Jafo ataka ujenzi wa nyumbani uendane na upandaji miti

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo (katikati) akiwakabidhi mti kikundi cha mazingira Cha Chapa Kazi Dodoma. Kushoto Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Seleman Jafo, ameagiza Wakurugenzi kutoruhusu vibali vya ujenzi ikiwa kiwanja hakina nafasi ya kupanda miti japo miwili

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Seleman Jafo, ameagiza Wakurugenzi kutoruhusu vibali vya ujenzi ikiwa kiwanja hakina nafasi ya kupanda miti japo miwili.

 Waziri Dk Jafo ametoa agizo hilo jana Jumatano Agost 11, 2022 wakati akizindua kampeni ya upandaji miti 2000 iliyoongozwa na Shirika la madini la Taifa (STAMICO).

Dk Jafo ameagiza mpango huo uende sambamba na utunzaji wa miti yote ambayo imepandwa katika kutimiza lengo la kijanisha Tanzania.

"Wekeni malengo ya na mkakati katika suala zima la kupanda miti, naagiza Wakurugenzi kwa nchi nzima kuanzia leo ni marufuku kutoa kibali cha kujenga nyumba kama hakuna mpango wa eneo hilo kuwa na miti japo miwili kwa uchache," amesema Jafo.

Amesema hali ya mazingira kidunia siyo nzuri na kwa Tanzania tatizo ni ukosefu mkubwa wa misitu ambayo inaendelea kumalizwa kila uchwao.

Waziri huyo ameagiza taasisi zingine kuangalia namna zinavyoweza kuunga mkono juhudi hizo ili Taifa lifikie malengo yake na kwa wakati.

Akizungumzia kampeni hiyo, Waziri wa Madini Dk Dotto Biteko amesema lengo la kupanda miti hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali lakini kwa faida kubwa ya wananchi hasa kipindi hiki ambacho hali si nzuri.

Dk Biketo amesema tofauti na maeneo mengine, lakini wao wameamua kwa dhati kuwekeza nguvu zao kwenye misitu na kwamba mpango wa wao ni kuhakikisha miti yote inastawi, hivyo ukifanya mmoja lazima wapande kufidia.