguo, sahani na sufuria. Watu huwajibika panapokuwepo mfumo wa kuwawajibisha kwa vitendo, hasa pale wanapofanya uhalifu.

Rais Mwinyi aliorodhesha uoza, madhila na uonevu aliougundua katika idara na mashirika ya umma na kusisitiza kwamba dhulma za aina yoyote ile sasa basi. Lakini ni muhimu akafahamu orodha ya uonevu visiwani ni kubwa.

Mojawapo ni watu wengi kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari licha ya kuwa na vya zamani, cheti cha kuzaliwa na uthibitisho wa kusoma na kuishi visiwani. Watu hawa wamegeuzwa wakimbizi katika nchi yao kwa vile wanakosa kushiriki katika uchaguzi, kupata leseni za biashara na nyingine, kufungua akaunti benki, hati ya usafiri na haki nyeingine za raia. Madhira yanayosikika na kuonekana kwa video na picha ni pamoja na mwenendo wa vyombo vya ulinzi na hili lilionekana wazi kabla na baada ya uchaguzi uliomuweka madarakani.

Wapo watu waliolalamika kwa kuwekwa kizuizini muda mrefu bila kushitakiwa au kupewa dhamana wakati sheria inataka mtuhumiwa afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 na hapana kipengele cha kuhalalisha kumpiga au kumtesa mtu.

Hili linahitaji kuchunguzwa na waliofanya haya wawajibishwe kusudi kuonyesha dhamira ya kauli yake ya kusema madhila na uonevu Zanzibar sasa basi katika Zanzibar mpya. Wapo waliosema waliteswa kwa kupigwa kwa virungu na nondo na kuonekana wamevunjika miguu, mikono na kuvunjwa viungo. Kauli za Rais Mwinyi zinatoa matumaini makubwa ya kuwa na serikali yenye weledi na inayojali haki na sheria.

Lakini ni muhimu kwa maneno kuthibitishwa kwa vitendo ili kujenga jamii inayoelewana, na watu wake wajione wanaishi katika mazingira yanayojali haki na sheria.

Zanzibar mpya ya raha, furaha na amani inawezekana kama dhamira ya Dk Mwinyi itatekelezwa kwa vitendo.

Advertisement