‘Passport’ mpya kikwazo upigaji kura katika uchaguzi wa Kenya

Wapiga kura raia wa Kenya wakihakiki majina yao kwenye kituo cha kilichopo ubalozi wa Kenya jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Wakati wakenya wakipiga kura za kuwachagua viongozi wao, baadhi ya raia hao wanaoishi Tanzania wamekosa haki hiyo kwa sababu ya kutokuwa na pasi ya zamani ya kusafiria.

Dar es Salaam. Wakati Wakenya wakipiga kura ya kuwachagua viongozi wao, kukosekana kwa pasi za kusafiria za zamani kwa baadhi ya raia wa taifa hilo wanaoishi Tanzania, kumekuwa kikwazo kwao kutekeleza haki hiyo ya kikatiba.

Upigaji kura huo umefanyika leo Agosti 9, 2022 katika Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania, ukihusisha vituo viwili vilivyoandikisha wapigakura 492 kila kimoja kwa Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumzia changamoto katika upigaji kura huo, Said Suleiman anayeishi Kibaha, amesema maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) wamemzuia kutekeleza hilo kwa kutokuwa na pasi ya zamani.
“Nimezuiliwa kupiga kura kwa sababu pasi niliyoitumia sio ile niliyokuwa nimesajiliwa zamani, lakini tangu juzi wakati tunaelimishana kuhusu kupiga kura walisema pasi mpya inaruhusiwa.
“Kwa sababu namba za pasi ya kusafiria ya zamani zinaendana na pasi mpya, lakini leo wanatwambia haiwezekani na nimemfuata ofisa mmoja anasema hawakujua kama haiwezi kutumika,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Msimamizi wa upigaji kura wa Kituo hicho, Samwel Omwangi amesema kabla ya upigaji kura raia hao wanaoishi Tanzania walipewa muda wa kusajili pasi mpya.
Amesema tangu kuanzia Septemba mwaka jana hadi Machi mwaka huu, raia hao walipewa nafasi ya kusajili pasi hizo ili zitumike, lakini baadhi yao hawakutekeleza hilo.
Wanaowania urais nchini Kenya ni Raila Odinga wa  Azimio La Umoja, William Ruto wa Kenya Kwanza, George Wajackoyah wa Chama cha Roots na David Waihiga wa Chama cha Agano.