Profesa Mwaikambo Daktari wa kwanza mwanamke Tanzania

Daktari wa kwanza nchini Mwanamke, Dk Esther Daniel Mwaikambo akizungumza wakati wa mahojiano maalumu kuhusu Siku ya Wanawake Duniani. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Wakati Tanzania sasa ikijivunia kuwa na madaktari wanawake zaidi ya 3,000, ilimchukua miaka 20 Profesa Esther Mwaikambo (80) kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari wa binadamu.

Yeye ni mwanamke wa kwanza kuwa daktari nchini. Wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi wiki hii amefunguka mengi akielezea namna alivyosota kufanikisha ndoto zake na hata baada ya kuzifanikisha alikumbana na changamoto nyingi.

Profesa Mwaikambo, ambaye pia ni mwanzilishi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) anasema haikuwa rahisi, kwani njia yake ilijaa miba na hata alipofanikisha kupenya bado alikumbana na changamoto nyingine nje ya kazi.

Anasema ndiye daktari wa kwanza mwanamke kukumbana na changamoto nyingi katika maisha yake ya kazi na mahusiano anazozitaja bado zipo mpaka leo na zinawavunja moyo, kuwarudisha nyuma na kuwaumiza madaktari wengi wanawake.

“Katika maisha ya kazi na mahusiano kwa madaktari wanawake, wanaume wengi wamekuwa waelewa, lakini wanaume wachache si waelewa, wengi hupata matatizo, si rahisi kuyazungumza lakini wengi huishi kwa shida ili kuweza kuhudumia Watanzania, mimi ni mmoja wao,” anasema.

Kauli ya Profesa Mwaikambo, ambaye alikuwa daktari wa kwanza wa watoto mwaka 1977, inatukumbusha usemi usemao madaktari huoana wao kwa wao kama wafanyavyo wanasheria, lakini usemi huu anaupinga vikali.

“Tena ile ndiyo mbaya zaidi kwa kuwa kazi ya udaktari ni ngumu sana, hasa wanapokuwa vijana, ukishakuwa daktari mkubwa kama mimi unaweza kuwapa madaktari wengine majukumu, lakini ukiwa kijana unatumia muda mwingi hospitali,” anasisitiza.

Hata hivyo, anasema ili daktari afanye kazi vizuri hahitaji kusumbuliwa na mume akimsumbua kidogo kwa maneno au kumpiga kofi kazi haziendi. “Nimepata shuhuda nyingi sana kutoka kwa madaktari wanawake.”

Katikati ya changamoto hiyo, Profesa Mwaikambo anasema uwepo wa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania ni hatua nzuri ya kutafuta suluhu ya changamoto hizo, lakini pia kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuungwa mkono.

“Rais aliyepo ni mwanamke, tumtumie kuona atatusaidia vipi, haya mambo yote ya Mewata yanahitaji kuungwa mkono, kauli yake siku zote ametutaka wanawake kuwa mstari wa mbele, lakini bila kuwa na afya iliyo bora hatuwezi kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” anasema Profesa huyo aliyezindua kitabu cha maisha yake Machi 3, 2023 katika mkutano wa 20 Mewata.


Safari ya udaktari

Anasema alivutiwa na kazi hiyo baada ya mama yake kufariki dunia akiwa na umri wa miaka sita na alifanikiwa kutimiza ndoto zake miaka 20 baadaye.

“Wakati mama yangu anafariki nilikuwa kijijini, kwa kuwa aliugua jicho ambalo lilivimba sana kuanzia hapo nikatamani kujua kwa nini amefariki kwa maana kila mtu alisema amelogwa na anayesema hivyo ni mama wa jirani ambaye ameolewa na baba mdogo na mimi nilikuwa nampenda sana baba mdogo, kwa hiyo sikufurahi hata kidogo,” anasimulia.

Anasema hali hiyo ilimuumiza lakini hakuwa na la kufanya. “Nikasema nikiwa mkubwa lazima nijue huu uchawi unaoua mama yangu ni nini na huyu mtu aliingiaje ndani ya jicho la mama yangu na nini kikatokea.”

Anasema siku chache baadaye mdhamini wake alimchukua na kwenda kuishi naye na huko alikumbana na kazi nyingi, ikiwemo kuwapikia watoto, kwenda shamba, kuchuma kahawa, kazi ambazo hakuzipenda.

Profesa Mwaikambo anasema dada yake alipelekwa shule, hilo lilimuumiza kwa nini yeye ameachwa. “Nilimwambia baba yangu lazima na mimi nianze shule kila siku nalia wakija kuniona, nikiwa kule nalia nafanya kazi sina raha, akamwambia mdhamini wangu anipeleke shule nikasoma darasa moja na dada yangu.”

Anasema baada ya kuhitimu darasa la nne alichaguliwa kujiunga Ashera Girls ambapo kutokana na kiu ya kutaka kujua zaidi kuhusu chanzo cha kifo cha mama yake alisoma kwa bidii zaidi.

“Nilifaulu vizuri sana, wakati ule wa mkoloni unajua wachache sana tulienda kule Ashera Girls, tena ilikuwa ni pori nyumbani kwetu ilikuwa shida sana, tunakula kwa kuokota sana, unaokota nyanya na ndizi unachemsha, vyakula hakuna, kwa hiyo nilipoenda huko tunapata milo mitatu nikasema ndiyo hapahapa.

“Nikapenda shule sana, nikasoma vizuri mpaka darasa la nane, dada yangu akachaguliwa kwenda ualimu mimi nikachaguliwa kwenda Tabora Girls, shida ikarudi palepale.”

Anasema akiwa Tabora Girls mambo yalianza kuwa machungu kwa kuwa kuna kipindi baba yake hakuweza kulipia karo ya Sh20 hivyo alikuwa akirudishwa nyumbani.

“Kufika mnachukua siku tatu mpaka nne mnaenda mara daraja limevunjika, mnabaki njiani Babati mara mnafika Dodoma treni la ngongongo halijaja, mnalala mpaka siku nne unafika shule baba hajalipa Sh20 ya ada unarudi, mambo yalienda hivyo mpaka nikahitimu darasa la 12.”

Profesa Mwaikambo anasema hakufanikiwa kufaulu kuingia kidato cha tano, lakini alipata ufaulu mzuri na kuchaguliwa kujiunga na chuo cha ukatibu muhtasi na baada ya kuhitimu mwaka mmoja alifaulu vizuri.

Alianza kazi yake ya kwanza kuwa katibu muhtasi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. “Wakati huo Uhuru wa Tanzania bado nilikuwa nafanya kazi ile ofisi, sikumaliza mwaka yule bwana mzungu alikuwa anaitwa Dk Anderson na msaidizi wake Masanja sasa ile bosi akikuhitaji anakuita kwa kengele nikasema hapa sitaweza, nikaichukia hiyo kazi.”

Baada ya kufanya kazi hiyo kwa miezi sita na kuiacha, alirudi kwa dada yake ambaye hata hivyo hawakuelewana na baadaye alipata kazi ya kuwa mhudumu wa ndege.

“Nilipata kazi East African Airways, nilikuwa miongoni mwa wahudumu wa ndege wa kwanza Afrika Mashariki, tukasomeshwa tukasikia raha tunaingia kwenye ndege na tunasafiri nikaona nimeingia kwenye moto zaidi.

“Lakini Wachaga wanakuja Moshi kuniangalia nashuka kwenye ndege wanafurahi, lakini bado nikaona sisomi, ilivyofika mwaka 1961 wakati tunapata Uhuru nikaacha ile kazi,” anasema.

Baada ya kuacha kazi alipata nafasi ya kwenda kusoma nchini Urusi.

Agosti 1969 alirudi nchini na kuwa mwanamke wa kwanza daktari, licha ya mafanikio hayo alikuwa mwiba kwa madaktari wengine wa kiume, kwani wengi hawakukubali uwepo wake.

“Nimerudi nikawa tofauti na wenzangu, nimesoma udaktari kwa Kirusi na Kilatini na wenzangu wamesoma kwa Kiingereza, hali ilikuwa mbaya, nilifanya miezi mitatu maprofesa hawanielewi, hivyo nikaenda kuomba msaada wizarani.”

“Nikanung’unika kule wizarani wakanitafutia chuo New York Marekani kwenda kubrush Kiingereza changu, huko nilikuwa hospitalini huku nasoma, nikabobea kama daktari nikarudi nyumbani, nikakubalika nikaanza kazi rasmi mwaka 1971,” anasimulia.

Anasema kwa kipindi chote amefanya kazi akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili mpaka alipostaafu mwaka 1998, baadaye alisoma shahada ya uzamili kuanzia mwaka 1974 na kuhitimu mwaka 1977 na kuwa mkufunzi na hapo alipata nafasi nyingi, ikiwemo kurudi nchini Uingereza kujiendeleza katika ubobezi wa magonjwa ya watoto.

Wakati wote huo alikuwa akiandika machapisho mengi kwa kuwa alikuwa bado anasoma, lakini mambo yalikuwa magumu upande wake, anasema madaktari wanawake walianza kuongezeka lakini bado kulikuwa na ugumu na madaktari wanaume walishapata uprofesa, lakini yeye iligonga mwamba.

“Haikuwa rahisi kwa mwanamke kupanda vyeo, ilikuwa ngumu, lakini nilifanikiwa mpaka kufikia ngazi ya Profesa na mwaka 1998 nikastaafu nikaenda kufanya kazi kama Mkuu wa chuo cha Kairuki na nikaendelea kutoa machapisho yangu mpaka nikawa profesa kamili,” anasimulia.


Changamoto

Licha ya kupata changamoto katika kupanda vyeo, Profesa Mwaikambo anasema hakukuwa na mtu aliyewahi kuona daktari mwanamke, hivyo wapo waliokataa kuhudumiwa, hasa wanaume na wengine walishindwa kuamini kama kweli ni daktari.

“Kuwashawishi kwamba mimi ni daktari ilikuwa vigumu na wale wenzangu wanaume sasa hawajawahi kuona daktari mwanamke, kwa hiyo kila wakati wanaona huyu naye daktari sidhani kama anaweza.

“Kwangu nilijua ni suala la muda, nakumbuka kuna wakati nilifanywa mkuu wa kitengo cha watoto Muhimbili, kuna kijana alisema sitaweza kufanya kazi na wewe, nikakomaa nikamwambia utafanya utake usitake, lakini mwishowe aliondoka, lakini kwa sasa mimi na yeye ni marafiki wazuri na si yeye pekee, ni wengi.”

Anasema hata kupanda cheo haikuwa rahisi, “machapisho yangu siku zote yalikuwa yanasemekana kwamba yapo chini ya kiwango, mabovu hayafai, yaani maprofesa hawakunikubali, kwa hiyo nikayafungasha yote kwa pamoja nikayapeleka Kenya na nilimwambia awapelekee moja kwa moja majibu, wao wakapeleka nikawa profesa kamili.”

Licha ya hivyo anasimulia kuwa ilimchukua miaka zaidi ya minane kuwa mkufunzi kwa kuwa bado hawakumwamini kama angeweza na yeye aliendelea kupambana bila kuchoka.

Licha ya changamoto ya vyeo, anasimulia kwamba alipata changamoto katika kazi kutokana na kutumia muda mwingi kuhudumia wagonjwa na alilala hospitalini kwa muda mrefu kutokana na uchache wa wataalamu wakati huo.

“Tulilala siku tatu Temeke, kinamama walikuwa wanajifungulia Ocean Road, kutoka Ijumaa mpaka Jumatatu hujaenda nyumbani na suala la watoto walikuwa wanakufa kama nzige inatisha, lakini mpaka zilipokuja chanjo mwaka 1974 ilisaidia wakapungua vifo kwenye kifaduro, pepopunda, polio misos,” anasimulia.

Anasema baada ya ujio wa chanjo madaktari nchini walianza kufanya kazi kwa amani, kwani walitibu watoto ambao walipona na kurudi nyumbani, hali iliyoleta amani.


Kwa nini alianzisha Mewata

Profesa Mwaikambo anasema lengo la kuanzisha Mewata ilikuwa kuhamasisha wanawake kusoma masomo ya sayansi, ili kuongeza madaktari wanawake, kupunguza maradhi yanayowatesa wanawake na kusaidia changamoto zilizowakumba madaktari wanawake nchini.

Anasema pia walilenga kusaidia wanawake na matatizo ya saratani, uzazi wa mpango na hasa kusaidia wanawake walio katika tasnia mbalimbali, lakini pia wanawake ambao wapo tu majumbani kwa kuanzisha kampeni kuhamasisha wanawake wengi wajikinge na magonjwa mbalimbali.

Profesa anasema wakati anaanzisha Mewata kulikuwa na madaktari wanawake 29 pekee na sasa wapo zaidi ya 3,000.

“Wanawake tulikuwa hatuhamasishwi kusoma masomo ya sayansi, labda walikuwa wanadhani hatuna akili sana na sisi wenyewe tukayaogopa, sasa hivi mambo yamebadilika. Wapo wanaosoma ingawaje wengi bado wanayaogopa.

“Tulianzisha Mewata mwaka 1987 na sasa mambo yamebadilika, wanafunzi wa kike na kiume wanafanya vizuri. Mimi nina wajukuu zangu watoto wa dada zangu wengine wamesoma sayansi na ni madaktari wakubwa Uingereza, Marekani.

“Siku zote nilihamasisha wasichana kwa nini umuache mvulana akupite, kwa nini awe daktari na si wewe? Kwa nini awe Rais na si wewe, hali ilivyo kwa sasa ni nzuri, zamani ilikuwa vigumu wanawake waliishia kuolewa na kutunza watoto. Wazazi walitujenga hivyo, miaka 30 hujaolewa waliona unakosea.”


Mahusiano

Pamoja na mafanikio makubwa aliyoyapata, Profesa Mwaikambo ni mama wa watoto watano na wajukuu kadhaa.

“Niliolewa nikiwa na miaka 28, zamani tulikuwa hatuolewi mapema sana, angalau sisi Wachaga ilikuwa unaruhusiwa kuolewa ukiwa na umri kuanzia miaka 20 hadi 23,” anasema.

Akiwa msomi anayeamini kuhusu kujituma kwa mwanamke katika kufanikiwa, anasema yupo tofauti na wanawake walio wengi.

“Sasa hivi wasichana wenye akili wakifanya vizuri kwenye masomo wanakataa kuolewa. Suala hilo linanipa mimi changamoto kwa sababu ninaamini mwanamke anapaswa kusoma sana apate kazi, ajitegemee au afanye biashara yenye mafanikio lakini bado aolewe na kuzaa watoto awe mke, naamini sana katika hilo.

“Ninagombana na mabinti wengi kuhusu hili, wengi walioolewa hawaoni suala hilo ni la muhimu, wanawake tumewezeshwa, lakini saa nyingine inapitiliza, siwezi kuencourage msichana miaka 30 mpaka 40 na una kazi nzuri maisha na hutaki kuolewa,” anasema.

Anasisitiza kuwa ni vema kutimiza malengo ya kuwa na familia, “asizae wengi, azae wachache, lakini awalee waje kuwa kama yeye, wanawake wengine wamefanya vizuri lakini hataki kuolewa, kama umekosa watoto sawa, lakini huwezi kukosa mume ukiamua.”