Kupanda bei mafuta ya kupikia, mbolea, sukari kulivyotikisa 2021

Muktasari:

  • Mafuta ya kupikia mpaka sasa hayajarudi katika bei ya kawaida licha ya kuwapo na ahadi kadhaa kutoka serikalini za kushughulikiwa changamoto hiyo.

Dar es Salaam. Mwaka 2021 unaelekea kutia nanga. Umekuwa ni wenye safari ndefu yenye milima na mabonde, furaha na huzuni.

 Mengi yalijitokeza katika mwaka huu miongoni mwa mambo yaliyotikisa jamii hasa katika huduma na bidhaa ni pamoja na ongezeko la bei ya mafuta, sukari na kupanda kwa bei ya mbolea.

Mmabo hayo siyo tu yamekuwa kilio cha wananchi kwa mwaka unaishia wiki ijayo, bali pia hali hiyo inaendelea na ahadi mbalimbali zinatolewa na Serikali kupitia wizara husika kuwa ayatpatiwa ufumbuzi.

Kupanda kwa bei ya mafuta

Mwanzoni mwa Januari, bei ya mafuta ya kula ilipanda katika maeneo yote nchini, huku bidhaa hiyo ikiadimika madukani.

Kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kulisababisha kupanda kwa bei ya vyakula ambavyo maandalizi yake yanategemeana na bidhaa hiyo kama vile chips na vitafunwa mbalimbali.

Mfano, katika jijini Dar es Salaam, mafuta ya alizeti ya ujazo wa lita tano yanauzwa kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 kutoka Sh19,000.

Kwa upande wa mafuta yanayotoka nje ya nchi, dumu la lita 20 lililokuwa likiuzwa Sh50,000 hadi Sh55,000 sasa linauzwa kati ya Sh78,000 hadi Sh80,000.

Wakati huohuo, dumu la mafuta la lita tano linauzwa Sh22,000, lita tatu Sh14,500 na lita moja Sh5,500 kutoka Sh3,500.

Katika wilaya ya Sumbwanga mkoani Rukwa, bei ya mafuta ya alizeti imepaa kutoka Sh50,000 iliyozoeleka kwa lita 20 mpaka Sh90,000. Pia mafuta aina nyingine yanayoagizwa kutoka nje ya mkoa huo nayo yanauzwa Sh105,000.

Jijini Mwanza, lita tano za mafuta ya kula zinauzwa kwa Sh28,000, lita 10 ni Sh43,500 na lita 20 zikiuzwa kwa Sh81,000.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe kwa mwaka mahitaji halisi ya mafuta ya kupikia nchini ni tani za ujazo wa 570,000 na kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000, hivyo kuna upungufu wa tani 365,000 ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipoulizwa kuhusu uhaba wa mafuta alisema mahitaji ya mafuta kwa Tanzania ni tani 600,000, wakati uzalishaji wa ndani ni tani 250,000 kwa mwaka, hivyo kuna upungufu wa tani 350,000.

Mwenyekiti wa chama cha wasindikaji wa mafuta ya kupikia Tanzania (Tasupa), Ringo Iringo alitaja sababu mbili zilizosababisha bei ya mafuta kuwa juu zikiwamo mvua kubwa zilizonyesha katika msimu wa mwaka jana nna kusababisha mavuno kidogo katika msimu huo na kufanya wenye mafuta wayapandishe bei.

Alisema zao la alizeti ambalo ndilo linazalisha mafuta kwa wingi halihitaji mvua kubwa lakini katika msimu wa mwaka jana mvua zilinyesha kwa wingi kiasi cha kuharibu mazao hayo mashambani.

Kupanda bei ya mbolea

Mbali na kupanda kwa mafuta na sukari, katika mwaka 2021 wakulima wamejikuta katika wakati mgumu baada ya bei ya mbolea kuendelea kuwa juu.

Kupanda kwa bei hii inaeleza kuwa ni duniani kote kwa sababu ya uzalishaji wa baadhi ya mazao kupungua wakati wa mlipuko wa kwanza Uviko-19.

Hata hivyo Serikali ilishauri njia tatu za kukabiliana na changamoto hiyo zikiwamo kuwashauri wakulima kutumia mbolea aina ya NPS na NPS ZIN-N.K kwa ajili ya kupandia ambazo gharama yake ni nafuu ikilinganishwa na mbolea ya DAP ambayo kwa sasa bei yake ipo juu kwenye soko la dunia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda mbolea zote hizo tatu zinatumika kupandia mazao, lakini kwa kuwa moja gharama yake ipo juu na hivyo kuwashauri wakulima kutumia mbolea ambazo bei yake ina unafuu

“Mbolea ya DAP kwenye maduka ya Dar es Salam kilo 50 inauzwa Sh75,000 na bei yake inaongezeka huko mikoani inafika hadi Sh100,000 hii bei itawaelemea wakulima,” alisema.

Alisema wamefanya mazungumzo na watu wanaoagiza mbolea ya NPS na NPS-ZIN-N.K na tayari kuna shehena inayotarajiwa kuuzwa Sh60,000 kwa mfuko wa kilo 50, ambayo ni sawa na bei ya mwaka jana.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma kuhusu suala hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali inafanya kila namna ili kupunguza makali hayo na hivi karibuni alikutana na Waziri wa Kilimo wa Morocco aliyemweleza kuwepo kwa uhaba wa mbolea kutoka katika kiwanda kikubwa nchini humo, ambacho kimekuwa kikiuza mbolea hadi nje ya nchi.

Majaliwa pia alisema hivi karibuni alikutana na mwekezaji kutoka Burundi ambaye amekubali kuja nchini kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea na maandalizi yake yameanza jijini Dodoma. Pia wameruhusu wafanyabiashara wa mbolea kuingiza nchini kwa masharti nafuu.

Aliwaomba watu wengine na taasisi zenye uwezo wa kuingiza mbolea, wafanye hivyo katika kipindi hiki kuliko kuendelea kutegemea kiwanda kimoja cha Minjingu ambacho uzalishaji wake hauwezi kukidhi soko la wakulima wa Tanzania.


Kupanda kwa bei sukari

Kama ambavyo imezoeleka kila inapofika mwezi Mtukufu wa Ramadhan bei ya sukari hupanda, hata kwa mwaka huu ilikuwa ni hivyohivyo.

Aprili ambapo Waislamu walianza kufunga bei ya sukari ilipanda na maeneo mengine kuadimika kabisa, jambo ambalo lilisababisha wananchi kuiomba Serikali kuingilia kati ili kuthibiti hali hiyo.

Ilipanda kati Sh2400 hadi 3200 kwa kilo moja kwa Mkoa wa Dar es Salaam, na kwa sasa mahitaji ya bidhaa hiyo.

Huku katika mikoa mbalimbali ikipanda kutoka Sh2700 hadi 3500 kwa kilo moja.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo aliwataka wafanyabiashara wanaofanya hivyo kuacha kutumia fursa ya mfungo wa Ramadhan kupandisha bei.

Waziri Mkumbo alieleza kuwa anaendelea kutafuta takwimu ya kiwango cha sukari kilichopo nchini, huku akiwataka wafanyabiashara kufuata bei elekezi.

“Watu wa bodi ya sukari wameweka bei elekezi, kwa hiyo tunawakumbusha wafanyabiashara kuzingatia hilo,” alisema Profesa Mkumbo.