Ngome ya wanawake ACT-Wazalendo wachaguana, Rithe kidedea

Janeth Rithe, mshindi wa uenyekiti Ngome ya Wanawake, Chama cha ACT- Wazalendo

Muktasari:

Ngome ya Wanawake ya chama cha ACT-Wazalendo, imemteua, Janeth Rithe kuwa mwenyekiti wa wanawake akimshinda mpinzani wake, Severina Mwijage

Dar es Salam. Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo, imekamilisha safu za mchakato wa uchaguzi wa ngome ndani ya chama hicho, Janeth Rithe akiibuka mshindi wa uenyekiti wa wanawake.

Katika uchaguzi uliofanyika leo Machi 2, 2024, Rithe amepata kura 65 sawa asilimia 58.5 dhidi ya Severina Mwijage aliyepata kura 46 sawa na asilimia 41.4.

Katika uchaguzi wa ngome ya wanawake wa mwaka 2020 Rithe alishika nafasi ya pili dhidi ya Mkiwa Kimwanga.

Matokeo yametangazwa na Mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi ya chama hicho, Joran Bashange.

"Nitafanya kazi usiku na mchana bila kuchoka kazi ndiyo imeanza tutaenda bara na visiwani," amesema Rithe baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho.

Ngome ya vijana ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanya uchaguzi ambao Abdul Nondo alitetea nafasi ya uenyekiti kwa kura 66 dhidi ya Julius Massabo aliyepata kura 45.

Kwa upande wa ngome ya wazee, Yassin Mohamed ametetea nafasi ya uenyekiti kwa kura 44 dhidi ya Sendwe Ibrahim aliyepata kura 31.

Kwa hatua hiyo, ngome hizo zimekamilisha mchakato wa uchaguzi kwa kupata viongozi wapya.

Kwa utaratibu wa chama hicho, kinachofuata ni vikao vya ngazi ya juu vitakavyoaanza kesho Machi 3, 2024 kwa ajili ya kufanya mchujo wa wagombea wa nafasi za juu.

Vikao hivyo vitaanza katika ofisi za makao makuu ya chama zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam.

Nafasi za juu zinazoshindaniwa ni Kiongozi wa Chama (KC), atakayerithi mikoba ya Zitto Kabwe anayemaliza muda wake.

Katika nafasi ya KC wanaochuana ni Dorothy Semu ambaye ni makamu mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara) dhidi ya Mbarala Maharagande ambaye ni Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu katika chama hicho.

Mchuano mwingine ni katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, inayowaniwa na Juma Duni Haji 'Babu Duni' anayetetea dhidi ya Othman Masoud ambaye ni makamu wa mwenyekiti chama hicho, Zanzibar.

Nafasi ya makamu mwenyekiti mgombea aliyejitokeza ni Isihaka Mchinjita kwa upande wa Bara. Kwa Zanzibar amejitokeza Ismail Jussa na Hija Hassan Hija.

Mchujo utahusisha pia wagombea walioomba nafasi ya ujumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho.

Machi 4, 2024 wagombea wa uenyekiti na KC watafanya mdahalo kunadi sera zao na Machi 5 na 6, utafanyika uchaguzi.