Makinda ashangaa wasomi wanaokula bure makwao

Muktasari:

  • Wakati kilio cha watu kukosa ajira hasa kwa vijana kikiendelea kushika kasi, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda, amesema kuna idadi kubwa ya wasomi wanaoishi kwa wazazi wao wakila bure kwa kutotaka kufanya shughuli za kuingizia kipato.


Tabora. Wakati kilio cha watu kukosa ajira hasa kwa vijana kikiendelea kushika kasi, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda, amesema kuna idadi kubwa ya wasomi wanaoishi kwa wazazi wao wakila bure kwa kutotaka kufanya shughuli za kuingizia kipato.

Makinda ametoa kauli hiyo leo ijumaa, Septemba 23, 2022  alipokuwa akizungumza na kamati za Sensa za Mkoa wa Tabora ambapo amesema jambo hilo halifurahishi kwa sababu elimu anayopata mtu anatakiwa aitumie kupambana na mazingira.

"Tumeambiwa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na wala sio ufunguo wa ajira, watu wanahangaika kila kukicha kusaka ajira" amesema

Kamisaa Makinda amesema idadi ya watu inazidi kuongezeka kila kukicha na mbaya zaidi wengi hawafanyi kazi.

“Ni jambo la kushangaza kuona wasomi hawapendi kujishughulisha na vitu vya kuwaingizia kipato, hawafanyi  hata biashara wakati wasiosoma wanafanya shughuli za kuingiza kipato” amesema.

Ameongeza kuwa Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwezi uliopita itasaidia kupatikana kwa takwimu zitakazotumika kutunga sera mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, alimweleza Makinda kuwa makarani wa sensa wawili walifariki mkoani humo ambapo mmoja alijiua kutokana na matatizo ya kifamilia na mwingine alifariki akiwa katika nyumba ya wageni aliyofikia baada ya mafunzo ya siku 21.

Amesema mwingine alijeruhiwa baada ya kupata ajali wakati akienda kutuma taarifa za Sensa na mguu wake kushoto kusagika na hivyo kukatwa na hivi sasa wanafanya utaratibu wa kumtafutia mguu wa bandia.

Dk Batilda amesema awali walikadiria kuhesabu kaya 490,000 lakini hasa wanakamilisha walihesabu kaya 577,128 sawa na asilimia 118.