Rais Samia aanika ugumu wa mradi wa maji Chalinze

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema upatikanaji wa maji katika eneo la Chalinze haukuwa rahisi kwa sababu kulikuwa na mvutano mkali baina ya viongozi ambao uliolenga kujenga.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema upatikanaji wa maji katika eneo la Chalinze haukuwa rahisi kwa sababu kulikuwa na mvutano mkali baina ya viongozi ambao uliolenga kujenga.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Machi 22, 2022 mara baada ya kuzindua mradi wa maji Mlandizi Chalinze – Mboga ulioanza Julai 2019 na kukamilika Novemba 2021.

“Nakumbuka wakati wa kampeni tulipokuwa tunapita kuomba ridhaa ya wananchi kuongoza Serikali kupitia CCM, nilijionea mwenyewe changamoto za maji nchi nzima ikiwemo mkoani Pwani, hasa hapa Chalinze baada ya kampeni nilikuja kwa tukio jingine.

“Ndiyo hiyo siku nilimuona mwanangu Ridhiwan akifoka moto mdomoni unatoka akimfokea Injinia Luhemeja kwamba usipoleta maji hapa nakushtaki kwa wananchi lakini leo nimeshuhudia kila mmoja kamuomba radhi mwenzake kwa matamshi makali lakini maji yamepatikana Chalinze leo tunavyofurahia safari ilikuwa ndefu na ngumu,” amesema Rais Samia.

Amesema Serikali imeipa upekee mkubwa mkoa wa Pwani na maeneo mengine kwa  kuwa ina dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani.

Rais Samia amewaagiza Dawasa kuhakikisha wanakamilisha mradi huo na miradi mingine ukiwemo wa  awamu ya tatu unaotekelezwa kwa Sh100 milioni ambao umefikia asilimia 90.

“Nimeambiwa kwamba mradi huu unatoa lita milioni 9.3 kwa siku na utawafikia wakazi 120,912 kwa siku, kukamilika kwake kutaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa kufikia asilimia 79 na Ilani ya CCM ni asilimia 85, Pwani ni mkoa wa viwanda tunakwenda kuzidi asilimia 85 na kwa takwimu zilizotolewa tukifikia mwaka 2025 tutafikia asilimia 100 kupata maji safi na salama,” amesema Rais Samia.