Msomera kujengewa bwawa la Sh1.9 bilioni kwa ajili ya mifugo

Msomera kujengewa bwawa la Sh1.9 bilioni kwa ajili ya mifugo

Muktasari:

  • Wakati mawaziri wawili wakiweka kambi katika kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kushuhudia watu waliokubali kuhamia kwa hiari, Serikali imetenga Sh1.9 bilioni kwa ajili ya kujenga bwawa litakalotumika kunyweshea maji mifugo.

Handeni. Wakati mawaziri wawili wakiweka kambi katika kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kushuhudia watu waliokubali kuhamia kwa hiari, Serikali imetenga Sh1.9 bilioni kwa ajili ya kujenga bwawa litakalotumika kunyweshea maji mifugo.

Juzi uongozi wa Mkoa wa Tanga na kijiji hicho uliwapokea wakazi waliokuwa wakiishi katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambao walikubali kwa hiari yao kupisha uhifadhi katika eneo hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, walishuhudia kaya 20 zikiwasili eneo hilo na kupata mapokezi makubwa huku Serikali ikiahidi kuendelea kuboresha mazingira ili wahusika waishi vizuri.

Waziri wa Maji

Akizungumza akiwa kijijini hapo, Waziri Aweso alisema uwekezaji wa miundombinu ya maji ipo tayari na maji yaliyopo yanatosheleza wananchi hao na mifugo yao.

Aweso alisema mahitaji ya maji katika eneo hilo ni lita 458,000 na kwa sasa tayari visima vimeshachimbwa na vinatoa lita 558,000 za maji ambayo yameshaunganishwa kwenye majengo ya kutolea huduma, yakiwemo ya zahanati na shule.

“Kwa lugha nyepesi tuna maji toshelevu, lakini pia tumepata Sh1.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa bwawa ambalo litakuwa na maji mengi yatakayowasaidia wananchi na mifugo yao, ili wasipate usumbufu. Tunao wataalamu wanaendelea na uwekaji wa miundombinu ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama muda wote,” alisema Aweso.

Kauli ya Waziri Chana

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alisema mifugo na mali nyingine za kaya 20 za wananchi waliohamia kwa hiari Kijiji cha Msomera zimewasili kijijini hapo na taratibu za kuwakabidhi wahusika zinaendelea kulingana na utaratibu uliowekwa.

Juzi Waziri Chana aliwaambia waandishi wa habari hati miliki zimekamilika na watakawakabidhi wahusika.

“Kaya hizi zimeshahamia na juzi wamelala kwenye nyumba zao, jambo la kushukuru Mungu ni kwamba mifugo yao pia imefika salama.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima alisema ni jambo la kushukuru kuona wageni hao wamefika salama na wamepokelewa pamoja na mifugo yao na mali nyingine.

Usalama

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo alisema hali ya ulinzi na usalama katika kijiji hicho imeimarishwa.

“Tumepokea ugeni wa wenzetu kutoka Ngorongoro, niwahakikishie hali ya ulinzi wilayani Handeni imeimarishwa na tuna kituo cha polisi na askari wa kutosha pamoja na vitendea kazi, hivyo niwatoe hofu na kuwakaribisha kwani Tanga iko salama,” alisema Kamanda Safia.

Wananchi watoa kauli

Paulo Tirike, mmoja wa waliohamia kijijini hapo kutokea Ngorongoro, alisema anapongeza hatua ya Serikali kuwapatia hati ya umiliki wa maeneo waliyopewa pamoja na nyumba za kisasa.

Akizungumza na Mwananchi, alisema walipokuwa Ngorongoro walikuwa wakiwasiliana na ndugu na jamaa zao waliokuwepo Msomera na waliwatoa hofu kwamba eneo hilo ni zuri na kila kitu kimewekwa katika utaratibu mzuri, hivyo wasisite kuhamia.

“Kwenu suala la nyumba kwa kweli limetufurahisha. Nyumba ni nzuri, lakini kama mnavyojua sisi ni wafugaji Serikali imetutengea na maeneo ya malisho pamoja na mashamba ambayo tutalima chakula. Tunashukuru na hati tumepewa, sasa mimi namiliki ardhi. Ni ajabu kwa Mmasai na nawaambia waliobaki Ngorongoro waje hapa ni pazuri na hakuna wizi wa mifugo, kwani tumewadhibiti,” alibainisha Tirike.

Wamasai waandamana

Wakati Serikali ikiendelea na kazi ya kuweka mipaka katika eneo la Loliondo na kuwahamisha baadhi ya wakazi walioridhia kuhama ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, jana Wamasai kutoka maeneo mbalimbali nchini walifanya maandamano ya amani hadi ubalozi wa Kenya nchini kuiomba Serikali ya Kenya kuingilia kati upotoshaji unaofanywa na zilizodai kuwa ni asasi za kiraia na wanaharakati waishio nchini humo.

Katika barua ya pamoja waliyoiwasilisha ubalozini hapo ambayo imesaniwa na aliyejitambulisha kuwa ni Katibu wa Umoja wa Wamasai hao, loishiye Lashilunye, ilisomwa na kiongozi wa msafara huo, Emmanuel.

Lashilunye alisema upotoshaji huo unalenga kuichonganisha jamii ya Wamasai na Serikali ya Tanzania, pamoja na kuzorotesha jitihada mbalimbali za makubaliano zilizofikiwa na pande zote mbili.

“Licha ya Serikali kutanabahisha uwepo wa makazi mapya katika eneo la Handeni, kumetokea upotoshaji na uchochezi unaolenga kukwamisha zoezi hili.”