Kilio kwa madereva operesheni ya Sirro

Friday June 11 2021
siro pic

Askari wa usalama barabarani akisimamisha gari kwa ajili ya kulifanyia ukaguzi katika eneo la Tabata relini jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha na Ericky Boniphace.

By Mwandishi Wetu

Dar/Mbeya. Wakati madereva jijini Dar es Salaam wakililalamikia Jeshi la Polisi namna linavyoendesha operesheni za kukamata magari mabovu, huko Mbeya limenasa mabasi mabovu 12 kati ya 32 yaliyokaguliwa, kwenye operesheni ya kudhibiti usalama wa barabarani na uhalifu inayotekelezwa nchi nzima kuanzia jana.

Juzi Mkuu wa Jeshi hilo nchini (IGP), Simon Sirro wakati wa kikao kazi cha kufanya tathmini aliagiza wakuu wa usalama barabarani mikoa yote kufanya operesheni dhidi ya magari mabovu yasiyokidhi vigezo, sambamba na kubaini mianya ya uhalifu na wahalifu itakayofanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Operesheni hiyo inatokana na kuibuka wimbi la ajali, ambapo Juni 2, 2021 watu wanne walifariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa, baada ya basi la kampuni ya Classic kupata ajali katika kijiji cha Buyubi kata ya Didia mkoani Shinyanga.

Katika jiji la Dar es Salaam jana, baadhi ya makamanda wameanza kutekeleza agizo hilo, ambapo wameapa kufanya operesheni hiyo usiku na mchana, hasa kwa madereva watakaobainika kuingiza magari mabovu nyakati za usiku.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Richard Ngole aliwataka wenye magari mabovu, ikiwemo daladala zinazofanya kazi usiku, kutoyapeleka barabarani na endapo watakamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Alisema operesheni hiyo ilianza juzi baada ya agizo la IGP, ambapo jeshi hilo limebaini magari mabovu kufanya kazi nyakati za usiku, ili kukwepa kukamatwa bila kujali usalama wa abiria.

Advertisement

“Tumebaini magari mabovu yanaanza kutembea usiku, hivyo Jeshi la Polisi limejipanga kwenda kwenye barabara zote ili kuhakikisha magari hayo yanakamatwa,” alisema Ngole.

“Inapofika usiku wenye magari mabovu wanayatoa barabarani, natoa onyo kwa wote kuacha mara moja, tutawafuata huko wanakoficha magari yao,” alisema.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema jeshi hilo halina usiku wala mchana, wameshaanza kufanya msako kwa saa 24 bila kujali jua wala mvua.

“Tumepokea maelekezo na tayari vikosi vyetu vimejipanga kukabiliana na uhalifu wowote utakaojitokeza, iwe usiku au mchana kama mlivyosikia IGP alivyosema, operesheni iliyopita ilikuwa ya mafanikio makubwa, hii nayo tumejipanga vizuri,” alisema Kingai.

Hata hivyo, baadhi ya madereva wameeleza malalamiko yao kuwa polisi wameanza kutumia operesheni hiyo kuwaonea, ikiwemo kukamata magari ambayo yameshaandikiwa kulipa faini.

Kado Ramadhani, dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Mabibo na Makumbusho alisema wakati mwingine gari linakuwa na hitilafu na limeshaandikiwa kulipa faini ndani ya kipindi cha siku saba, lakini inakamatwa.

“Nadhani operesheni hii isihusishe magari yanayodaiwa, kama gari limeshaandikiwa kulipa faini basi katika operesheni hii lisihusishwe hadi muda wa kulipa utakapokwisha,” alisema Ramadhani. Dereva Jimmy Moshi alisema ni utaratibu wao kufanya ukaguzi mara kwa mara, lakini aliliomba jeshi hilo wakati wanapotekeleza agizo la IGP kuwatendea haki.

“Madereva wengi wameanza kupaki magari mchana na kuyatoa usiku, hata ukiangalia baada ya agizo la IGP idadi ya magari barabarani imepungua, ombi langu wakati wa hii operesheni polisi watende haki,” alisema Moshi.

Mbeya

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Urlich Matei alisema wameanza ukaguzi jana alfajiri kwenye kituo kikuu cha mabasi ya mikoani ambapo kati ya mabasi 32 yaliyokaguliwa, 12 yalibainika kuwa mabovu na kusitishwa kuendelea na safari.

“Hatua hii tumeianza toka jana (juzi), licha ya mabasi ya mikoani, pia mabasi 53 ya wilayani yamekaguliwa na baadhi yamebainika ni mabovu na kusitisha safari hadi yatakapotengenezwa, ingawa sina takwimu kwa sasa,” alisema Matei.

Alisema hatua hiyo ni endelevu na wanashirikiana na wakaguzi wa jeshi hilo kwenye maeneo yaliyoelekezwa, hususani kituo cha mabasi Nane nane na stendi kuu lengo ni kuhakikisha vyombo visivyokuwa na ubora kutoendelea kusafirisha abiria.

Mkaguzi wa mabasi kutoka jeshi hilo, Ibrahim Samwix alisema pamoja na kufanya ukaguzi mara kwa mara, wamefanya operesheni maalumu iliyoenda sambamba na kutoa mafunzo kwa mafundi magari.

Alisema mafunzo hayo yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yalilenga kutoa elimu na kuwajengea uwezo na weledi mafundi wa mabasi, ili katika kazi zao mabasi yasiwe yanakamatwa kila siku kutokana na ubovu.

Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa alisema wamepokea maelekezo na kuanza kuyatekeleza nchi nzima. “Wakuu wote wa usalama barabarani (RTO) katika mikoa na wilaya zote, wameanza kukagua na kukamata magari yote mabovu,” alisema.

Imeandaliwa na Fortune Francis, Pamela Chilongola (Dar) na Hawa Mathias (Mbeya).

Advertisement