Mauaji ya wageni yanavyoendelea kusumbua Afrika Kusini

Neno ‘xenophobia’ kwa raia wa kigeni walioko Afrika Kusini ni miongoni mwa maneno yanayochukiza, kupingwa na kuwaingiza wengi katika dimbwi la mawazo wanapofikiria ama yaliyowatokea wao wenyewe au wapendwa wao.

Xenophobia linatumiwa na raia wa Afrika Kusini kama mkakati au shinikizo kutaka kuondolewa kwa wageni walioko nchini humo hususani wanaotoka katika mataifa ya Afrika na ambao wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo wenyeji wanaona ni kama kuwapoka ajira.

Katika wiki za karibuni takribani watu wanne wameripotiwa kuuawa kutokana na maandamano ya kushinikiza kuondolewa kwa wageni hao.

Agosti mwaka 2018, chama cha kisiasa kinachopinga wageni wa namna hiyo, kilitoa tamko kutaka raia wasio wa Afrika Kusini kuondoka nchini humo. Waandamanaji takribani 150 waliingia mitaani kushinikiza Serikali kuwaondoa wote wanaoishi bila ya vibali.

Maandamano hayo yalifuatiwa na vurugu katika eneo la Soweto, jijini Johannesburg ambapo polisi inasema watu 27 walitiwa mbaroni huku wawili wakifunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji.

Machafuko kama hayo yameibuka tena wiki iliyopita katika mji wa Kwazulu Natal. Akizungumza na Shirika la Habari la BBC, Mtanzania anayeishi Kwazulu Natal, Egbert Mkoko anasema hali sio shwari hususan kwa raia wa Zimbabwe, Malawi na Ethiopia ambao wapo kwa wingi Afrika Kusini wakitafuta maisha.

Mkoko anasema kuwa kuna baadhi ya watu wanaodaiwa kuuawa.

“Vurugu zilizotokea hapo awali zimeibuka tena na chanzo ni kwamba raia wa kigeni wanaoishi nchini humu wanachukua kazi za raia wa taifa hilo,” anasema.

Hata hivyo, anasema mpaka juzi hakukuwa na suluhu yoyote iliyotolewa na Serikali hatua ambayo imewafanya raia wengi wa kigeni kusalia majumbani.

Anaongezea kuwa hali ni ngumu kwa wageni kwa kuwa wanaishi kwenye maeneo ya raia wa kipato cha chini mchini humo. Mkoko anasema kuwa siku kadhaa zilizopita raia wengi wa kigeni walijaa kwenye vituo vya polisi katika mji wa Durban.

Kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters, Julius Malema, anakemea vikali xenophobia akisema ni unyama usiostahili kufanywa na Waafrika Kusini kwa ndugu zao wa Afrika.

Malema anasema hata kama atachukiwa kutokana na msimamo wake huo lakini yupo tayari kuutetea kwa gharama yoyote kwa kuwa kinachofanywa si sahihi na hakistahili kufanyika kwa watu waliosaidia kupambana kuhakikisha Afrika Kusini inakuwa huru.

Madai yanayolewa na wahamasishaji wa vurugu hizo ni kuwa wageni wanateka ajira za Waafrika Kusini. Hata hivyo, watafiti mbalimbali wanasema utafiti unaonyesha wageni wamekuwa sehemu ya wazalishaji wa ajira nchini humo.

Msimamo wa wanaopinga

Sharon Ekambaram, ambaye anaongoza kikundi cha wanasheria wa kutetea haki za wakimbizi na wageni walioko Afrika Kusini cha Lawyers for Human Rights, baada ya kuibuka machafuko kama hayo mwaka jana aliahidi kufungua kesi dhidi ya wenye kuchochea jambo hilo.

Anasema matamko na hotuba za uchochezi, zilizo kinyume na sheria za Afrika Kusini zinachangia kwa kiasi kikubwa kukuza vurugu na jambo hilo halipaswi kuachwa.

“Ni hatari sio tu kwa wageni, kaka na dada zetu kutoka nchi jirani, bali ni hatari pia kwa Waafrika Kusini na maskini. Taasisi za kisheria zinapaswa kuchukua hatua. Polisi ichukue hatua dhidi ya vitendo hivi visivyo vya kisheria,” anasema Sharon.

Chama tawala cha ANC mara kadhaa kimekosoa na kulaani vurugu kama hizo na kusema xenophobia haipaswi kupewa nafasi nchini humo.

Raia wa Malawi anayeishi Afrika Kusini na kufanyakazi katika salon ya kusafisha kucha, Tasira Banda, anasema Waafrika Kusini hawataki kujishughulisha na shughuli ndogondogo kama aifanyayo.

“Wanatuambia wageni tunaiba kazi zao. Ni sawa, lakini ni kwa kuwa hawafanyi ninachofanya. Wanaweza kusema wageni tunawachukulia wake zao, sawa, lakini ni kwa kuwa hawawaungi mkono. Wanachofanya ni kunywa bia na mengine yasiyo na tija, basi,” anasema.

Historia

Tatizo la ubaguzi na raia wa Afrika Kusini kuwatimu wageni lilianza kushika kasi baada ya kukoma kwa utawala wa kibaguzi na nchi hiyo kutawaliwa na wazawa.

Kati ya mwaka 1984 na mwishoni mwa utawala wa makaburu 1990, watu wanaokadiriwa kuwa kati ya 50,000 na 350,000 kutoka nchi jirani ya Msumbiji waliingia Afrika Kusini, na ingawa hawakupewa hadhi ya ukimbizi lakini waliruhusiwa kuishi maeneo ya watu weusi na kushiriki shughuli mbalimbali.

Baadaye kati ya mwaka 1993 na 1997 raia wengi wa Congo walikimbilia nchini humo kutokana na mapigano ya nchini mwao ambapo waliishi na kupata elimu lakini baadae uliibuka mjadala baada ya kudaiwa kubaguliwa katika haki ya msingi ya huduma za afya.

Tafiti mbalimbali ikiwamo iliyofanywa na Mpango wa wahamiaji kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SAMP) na kuzihusisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Afrika Kusini ilionekana kuwa na matukio na viashiria vingi zaidi vya unyanyasaji dhidi ya wageni.

Mwaka 1998 raia mmoja wa Msumbiji na wawili wa Senegal walirushwa nje ya treni huku ikitembea kitendo kilichofanywa na kikundi cha watu waliodai wageni wamekuwa sababu ya ukosefu wa ajira na kusambaa kwa virusi vya ukimwi.

Mwaka 2000, raia saba wa kigeni waliuawa Cape Flats wakati wa wiki tano za machafuko. Polisi walieleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wenyeji kuhofia wageni watadai umiliki wa mali kutoka kwa Waafrika Kusini hapo baadaye.

Katika wiki ya mwisho ya 2005 na wiki ya kwanza 2006, watu wanne wakiwamo raia wawili wa Zimbabwe waliuawa katika makazi ya Olievenhoutbosch, baada ya kudaiwa kuhusika na kifo cha Mwafrika Kusini. Mali zao ziliharibiwa na raia katika eneo hilo waliwataka polisi kuwaondoa wageni wote.

Januari 2008 raia mmoja wa Somalia aliyekuwa akimiliki duka huko Eastern Cape aliuawa. Machi 2008, watu saba wakiwamo raia wawili wa Zimbabwe waliuawa na maduka yao kuchomwa moto.

Msimamo wa Serikali

Rais Cyril Ramaphosa amelaani machafuko yaliyoibuka na kuwataka Waafrika Kusini kuachana nayo kwani yanakiuka uhuru wa watu wengine. Akizungumza kwa nyakati tofauti ikiwamo katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na ANC Jumatatu, Ramaphosa aliagiza taasisi zinazohusika na masuala ya kisheria kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuhusika.

“Afrika Kusini ni nchi iliyopata uhuru kwa ushirikiano na msaada kutoka kwa wapambanaji wengine katika bara letu na dunia nzima,” alisema. Kwa mara nyingine KwaZulu Natal imekuwa kitovu cha machafuko hayo baada ya watu wawili kuripotiwa kuuawa wiki iliyopita. Wakazi wa eneo hilo waliueleza mtandao wa habari wa News24 kuwa baadhi ya wageni walitimuliwa katika nyumba zao na kuomba hifadhi kwenye nyumba za ibada.