Jinsi waliomuua Dk Sengondo Mvungi walivyonaswa, kuhukumiwa kifo (2)

Jinsi waliomuua Dk Sengondo Mvungi walivyonaswa, kuhukumiwa kifo (2)

Muktasari:

  • Baadaye, watu sita ambao ni Msigwa Matonya, Mianda Mlewa, Paulo Mdonondo, Longishu Loshingo, Juma Kang’ungu na John Mayunga au Ngosha walishitakiwa kwa mauaji ya nguli huyo wa sheria nchini.

Dar es Salaam. Wakati Dk Sengondo Mvungi akipelekwa Hospitali ya Tumbi ili kuokoa maisha yake baada ya kushambuliwa na majambazi, tayari Jeshi la Polisi lilikuwa linaendelea kulifuatilia tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotekelezwa nyumbani kwake.

Bila kupoteza muda, askari kutoka Kituo cha Polisi Kimara walikwenda eneo la tukio. Walipofika walikuta mlango wa jikoni ukiwa umevunjwa huku damu ikiwa imetapakaa. Askari hao walianza kazi yao kwa kuandaa mchoro wa eneo la tukio.

Siku iliyofuata Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliamuru kikosi kazi maalumu kufuatilia kwa kina kuhusu tukio hilo ambapo Sh2 milioni, kompyuta mpakato moja, simu nne na bastola moja viliporwa.

Baadaye, watu sita ambao ni Msigwa Matonya, Mianda Mlewa, Paulo Mdonondo, Longishu Loshingo, Juma Kang’ungu na John Mayunga au Ngosha walishitakiwa kwa mauaji ya nguli huyo wa sheria nchini.


Washukiwa wakamatwa

Kazi ya kuwasaka wahalifu hao ilianza kwa kiongozi wa kikosi kazi kuwasiliana na wasiri wake. Mawasiliano ya kwanza yalifanikisha kukamtwa kwa mtuhumiwa wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Hamad eneo la Mwananyamala. Hamad alikamatwa Novemba 6 mwaka 2013.

Hata hivyo, alikana kushiriki katika tukio hilo lakini alimtaja Matonya Msigwa (mshitakiwa wa kwanza) na mwenzake Chibago kuwa miongoni mwa watu walioshiriki uhalifu huo.

Akiwa mikononi mwa polisi, Hamad alikuwa na ahadi ya kukutana na washukiwa hao siku iliyofuata. Hapa askari walimwamuru apige simu na awaombe watu hao wakutane Kinondoni Biafra siku hiyo saa 2:30 usiku.

Mpango ukaenda vizuri. Matonya na Chibago waliitika wito na kufika eneo hilo. Haukupita muda wakajikuta mikononi mwa polisi.

Wakati akihojiwa, Matonya alikiri kushiriki ujambazi ule na kwamba bastola waliyoipora ilikuwa kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Ngosha (mshitakiwa wa sita). Akawaeleza polisi kwamba tayari alikuwa amepanga kukutana na Ngosha siku inayofuata huko Vingunguti.

Majira ya saa 5:30 usiku askari waliondoka na Matonya hadi kituo cha Polisi Oysterbay. Wakiwa kituoni, simu ya Matonya iliita. Paulo (mshitakiwa wa tatu) ndiye alikuwa anapiga. Hapa, askari walimwamuru Matonya aweke sauti kubwa na amwombe mtu huyo wakutane kesho asubuhi.

Saa nane usiku, Paul alimpigia tena Matonya na kumweleza kuwa angekwenda Vingunguti pamona na Mianda (mshitakiwa wa pili) saa tatu asubuhi.

Siku iliyofauata saa tatu, kikosi maalumu tayari kilikuwa kimefika Vingunguti wakiwa na Matonya na Chibago. Ilipofika saa 4:30, Paulo na Mihanda nao wakawasili. Haukupita muda wakaangukia mikononi mwa polisi.

Msako ukaendelea. Watuhumiwa wote wanne sasa wakapelekwa Kituo cha Polisi Vingunguti kwa ajili ya mahojiano. Wakati Paulo akihojiwa, Matonya alimtaka aseme ukweli kuhusu kila kilichotokea kwani tayari walishaeleza mambo yote siku walipokamatwa.

Majira ya saa 5:15 wakati mahojiano yakiendelea, simu ya Paulo iliita tena. Simu hii ilipigwa na mtu aliyeitwa Masai. Paulo aliwaeleza polisi kuwa aliyekuwa anapiga ni mshirika wao katika uhalifu na kwamba alikuwa Tazara akija kukutana naye Vingunguti.

Askari wakaondoka na washukiwa wao hadi kituo cha basi Vingunguti na kuweka mtego. Wakiwa kituoni, Masai (mshitakiwa wa nne) alishuka kutoka kwenye daladala na mtu mwingine aliyeitwa Hamisi Juma King’ungu (mshitakiwa wa tano). Wote walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Vingunguti.

Katika mahojiano, Kang’ungu aliungama kuwa yeye ndiye aliyechukua kompyuta mpakato (laptop) ya Dk Mvungi na kuiuza Vingunguti kwa mtu aliyeitwa Chief kwa Sh200,000.

Hadi kesi dhidi yao inaisha Septemba mwaka jana, si laptop iliyopatikana wala Chief aliyekamatwa na polisi.

Alipobanwa ni wapi ilipokuwa bastola, Kang’ungu alijibu kuwa ilikuwa mikononi mwa mtu aliyeitwa Ngosha (mshitakiwa wa sita).

Askari wakisaidiana na Kang’ungu walianza kumtafuta Ngosha kupitia simu yake ya mkononi bila mafanikio na kuamua kurudi Kituo cha Polisi Oysterbay. Wakati huo ilikuwa ni saa 7:30 mchana, Novemba 7 mwaka 2013.

Walifika kituoni Oysterbay saa 11 jioni na kumfahamisha Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) walichokipata na kumkabidhi washukiwa wote saba kwa mahojiano zaidi.


Ngosha akamatwa

Novemba 12 mwaka 2013, Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Ujambazi katika Kituo Kikuu cha Polisi alipokea simu kutoka kwa msiri wake majira ya saa 11:30 jioni akimweleza kuwa mmoja ya watu walioshiriki mauaji na uporaji wa Dk Mvungu alikuwa Jangwani, Kariakoo akiangalia mazoezi ya timu ya Yanga katika uwanja wa Kaunda.

Mkuu huyo aliambatana na askari wengine hadi eneo hilo wakiwa na msiri wao aliyewaonyesha sehemu aliyosimama na nguo alizovaa ili kurahisisha ukamataji. Walimsogelea bila yeye kuhisi anatafutwa na kukamatwa.

Alikiri kushirika uhalifu huo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa kuonyesha silaha aliyoiba siku ya tukio.

Saa 12:30 jioni askari walikwenda kwenye makazi ya Ngosha yaliyopo eneo la Kiwalani Migombani kufanya upekuzi. Walipofika, askari walimwita Ali Mlekwa, baba mwenye nyumba aliyoishi mshukiwa huyo na John Ikondya Mayunga au Ngosha ili washuhudie upekuzi wa chumba cha mshukiwa.

Walimwita pia mjumbe wa nyumba 10, Mzee Abdallah Ally na mpangaji mwenzake, Emmanuel Mwakipusa kushuhudia upekuzi huo. Wakiwa na mpigapicha wao aliyerekodi tukio zima, polisi walipekua makazi ya mtuhumiwa huyo kama ilivyopangwa.

Kabla ya upekuzi kuanza, polisi walimfahamisha Ngosha kuwa nia nzima ya kazi hiyo ilikuwa kusaka silaha wanayoitafuta. Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa kazi hiyo, Ngosha alikiri kuwa alikuwa akimiliki bastola kinyume kinyume na sheria.

Aliwaonyesha sehemu aliyoficha silaha hiyo, ilikuwa ndani ya mfuko wa plastiki uliofichwa chini ya tofali kwenye kona ya nyumba, kuta zinapokutana. Mfuko ule ulipofunguliwa, bastola nyeusi aina ya Airweight Revolver ilipatikana.

Ilikuja kuthibitishwa mahakamani kuwa bastola hiyo ndiyo iliyoibwa nyumbani kwa marehemu Dk Mvungi siku amevamiwa na kuuawa.

Msako uliendelea na polisi walipata risasi 21 na vifuko vitano vya baruti. Baada ya kazi hiyo hati ya upekuzi ilisainiwa na wote kabla ya kuondoka na mshukiwa hadi Kituo cha Polisi Msimbazi.

Katika hatua hii, askari wa upelelezi kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay aliitwa na kukabidhiwa mshukiwa na vidhibiti vyote kwa hatua inayofuata.


Washitakiwa wajitetea

Mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Matonya anayefanya biashara ya kuchinja ng’ombe eneo la Gongolamboto alisema yeye na wenzake sita walikamatwa na polisi wakinywa pombe Novemba 6 mwaka 2013 saa 11 jioni na hawakuambiwa sababu za kukamatwa kwao.

Alisema walipelekwa Kituo cha Polisi Kijitonyama ambako alipewa karatasi ya kusaini na alipokataa alipigwa na kirungu magotini, miguuni na kuingizwa chupa sehemu ya haja kubwa. Anadai kwa mateso yale, alilazimika kusaini karatasi zile.

Mshitakiwa mwingine Juma Kang’ungu anayefanya biashara ya viatu eneo la Buguruni alisema alikamatwa wakati akiendelea na shughuli zake Buguruni kwa madai ya kujihusisha na dawa za kulevya.


Wahukumiwa kunyongwa

Baada ya kuisikiliza kesi dhidi ya watuhumiwa hao sita, Septemba 17 mwaka jana, Jaji Seif Kulita aliridhika kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha kosa dhidi ya washitakiwa wote isipokuwa mshitakiwa wa tano ambaye aliachiwa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha dhidi yake.

“Mshitakiwa alikamatwa na polisi kwa sababu tu alionekana akishuka kwenye basi eneo la Vingunguti na Maasai aliyekuwa akisubiriwa na polisi. Tofauti na washitakiwa wengine watano, polisi hawakuwa na taarifa zozote za awali kuhusu mtu huyu (Kang’ungu ) kabla hajakamatwa,” alisema Jaji Kulita alipotoa hukumu iliyomwachia huru Kang’ungu wakati wenzake wakihukumiwa kunyongwa.