Nyongeza bajeti ya dawa yapigiwa debe

Sunday June 13 2021
dawa pic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Wataalamu na wadau wa afya wameishauri Serikali kuhakikisha wanatenga fungu la bajeti ya dawa kama wanavyoidhinisha kwenye bajeti ili kuondoa malalamiko ya wananchi kutokana na upungufu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Akitaja sura ya bajeti, Dk Mwigulu alisema Sh233.3 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, ikilinganishwa na Sh200 bilioni iliyotengwa mwaka 2020/2021.

Hata hivyo, wadau wamesema kupanga pasipo kuwasilisha fedha husika katika ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, ni kuumiza wananchi ambao wanalazimika kuvitumia.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe alisema bado Serikali inapaswa kufanya juhudi katika upande huo, kwani fedha nyingi zinazotengwa katika bajeti hazipelekwi kwa ajili ya manunuzi katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Hata hivyo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mashirika ya umma na taasisi iliyotolewa Machi mwaka huu, ilionyesha mwenendo usiofaa wa utoaji wa bajeti ya dawa na vifaa tiba kwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa kipindi cha miaka mitano.

Advertisement

Kwa mujibu wa CAG, mwenendo wa utoaji wa bajeti kutoka Serikalini kwa kipindi hicho ulikuwa wa wastani wa asilimia 30.

“Katika mwaka wa fedha 2019/20, Bohari Kuu ya Dawa ilitarajia kupokea Sh200 bilioni kutoka serikalini kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaatiba vingine, lakini fedha hizo hazikupokelewa.

“Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Bohari Kuu ya Dawa ilipokea Sh315.39 bilioni kati ya jumla ya bajeti ya Sh1.04 trilioni,” ilieleza taarifa hiyo.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema suala la bajeti ya dawa ni mtazamo, shida kubwa fedha zinawekwa lakini kwenda kwenye matumizi ya dawa na vifaa tiba inakuwa tatizo.

“Serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kupeleka kwenye dawa, lakini hazifiki, hii inaumiza taasisi zinazohudumia maeneo hayo, hospitali mpaka kwa watumishi wa afya kwa maana kama hakuna vifaa tiba vya kutosha ni tatizo.”

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Issa Hango alisema bajeti ya dawa kuongezwa ni jambo lililotarajiwa kutokana na gharama za usafirishaji wa dawa kupanda kutokana na Covid 19, lakini alisisitiza suala la utekelezaji wa bajeti kusuasua.

“Serikali iajiri wataalamu wa dawa ‘wafamasia’, wanataaluma katika maeneo yao ya kazi wafanye kazi kwa weledi, lakini wataalamu wa famasia wanahitajika waliosomea kazi ya dawa waende wakasimamie eneo hilo, wasiende wasio na utaalamu,” alisema Hango.

Hata hivyo, akielezea utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, Dk Mwigulu alisema Sh265.8 bilioni zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara pamoja na ukarabati wa miundombinu ya afya.

Advertisement