Hofu rungu la Samia yatanda serikalini

Rais Samia Suluhu Hassan.

Muktasari:

  • Rais Samia baada ya kukamilisha safu ya uongozi CCM, hofu yazidi kutanda serikalini kutokana na ahadi ya kupata watendaji wapya wanaoendana na kasi yake

Moshi/mikoani. Joto kwa wateule wa Rais linazidi kupanda baada ya mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kukamilisha kuunda safu ya uongozi wa juu wa chama hicho huku akiendelea kutimiza ahadi yake ya kuisuka upya Serikali.

Kufuatia ahadi hiyo ambayo haijulikani ukomo wake, baadhi ya wateule wanaishi kwa hofu na wasiwasi wakiwemo mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.

Pia, wapo wakuu wa mashirika, wakala na taasisi mbalimbali ambao wamekuwa roho juu wasijue ukomo wa ahadi hiyo ya mkuu wa nchi.

Desemba 8 mwaka jana akiwa katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM jijini Dodoma, Rais Samia alisema katika safari yake ya miaka miwili aliyoianza Machi 19, 2021 anahisi ana watu ambao mwendo wao hauendani na kasi ya Serikali yake ya awamu ya sita.

“Nawaomba sasa mnipe baraka zenu nikaipange Serikali pia. Nikaipange Serikali kwa jinsi ambavyo nahisi timu hii (ya CCM) tunaweza kwenda kuyatekeleza yale mliyoyasema hapa kwa vizuri zaidi,” alisema Rais Samia, kauli iliyoashiria mabadiliko makubwa yanakuja.

Wakati anaomba baraka hizo na kupewa na mkutano mkuu, Samia alikuwa hajamaliza kuunda Kamati Kuu na Sekretarieti, hatua ambayo aliikamilisha juzi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kuteua na kuthibitisha wajumbe wa Sekretarieti ya CCM huku wengi wa waliokuwemo wakiachwa.

Wajumbe wa sekretarieti waliosalia ni wawili tu, Daniel Chongolo anayeendelea na wadhifa wa katibu mkuu na Dk Frank Hawasi anayeendelea kuwa katibu wa NEC, (Uchumi na Fedha).

Walioteuliwa ni Anamringi Macha anayekuwanaibu katibu mkuu (Bara), Mohamed Said Dimwa (Naibu Katibu mkuu Zanzibar.

Pia katika safu hiyo, Sophia Mjema ameteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi kuchukua nafasi ya Shaka Hamdu Shaka na Issa Haji Ussi katibu wa Ognaizesheni.

Katika mabadiliko hayo, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk aliteuliwa kuwa Katibu wa Siasa na uhusiano wa Kimataifa, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na kanali Ngemela Lubinga.


Mabadiliko hayaepukiki

Wachambuzi wa masuasa ya kisiasa na uongozi wanaona mabadiliko hayo ya wajumbe wa sekretarieti yanaashiria mabadiliko ya uongozi kwa wateule wa Rais serikalini kutoepukika.

Sababu ya kwanza ni pale Rais Samia atakapoamua kujaza nafasi mbili za walioteuliwa kuingia sekretarieti ya CCM, ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga inayoshikiliwa na Sophia Mjema na ya Balozi Mbarouk, ambaye ni Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mbarouk pia ni mbunge wa kuteuliwa na Rais.


Uchaguzi mkuu, mikutano

Ukiacha nafasi hizo mbili, kauli ya Rais kwamba “kuna wateule hawaendi na kasi yake” nayo ni kama haijafanyiwa kazi kwa uzito wake, hivyo bila shaka atahitaji kupata safu mpya ya viongozi wa kuivusha CCM katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani.

Uchaguzi huo mara zote huchukuliwa kama kipimo cha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani hivyo wachambuzi wanaona Rais Samia atakuja na safu anayoona inakwenda kukidhi haja hiyo.

Kulingana na wachambuzi hao, mazingira ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 ni tofauti na yale ya 2019 na 2020, na huenda kusiwe na mteremko hivyo CCM itahitaji kujipanga.

Jambo lingine ambalo linahitaji CCM na Serikali kuwa na safu imara ni kuruhusiwa kwa mikutano wa hadhara ya vyama vya siasa, ambayo inatabiriwa kuamsha upya hekaheka za kisiasa ambazo hazijashuhudiwa kwa miaka saba.

Mikutano hii, inailazimu CCM na Serikali yake kujipanga vyema kujibu hoja zitakazoibuliwa na vyama vya upinzani na hii inamfanya Rais Samia kuhitaji safu itakayoendana na hali hiyo.

Katika kuliona hilo, Januari 11 mwaka huu wakati wa kilele cha matembezi ya vijana kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Rais akiwa mgeni rasmi aliwataka kujiandaa kujibu hoja zitakazoibuliwa na wapinzani.

Alisema CCM imekuja na mwelekeo wa maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kuijenga upya nchi, kazi hiyo inatakiwa kufanyika hata kwenye chama.

“Naomba sana, tunapokosolewa tuangalie, yale ya kweli tuyachukue tuyafanyie kazi, yawe makosa yameondoka. Yale ambayo si ya kweli, twendeni tukajibu kwa hoja lakini kubwa ni ustahimilivu,” alisema


Kuandaa timu kawaida, lazima

Alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya mabadiliko serikalini, Wakili Godfrey Wasonga alisema ni jambo la kawaida kwa kiongozi yeyote duniani kuandaa timu anayooona itamsaidia katika kutimiza ndoto na ahadi zake kwa waliomchagua.

Wasonga alisema uteuzi wa Rais kwa viongozi wa chama chake pia lilikuwa jambo la kawaida ili kutimiza matakwa ya katiba ya chama hicho lakini jambo la kupongeza ni namna alivyoanzia ngazi ya juu kwa maana ya watendaji wa ikulu, hivyo anaona itakuwa mwanzo mzuri kuisuka Serikali kwa ngazi ya chini.

Tayari Rais amefanya mabadiliko ya Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), taasisi ambazo ni nyeti katika suala la uongozi wa nchi.

Pamoja na hayo, wakili huyo alisema ni wakati wa mkuu wa nchi kutulia ili ateue viongozi wenye kumsaidia na watakaosimamia miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, ambayo inawapa nafasi Watanzania kumpima.

Akizungumzia hofu kwa wateule wa ngazi ya chini kwamba wanaweza kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kuwaza teuzi, Wasonga alisema jambo hilo linawezekana kwa ambao hawajui kuwa nafasi za uteuzi ni nguo ya kuazima.

Kingine alisema ni mkakati wa Rais kuhakikisha anakuwa na kikosi imara kinachokwenda kumsaidia 2025 kwa kuwa hilo ni lengo namba moja kwa kiongozi yeyote.

Maoni ya Wasonga yanaungwa mkono na Dk Rwezaula Kaijage, ambaye alisema mabadiliko ya viongozi ni muhimu ili Rais apate watu wanaoweza kuendana na falsafa yake lakini akaomba washauri wake wamshauri vizuri.

Alisema utendaji wowote unatazamwa na aliyetoa nafasi hiyo kwamba alilenga kupata kitu gani na kilichotokea kwa mhusika ni kipi.

Alisema washauri wa Rais wakituliza mawazo watamshauri vema na kumfanya apate watu sahihi watakaoisaidia Tanzania kutoka ilipo kwenda mbele.

Hata hivyo alisisitiza ushirikiano kwa walioteuliwa na watakaoteuliwa baadaye ili waweze kutimiza malengo katika majukumu waliyokabidhiwa.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mbeya (Muce), Dk Oscar Magava aliyaelezea mabadiliko kama njia ya kujiimarisha kiushindani.

Alisema Rais Samia ametoa mwanya kwa wengi kuwa na fursa ya kuifanya siasa, bila kujiimarisha kuna hatari ya chama chake kufunikwa.

Alisema mabadiliko hayo yatarajiwe si tu kwa CCM pekee, bali hata vyama vya upinzani, kadhalika ndani ya Serikali kwa kuwa kunahitajika watendaji wazuri ili pasipatikane mengi ya kukosoa.

Dk Magava alikwenda mbali zaidi akitolea mifano ya baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliobadilishwa, si manguli wa siasa za ushindani wa majukwaani wana asili ya upole ukilinganisha na waliopewa nafasi hizo sasa.

Wakati wasomi hao wanayatazama mabadiliko kwa jicho hilo, mwanaharakati Edwin Soko alisema yatazalisha mpasuko katika baadhi ya maeneo kwa kuwa wengi wataondolewa na kuingia wapya.

Kwa mujibu wa Soko, Rais anatamani kuwa na safu yake ambayo ni imara huku akitazama anga la 2025 na kwamba watakaomvusha ni hawa anaoanza nao sasa kuanzia kwenye chama hadi serikalini.

Soko alisema ahadi ya Rais aliyoitoa mwanzoni mwa Desemba mwaka jana ni kuisuka upya Serikali. Kwa hiyo Watanzania wategemee mabadiliko makubwa kwa ngazi za wateule kama alivyoanzia Ikulu.

Hata hivyo, alisema mpasuko utakaotokea ndani ya chama hautakuwa mkubwa, hivyo (Rais) anaweza kuuzuia na kuudhibiti kwa mamlaka aliyonayo.

Vilevile, Soko alisema kwa sasa kutakuwa na utendaji kazi wa kusuasua kwa baadhi ya watu kwani wanahofu kama watakuwa miongozi mwa wateule au wataachwa hivyo akashauri kama ni mabadiliko yafanyike mapema ili kuondoa hofu hiyo.


Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Habel Chidawali (Dodoma) na Juma Issihaka (Dar).