Mwenyekiti jela kwa kulisha mifugo mashamba ya wakulima

Thursday October 21 2021
mwenyekitipic
By Hamida Shariff

Morogoro. Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Morogoro, Lucas Lemomo, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kuingiza mifugo kwenye mashamba na kuharibu mazao ya wakulima.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Tarafa ya Ngerengere, Godfrey Ng'itu, ameridhika kuwa mwezi Agosti mwaka huu mshtakiwa aliingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima watatu kwa makusudi na kuharibu mazao yao.

Ushahidi unaonesha kuwa moja ya shamba aliloharibu mshitakiwa huyo ambaye ni mfugaji wa jamii ya kimasai ni lenye mboga aina ya matembele na mahindi, vyote vikiwa na thamani ya Sh79,000.

Mfugaji huyo alidaiwa pia kuharibu shamba la mkulima mwingine lilikuwa na mahindi, kunde na mbaazi vyenye thamani ya Sh240,000.

Mahakama ilipokea ushahidi wa wakulima walioharibiwa mazao ambao ulioungwa mkono na ushahidi wa Diwani wa Viti Maalumu wa Tarafa ya Ngerengere, Mariamu Chamile, kabla ya kumtia mshtakiwa hatiani.

Mshitakiwa huyo anakanbiliwa nakesi nyingine ya kuharibu mazao ambayo hukumu yake itasomwa Novemba 3, mwaka huu.

Advertisement

Akijitetea, mshtakiwa huyo aliiomba apewe adhabu ndogo kwa madai kuwa ana familia inayomtegemea wakiwemo wake zake watatu na pia ni kiongozi ambaye anategemewa na wananchi.

Hakimu alitupilia mbali utetezi huo akisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake, hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni kiongozi ambaye alipaswa kuonesha mfano.

Alisema anatoa adhabu hiyo iwe pia fundisho kwa viongozi wengine wanaotumia madaraka yao kuharibu mali za raia.


Advertisement