'Maonyesho ya ubunifu yatahamasisha wanafunzi kupenda sayansi'

Muktasari:
- Wito umetolewa kwa mikoa na wilaya kuwa na maonesho bunifu na miradi ili kukuza vipaji kwa wanafunzi.
Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa mikoa na wilaya kuwa na matamasha na maonesho ya kazi za bunifu za sayansi na teknolojia zinazofanywa na wanafunzi ili kutoa hamasa kwa kundi hilo kupenda masomo ya sayansi.
Hatua hiyo itawezesha Taifa kuwa na uhakika wa wanataaluma katika fani hizo zenye mchango mkubwa katika kuendesha dunia.
Hayo yameelezwa leo Desemba 5, 2023 na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas)anayeshughulikia taalum, Profesa Bruno Sunguye wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi wa sekondari zilizoandaliwa na taasisi ya Young Scientist Tanzania (YST) na kufanyika Dar es Salaam.
Profesa Sunguye ambaye amemwakilisha Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema uwepo wa maonesho ya aina hiyo huibua hamasa kwa wanafunzi na upo uwezekano wa vijana wengi kuvutiwa na masomo hayo.
Amesema mashirika kama vile YST yana jukumu muhimu katika kukamilisha juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ili kutoa jukwaa muhimu ndani ya mfumo wa shule za sekondari nchini Tanzania kwa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (S.T.E.M.), ambayo ni masomo ya kimsingi na muhimu kwa maendeleo katika uchumi na jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Sunguye masomo haya yanaunda msingi wa uchumi unaotegemea maarifa na ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza uvumbuzi, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
“Ni muhimu kwa wadau wengi zaidi kupiga hatua mbele na kuchukua hatua sawa ili kuunga mkono juhudi za kupongezwa zinazofanywa na serikali yetu katika kukuza uchumi unaoendeshwa na sayansi na teknolojia.
“Vijana hawa ni wa mfano wanatuonesha tunayo hazina kubwa ambayo ikiendelezwa sayansi na teknolojia inaweza kupata msukumo kupitia vijana hawa. Tuendelee kufanya maonesho kama haya ngazi ya mikoa ili kutengeneza wanasayansi wengi,” amesema Profesa Sunguye.
Awali Mwenyekiti wa bodi ya YST Prof Yunus Mgaya amesema kupitia miradi hiyo Taifa linapata matumaini ya kuwa na wasayansi siku zijazo.
“Niwapongeze wanafunzi waliojitoa na kuwekeza nguvu zao kwenye kuandaa kazi walizoonesha kwenye maonyesho.
"Hawa wanaleta matumaini kwamba taifa letu litakuwa na wanasayansi huko mbeleni.Kinachofanyika matokeo yake ni zaidi ya ushindi wa wanafunzi bali kuzidi kuwatia moyo kupenda sayansi na teknolojia," amesema.
Naye mwasisi wa YST, Dk Gozbert Kamugisha amesema maonesho hayo yanafanyikwa kwa mwaka wa 13 na yamekuwa kivutio kwa wanasayansi wachanga.
“Kinachofanyika kutambua mchango unaofanywa na wanafunzi wa shule za sekondari wanaobuni na kuonyesha kazi zao za kibunifu.
“Tumekuwa tukihamasisha na kukuta matumizi ya teknolojia kwa wanafunzi, msisitizo wetu katika teknolojia umeifanya YST kuwa taasisi inayotengeneza wanasayansi wachanga,” amesema Dk Kamugisha.
Mwakilishi wa taasisi ya Karimjee Foundation ambayo ni mdhamini mkuu wa maonesho hayo, Vinoo Somaiya amesema taasisi hiyo inalenga kuwatengenezea kesho nzuri vijana wanaowekeza nguvu zao kwenye sayansi na teknolojia.
“Foundation inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watakaoshinda. Lengo ni kuhamasisha wanafunzi wengi kusoma sayansi na teknolojia na kuwa wabunifu. Tunataka kuwa na taifa la vijana wabunifu,” amesema Sumaiya.