Mutasa, mhitimu aliyeisotea PhD kwa miaka 41

Samuel Mutasa in a past interview

Muktasari:

Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikifanya mahafali yake ya 50 leo, Mzee Samuel Rugaiyamu Mutasa, atakuwa kivutio cha pekee pale atakaposimama na kuwa miongoni mwa wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD).

Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikifanya mahafali yake ya 50 leo, Mzee Samuel Rugaiyamu Mutasa, atakuwa kivutio cha pekee pale atakaposimama na kuwa miongoni mwa wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD).

Akiwa na miaka 82 Mutasa anaitia kibindoni shahada yake ya uchunguzi wa kikemia wa baadhi ya mimea lishe na mimea dawa ya jamii ya kasia (Cassia (L). Ni safari aliyoianza miaka 41 iliyopita.

Umri wake, ugunduzi wa ‘kampaundi’ katika mimea mbalimbali na ujasiri wake wa kupambana kutimiza lengo lake, vimemweka katika kundi la watu wachache wa umri wake waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu ya kemia nchini.

Mzee Mutasa anayeonekana kuwa na nguvu za kutosha amewahi kutumia pia elimu yake ya mimea kuzalisha dawa za mimea kusaidia watu wenye matatizo ya kisukari cha kupanda, tezi dume na magonjwa ya ngozi.

Katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi, Mzee Mutasa anaelezea safari ya maisha yake kusaka elimu, matatizo na mafanikio aliyoyapata katika utaalamu wa kemikali.

Anaamini kuwa elimu aliyoipata si kwa ajili yake binafsi bali ni kwa ajili ya jamii inayomzunguka na Taifa kwa ujumla.

Akiongea kwa sauti ya chini lakini yenye uhai wa kutosha, Mzee Mutasa anasema alitokea kupenda kemia tangu akiwa mtoto.

“Tangu utoto wangu nimekuwa rafiki na hilo somo. Nakumbuka sisi tulisoma Ilboru, wakati ule inaitwa Lutheran Ilboru Secondary School na tulipotoka kule wakatuchagua kwenda Tabora School ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa. Tuliwakuta wenzetu lakini I still shone out (niliendelea kung’ara) katika kemia. Mwaka 1960 nikapata zawadi kutoka kampuni ya mafuta ya Shell kwa kuwa mwanafunzi bora katika somo la kemia.

Baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya kemia mwaka 1968 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alichaguliwa kuwa mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyakato iliyopo Bukoba, mkoani Kagera. Hii ilikuja baada ya wizara kumkatalia kwenda kusoma ya kemia na jenetiki nchini Denmark baada ya kupata ufadhili.

“Kwa hiyo I was disappointed (nilivunjika moyo) kukosa hiyo nafasi.Hiyo ilikuwa mwaka 1968 lakini hamu yangu ya kujiendeleza katika masomo ilibaki kama deni. Nilijaribu kuwaomba tena niende wakakataa na wakanituma kufungua Shule ya Sekondari ya Sengerema na haukupita muda wakanileta makao makuu ya wizara ya elimu mwaka 1972,” anasema.

Kuletwa Dar es Salaam kulitoa nafasi nyingine kwa mzee huyu kutimiza ndoto yake ya kuendelea kusoma. Kwa bahati, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa kimeanzisha programu ya shahada ya kemia. Huo ulikuwa mwaka 1975. Alikubaliwa kujiunga na kufanikiwa kumaliza mwaka 1977.

Kufuatia kufaulu vizuri katika masomo hayo, UDSM walimshawishi abaki pale kwa masomo ya juu na baada ya mvutano kati ya wizara na chuo, wizara ilikubali kumlipia kwa ajili ya program ya shahada ya uzamifu mwaka 1979.

Ukosefu wa vifaa

Wakati akiendelea na program ya PhD, wakati huo kulikuwa na changamoto kubwa ya vifaa vya kupima mimea na kufanyia tafiti za kisayansi.

“Tulichokifanya ni kukata mizizi au majani halafu unayachambua na unapata kampaundi nyingi. Sasa, haya huwezi kuyasoma tu bila kuwa na instruments (vifaa). Kuna vifaa vingi hatukuwa navyo.

“Kwa hiyo ukipata hiki lazima ukitume overseas (nje ya nchi) ama kama utapata ufadhili utakwenda nje kwa muda mfupi kufanya kazi kwenye vifaa au unafanya kazi mtandaoni ambayo haikuwa inapatikana kwa urahisi wakati huo,” anasema.

“Sasa katika harakati hizo wakanipa miezi sita ya kwenda Uingereza, nikafanya kazi kidogo kwa matumaini kwamba nikirudi hapa tutakuwa tunawatumia hizo kampaundi kwa sababu nitakuwa na contact (mawasiliano) tayari na wao wanazifanyia kazi.

Kabla hajarudi nchini, wizara ya elimu ilimtaarifu kuwa alitakiwa nchini ili awe Mkuu wa Chuo cha Ufundi Dar es Salaam.

“Niliendelea kuwasiliana nao na nilipomaliza kazi jioni niliingia kwenye maabara kufanya shughuli zangu. Ilikuwepo changamoto kubwa. Hiyo ilikuwa miaka ya 1980, basi, unatuma kazi nje lakini wakati mwingine zinafika na wakati mwingine zinapotelea humo ndani.

“Sasa kilichofuata nikaona nisipokuwa careful (makini) hii kazi yangu yote niliyoianza tangu mwaka 1977 inaweza kuishia hewani.

Kazi kubwa aliyofanya katika masomo yake ilikuwa ni uchunguzi wa awali wa maandiko kuhusiana na mimea lishe na mimea tiba aliyoifanyia kazi.

Anasema lengo kubwa na kazi na tafiti zake ni kuthibitisha, kwa mfano, ni kampaundi gani zinapatikana kwenye miti inayotumika kama dawa na kujua kama inafanya kazi dhidi ya bakteria na fangasi.

“Sasa ukishathibitisha hilo unai-relate (unaihusisha) na matumizi ya dawa za asili wanazotumia. Tunaangalia kama wanatumia zaidi majani, mizizi au shina kupata dawa zao. Kama hizi compound (msondo) zimo katika hivi vyote, tunakwenda mbali zaidi na kujua quantity (kiasi) kingi kipo kipo wapi; je, ni kwenye mizizi, shina au majani? Hii itakuambia ni kwa nini wanapendelea zaidi mizizi kwa dawa fulani au majani kwa dawa nyingine.

Vikwazo vyaanza

Wakati kazi hiyo ikiendelea, Mzee Mutasa anasema (msimamizi wake katika masomo ya PhD aliondoka nchini na akapewa mwingine ambaye naye aliondoka kabla ya yeye kukamilisha masomo yake.

“Hali hii ilisimamisha shughuli zake kwa muda mrefu. Aliendelea kuandika machapisho mbali mbali ili kuilinda kazi yake.

“Machapisho yalisaidia kuilinda hiyo kazi mwingine asije akasema ni kazi yake. Sasa hiyo ikanisaidia kujua kuwa hata compound (msondo) ambazo wengine walikuwa bado hawajaziona kusema kweli ni mimi nimegundua wa kwanza.

Anasema kuchelewa kwake kumaliza shahada hiyo aliyoisomea kwa miaka 41 kumetokana na sababu nyingi.

“Mara nyingine local supervisor (msimamizi wa ndani hakuna). Vifaa vuipo lakini nani atasimama nafasi ya huyo msimamizi?

Mwaka 2012 aliomba apewe msimamizi wa ndani wa program yake ya PhD baada ya kuona muda unazidi kupotea huku pesa nyingi zikiwa zimetumika.

‘’Nikaenda pale, nikawaomba ndio wakakubali kunipa msimamizi wa ndani. Wakati ule nilikuwa nimekwishaandika karibu kila kitu, huyo msimamizi alipaswa kusoma na kutazama kama kazi yangu inakidhi vigezo vya kutunukiwa PhD.

“Sasa ikabidi nizunguke kutafuta pesa kwa sababu walikuwa wanataka karibu Sh6 milioni ambazo sikuwa nazo. Hatimaye watoto wangu wakasema hapana, tutalipa, wakanichangia na ndio nikamlipa yule msimamizi akaanza kazi ya kuisoma, kuirekebisha pale na kuipanga,” anasema.

Umri si kikwazo

Mzee Mutasa anasema umri si kikwazo na hautakuwa kikwazo kwa yeye kujiendeleza kielimu. “Haujawahi kuwa kikwazo, yaani mimi mentally (kiakili) nimekuwa nikijihisi kama kijana, labda mentally (kiakili) mimi nina miaka thelathini (anacheka). Kwa sababu hata nikikuonesha vitabu nilivyoandika utaamini.

Tayari Mzee Mutasa amendika vitabu takribani saba kuhusu masuala mbalimbali ya maisha kikiwemo kitabu cha malezi kwa watoto, jinsi ya kudumisha ndoa, watoto na matatizo yao na vya kemia kuhusiana na faida za mimea tiba.

Ugunduzi mkubwa

Anasema kuna kampaundi (misondo) kadhaa ambazo amezigundua yeye na hakuna mtu mwingine anaweza kujitokeza na kudai amezigundua.

“Ni mimi, hizo ni zangu. Ningesema kuna takriban kampaundi nane ambazo hizo ni zangu. Kuna nyingine ni structure (maumbo) mpya kabisa.

Abuni dawa

Mzee Mutasa hakuishia tu kufanya tafiti za mimea bali amewahi kutengeneza dawa kwa kutumia mimea tiba.

“Nimewahi kujaribu na kama ingekuwa wakati wa Magufuli, huyu ambaye ana-encourage (anasisitiza) viwanda si ajabu ningekuwa mbali. Nimewahi kutengeneza dawa ya kupaka ya ngozi. Mmoja wa madaktari aliyebobea katika magonjwa ya ngozi na mzio alikuwa akitumia dawa hizi kwa wagonjwa wake.

Somo kwa vijana

Anasema kuna mambo mawili ambayo vijana wanapaswa kuyazingatia. Kwanza, kuna kupanda na kushuka katika kutafuta umahiri katika elimu.

‘’ Pili, watu wamekuwa wakikwepa masomo ya sayansi. Sasa hiki nilichofanya ni somo tosha. Kama mzee nimeweza kusoma sayansi nikiwa na miaka 80, wewe je mwenye umri wa miaka 20 au 30 vipi?’’ anahoji.