Hisia tofauti uteuzi wa ma-DC

Rais Samia Suluhu Hassan.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2023 alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya 37 na kuwahamisha vituo vya kazi wakuu wa wilaya 48 huku 55 wakibaki kwenye nafasi zao.

Dar/Mikoani. Kuachwa katika uteuzi na kuhamishwa kwa baadhi ya wakuu wa wilaya kulikofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan juzi, kumepokewa kwa hisia tofauti huku baadhi ya wananchi, wadau na wachambuzi wakitaja sababu kadhaa zinazoweza kuwa zilimsukuma mkuu wa nchi kufanya mabadiliko hayo.

Licha ya kuwa na mamlaka kikatiba ya kuteua, kutengua au kuacha baadhi ya wateule wake, wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesema mabadiliko hayo yalitarajiwa.

Hii ni kutokana na kauli ya Rais Samia ya Desemba 8, 2022 aliyoitoa akiwa katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM uliomchagua kuwa mwenyekiti wa Taifa wa CCM jijini Dodoma, kuwa katika safari yake ya miaka miwili anahisi ana watu ambao kasi yao haiendani na ya Serikali yake.

Rais alitumia fursa hiyo kuomba baraka za wajumbe wa mkutano huo akaipange upya Serikali yake.

Pamoja na hilo, zipo pia sababu zilizotajwa kumsukuma kufanya mabadiliko hayo akiwateua wakuu wapya wa wilaya 37 (sawa na idadi ya walioachwa, kuwahamisha vituo 47 na wengine 55 kubaki vituo vyao vya kazi.

Wanadai kwamba misuguano ya kiutendaji baina ya wateule hao na watendaji wengine ndani ya wilaya imechangia mabadiliko hayo, wakitolea mfano wa wilaya za Kilwa, Korogwe, Arusha, Monduli, Arumeru na za Dar es Salaam.

Sababu nyingine ambazo wasomi, viongozi wa kisiasa na wananchi wanaona ziko nyuma ya pazia ni pamoja na Rais kujenga timu ya ushindi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Nyingine ni baadhi ya Ma-DC kufanya kazi chini ya kiwango, umri, kufanya kazi kwa mazoea, kuimarisha utendaji kazi, kutimiza maono ya Rais, Rais kufanyia kazi taarifa za vyombo, uhusiano mbaya na kutoiva na mfumo.


Kilwa walia na DC

Siku moja baada ya uteuzi huo, baadhi ya wananchi wilayani Kilwa wameliambia Mwananchi jana kuwa mkuu wa wilaya aliyeondolewa, Zainabu Kawawa, hakuwa mtendaji mzuri, hakuonyesha ushirikiano na ameshindwa kutatua matatizo yao.

Mmoja wa wananchi hao, Said Mohamed alidai DC huyo alishindwa kutafuta suluhu ya wakulima na wafugaji na hakuwa na uhusiano mzuri na wananchi.

Suala la migogoro ya ardhi ambalo ni tatizo la kitaifa lililopo maeneo mengi, pia lilizungumzwa na mwananchi Asha Mohamed Juma, aliyedai kuwa Kawawa Zainabu alishindwa kusimamia upangaji bora wa matumizi ya ardhi.

“Yaani alifikia hatua ya kutuambia tutawazoea wafugaji kidogo kidogo, tuwaacheni, hii ilipelekea migogoro ya mara kwa mara ya wafugaji na wakulima,” alidai mkazi huyo

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Kawawa azungumzie madai ya wananchi hao, alicheka, kisha akasema anashukuru kwa kuaminiwa na Rais kwenda kutumikia wilaya hiyo na mengine anamwachia Mungu.

“Yote namwachia Mungu, mimi nilienda Kilwa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan majukumu yake, miradi yote ilifanywa na Serikali, nilikuwa kama msimamizi tu. Nashukuru wananchi kwa upendo, ushirikiano na umoja wao kwangu. Namshukuru Rais aliniamini, nawatakia kila la heri wananchi wa Kilwa,” alisema Kawawa.

Wakati Kilwa wakieleza hayo, kutoka wilayani Handeni mkoani Tanga, inadaiwa kuwa aliyekuwa DC, Heriel Mchemba licha ya kuwa na maelewano mazuri na wananchi kulikuwapo watu waliokuwa wanampinga kwa sababu za kisiasa.

Akimzungumzia Mchemba, mkazi wa Misima, Twaha Mngatwa alisema alipenda mtindo wa utendaji wa DC huyo wa kujishusha chini na kuwa karibu na wananchi hali iliyomsaidia kutatua kero zao nyingi.

“Ni mabadiliko ya kiutendaji ya kimfumo kwa sababu yeye alijishusha chini kabisa kwa watu, labda kuna kazi kubwa zaidi Rais anataka kumpangia, ndiyo sababu hajapewa ukuu wa wilaya,” alisema Twaha.

Mkazi mwingine, Mwajabu Suphian alisema Mchemba alikuwa mchapa kazi na kazi zinaonekana, akitolea mfano alivyosimamia suala la Msomera mpaka lilipo sasa.

Baada ya mabadiliko hayo, Mchemba kupitia kwenye mtandao wake wa kijamii aliandika neno la kushukuru kupitia mitandao ya kijamii na kusema anawashukuru viongozi wote wa chama, Serikali, taasisi binafsi na wananchi wote wa Handeni kwa ushirikiano waliompa.

“Niombe radhi pale palipo na mapungufu kama mwanadamu sikukamilika. Ni Mungu pekee aliyekamilika. Mkumbuke kwenye mapungufu hayo yamkini kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni katika kutekeleza wajibu,” alisema.

Huko Korogwe, baadhi ya wananchi wamedai huenda kulikuwa na misuguano ya kiutendaji kati ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Basila Mwanukuzi na watendaji kupitia usimamiaji wake wa kazi.

Mkazi mmoja wilayani humo aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema Mwanukuzi amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na malalamiko ambayo amewahi kuyatoa dhidi wakurugenzi wa halmashauri zilizopo katika wilaya hiyo.

Mfano, mwezi mmoja uliopita, alinukuliwa na vyombo vya habari akilalamikia hatua ya fedha za miradi kukaa katika akaunti za halmashauri kwa kisingizio cha michakato ya manunuzi, mfumo na vifungu, akisema amechoka na hali hiyo.

“Mimi nasema enough is enough (imetosha), siwezi kuwa sehemu ya kumhujumu Rais. Kwani ni Korogwe tu ndiyo kuna vifungu na mifumo?” alisema huku akisisitiza kuwa Korogwe hali si nzuri na kutaka waziri wa Tamisemi aingilie kati.

“Tunahisi kiini cha Mwanukuzi kuondolewa ni kitendo cha kulalamika kuhusu fedha za miradi ya maendeleo wakati alipaswa kusimamia mapema kabla mambo hayajaharibika,” alisema Winfrida Guga.

“Nilipomsikia mkuu wetu wa wilaya akilalamikia kutotumika kwa muda fedha za miradi ya maendeleo huku akiwatupia lawama wakurugenzi wa halmashauri zake za Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini, nikaona hapa kuna tatizo,” aliongeza Guga bila kuonyesha tatizo lake hasa nini.

Naye Sadick Jumbe ambaye ni mkandarasi wa barabara wilayani Korogwe alisema alipoona Mwanukuzi anatofautiana na watendaji wa halmashauri alibaini kuwa lazima atakwamishwa kwa sababu ameonyesha kuishiwa mbinu za kuwaongoza.

Kutoka Songwe, Juliana Kalago ambaye ni mkazi wa Tunduma alisema kwake mabadiliko ya viongozi yamekuwa yakitokea ili kuimarisha utendaji na kuwaondoa ambao wameshindwa kuendana na kasi ya uongozi uliopo.

Kuhusu kuachwa kwa mkuu wa wilaya Mbozi, Abdallah Said, mkazi wa Vwawa, Asifiwe Mbena alisema huenda inatokana na umri wake (hakuutaja) kuwa mkubwa.

“Tumeambiwa amestaafishwa ili kuingiza nguvu mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025,” alidai Mbena.


Misuguano ya kisiasa

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wananchi wa mkoani Arusha, walidai migongano ya viongozi na wanasiasa na kushindwa kutatua migogoro ya ardhi, imekuwa changamoto kubwa kwa wateule hao.

Miongoni mwa migongano hiyo ni ule unaowahusisha wanasiasa akiwemo Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo na baadhi ya watendaji wa halmashauri na chama tawala. Mbali na hilo, Julius Kaaya, mmoja wa wakazi wa Arumeru alisema migogoro ya ardhi imekosa suluhu ikiwepo ya mashamba 11 ya maua ambayo sasa yamekufa huku waliokuwa wafanyakazi zaidi ya 4,000 hawajui hatima yao katika ajira na uchumi.

Wakati hali ikiwa hivyo maeneo mengine, kutoka Njombe, wananchi wilayani Ludewa walidai kuachwa kwa mkuu wa wilaya hiyo, Andrea Tsere kumewashtua kwa kiasi kikubwa kwani alikuwa kiongozi mchapa kazi na mpenda maendeleo na hivyo hilo limeacha fumbo kama ilivyo kwa Moshi, Mpwapwa na Mtwara.


Profesa Mahalu afunguka

Akizungumzia kuachwa na kuhamishwa kwa baadhi ya Ma DC hao, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Costa Mahalu alisema mara nyingi maamuzi ya Rais hujikita kwenye utendaji, malengo, maono na taarifa za vyombo vyake vya uchunguzi.

“Rais ana madaraka ya kufanya uteuzi, utenguzi na uhamisho kadri anavyoamua na kuona inafaa; anaweza kuamua kwa utashi wake kwa kutumia taarifa za vyombo kuhusu ubora na udhaifu wa wateule,” alisema.

Imeandikwa na Daniel Mjema na Florah Temba (Moshi), Peter Saramba (Mwanza), Noor Shija na Ramadhan Hassan (Dodoma), Lilian Lucas na Hamida Sharif (Morogoro), Seif Jumanne (Njombe), Mwanamkasi Jumbe (Mtwara), Mussa Juma (Arusha), Burhan Yakub (Tanga), Rajab Athman (Handeni), Jonas Simbeye (Songwe) na Hawa Mathias (Mbeya), Tuzo Mapunda (Dar) na Frolence Sanawa (Mtwara).