Ng’enda awaonya wabunge kurushiana maneno

What you need to know:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda amewataka wabunge kuishi kwa kuheshimiana, kuvumilia na kutorushiana maneno.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda amewataka wabunge kuishi kwa kuheshimiana, kuvumilia na kutorushiana maneno.

Ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 14, 2021 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Huku akieleza uzoefu wake wa kufanya kazi ndani ya CCM na kuwataja kwa majina wabunge waliomkuta katika chama hicho tawala, Ng’enda amesema, “nimekaa muda mrefu ninakijua sana chama chetu, ninajua uwezo wa CCM katika kusimamia msingi wa uongozi wa Taifa na hata ndani ya chama chenyewe. Inapofika kuna jambo lolote wewe kama ni mbunge, mwanaCCM au  mwananchi una mashaka lipeleke kwa CCM  litapata majibu.”

Akizungumzia kifo cha rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli amesema, “sisi makada tuliobobea vineno neno vingine tulivyoviona vinapita tulivitarajia. Ninachokiomba sisi wenye mapenzi mema,  wenye kujua kazi ya Rais Magufuli tutumie busara sana katika kusema jambo lolote lile.”

Amewataka wawakilishi wenzake wa wananchi kupima maneno wanayoyasikia kabla ya kuyatamka kwa kuwa chama hicho kina uongozi imara na kinaweza kupata majibu ya matatizo.

“Mimi ni mjumbe lakini nipo ndani ya Bunge. Tabia ya mtu kujipa ukaka wa Taifa, udada wa Taifa..., kama unaona jambo peleka kwenye  chama. Lazima tuishi kwa kuheshimiana hiki ni chombo kikubwa dunia wanatuangalia, tusirushiane vineno visivyokuwa na maana,” amesema.

Amesema wakati mwingine kama mbunge hajaelewa vizuri alichokisema mwenzake ni vyema akapata muda wa kujifunza.

“Hakuna kitu kibaya kama kumtafsiri mtu aliyesema vizuri. Umeshamchafua halafu unajiuliza utarudije kumsafisha,” amesema.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.