Mbunge Silaa alalamikia mfumo wa Tehama, ataka mifumo itambuane

Muktasari:

  • Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa amesema mpango wa Serikali wa Bima ya afya kwa wote hautaweza kufanikiwa ikiwa Watanzania hawataunganishwa katika mfumo wa pamoja wa mtandao.

Dodoma. Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa amesema mpango wa Serikali wa bima ya afya kwa wote hautaweza kufanikiwa ikiwa Watanzania hawataunganishwa katika mfumo wa pamoja wa mtandao.

 Silaa ametoa kauli hiyo leo Mei 20, 2022 wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Habari, Mwasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo amesema kitendo hicho kimekuwa kikiikosesha Serikali fedha nyingi.

Mbunge huyo amesema Tanzania inapata hasara kubwa inayotokana na kutokuwepo kwa kitu cha muunganisho na akashangaa hadi sasa hakuna mfumo wa pamoja ambao utafanya vitu vingi vionekana katika eneo moja.

Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato kwa Wizara yake, Waziri wa Habari Nape Nnauye amesema hivi sasa Tanzania ina watumiaji wa simu 55 milioni wakati watumiaji wa intaneti wanafikia 29 milioni.

Kwa mujibu wa Silaa, Taifa haliwezi kufikia malengo waliyojiwekea kwa sababu ya mifumo kutokuwa pamoja huku mingine ikisimamiwa na Wizara ambazo si wahusika wa moja kwa moja wa mifumo kama Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora.

“Mtu mmoja anatembea na vitambulisho lundo, NIDA, Rita, NHIF, Kadi za CCM, Leseni ya udereva, TIN namba, kadi ya Yanga na kadi za benki hadi unakuwa ni mzigo, hivi tunakwama wapi,” alihoji Silaa.

Ametolea mfano katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ukurasa wa 348 kwamba ilibaini upotevu wa Sh224 bilioni kutoka kwa Tanroad lakini chanzo chake ni kutokuwa na mfumo mzuri.

Mbali na Tanroad, lakini alitaja eneo lingine ambalo fedha nyingi zimepotea ni bodi ya mikopo ya vyuo vikuu ambayo inaeleza upotevu wa Sh428 bilioni kwa kushindwa kuwatambua wakopaji 155,725 jambo alilosema linashangaza sana.