Rais Samia akerwa wafanyabiashara kukwepa kodi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan akizungumza na wageni mbalimbali pamoja na waumini wa kiislamu kwenye Baraza la Idd El Fitri ambalo kitaifa limefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam leo Aprili 10 2024. Picha na Ikulu
Muktasari:
Baraza la Idd limefanyika jijini Dar es Salaam huku Rais Samia Suluhu Hassan akizungumzia masuala mbalimbali ya ulipaji kodi, chaguzi zinazo nchini humo kuwa zitakuwa huru na haki
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi ilhali Serikali yake ilitangaza kujitenga na kodi za dhuluma ili kutoa fursa nzuri kwao kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Mbali na hilo, Rais Samia amewahakikishia Watanzania Serikali anayoiongoza imejipanga kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kwa mujibu wa sheria husika za uchaguzi na hautakuwa chanzo cha uhasama.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatano, Aprili 10, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akihutubia Baraza la Idd El Fitri ikiwa ni sehemu ya sherehe za sikukuu ya Idd. Viongozi mbalimbali wa kisiasa na kiserikali wameshiriki kwenye baraza hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA), Mama Shamim Khan ambaye aliwasilisha kwa niaba ya wanajumuiya wenzake wakati wa Baraza la Idd El Fitri lililofanyika kitaifa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia suala la ukwepaji kodi amesema wakati Serikali yake inaingia madarakani Machi 19 mwaka juzi haikutaka kujihusisha na kodi za dhuluma lakini sasa dhuluma hiyo inafanywa na wafanyabiashara kwa kuzuia mapato ya Serikali.
“Nilipomuapisha kamishna wa kodi nilimwambia nenda kakusanye kodi, tunazihitaji kwa ajili ya maendeleo lakini kodi za dhuluma hapana. Nilisema hivyo kwa kutambua Serikali inahitaji mapato yatokanayo na kodi ili kuweza kutimiza majukumu yake ikiwamo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii.
“Nilisisitiza haki kwenye ukusanyaji wa kodi nikiamini kwenye dhuluma baraka za Mungu hazipo, leo miaka mitatu baadaye napenda kusisitiza msimamo wangu wa kutokukubaliana na kodi za dhuluma,” amesema Rais Samia.
“Nafarijika tangu tulipoanza kusisitiza ukusanyaji wa kodi kwa haki makusanyo yanaendelea kuongezeka kwa mfano makusanyo yamepanda kutoka Sh18 trilioni mwaka 2021 hadi Sh24 trilioni mwaka 2022.”
Amesema kwa idadi ya Watanzania na kiwango cha biashara zinazofanyika nchini, kuna uwezekano mkubwa wa Serikali kuboresha zaidi huduma za jamii ikiwa kutakuwa na nia ya pamoja ya kuongeza mapato na kupunguza ukwepaji wa kodi.
Rais Samia ameeleza masikitiko yake kutokana na uwepo wa wafanyabiashara wanaotumia mbinu mbalimbali kukwepa kulipa kodi, hawatoi risiti wanapouza au wakitoa risiti ni zenye upungufu.
“Ulipaji wa kodi ni jambo halali kidini, ni jukumu la kila mmoja wetu kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara kulipa kodi kwa haki kuendana na sheria za nchi.
“Nilikataa kodi za dhuluma ili tuendane na misingi ya haki, lakini inasikitisha kuona wafanyabiashara wetu sasa wamegeuza, tumekataa kodi za dhuluma kama Serikali halafu wafanyabiashara wanadhulumu kulipa kodi.
“Wanadhulumu mapato ambayo yangetumika kuhudumia wananchi, pengine wanafanya hivyo kwa sababu mbalimbali labda za kisiasa, kiuchumi ili wapate utajiri zaidi na mapato mengi zaidi au kuhujumu kwa makusudi maendeleo ya wananchi,” amesema.
Ametumia jukwaa hilo kuwasihi wafanyabiashara wanaokwepa kodi kuacha dhuluma hiyo inayochelewesha maendeleo ya nchi huku akiahidi kuendelea kusimamia haki kwenye ukusanyaji wa kodi, kuboresha mifumo na kuleta wepesi katika ukusanyaji na ulipaji wa kodi pamoja na kuhakikisha kodi inayokusanywa inatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
“Imebidi niseme kwa sababu kati yetu hapa kuna wafanyabiashara wakubwa lakini inasikitisha baadhi yao wana vipenyo vya kukwepa kodi. Ni imani yangu kwamba wafanyabiashara watanielewa watalipa kodi na wananchi watadai risiti,” amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan akiwasili kwenye Baraza la Idd El Fitri ambalo kitaifa limefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam leo Aprili 10, 2024.Picha na Ikulu
Kuhusu suala la uchaguzi wa Serikali za mitaa, Rais Samia amesema anatambua huo ni uchaguzi muhimu kwa kuwa unakwenda kuchagua viongozi ambao wapo karibu zaidi na wananchi.
“Niwahakikishie dhamira ya Serikali ni kuhakikisha chaguzi zetu zinakuwa sehemu ya wananchi kupata viongozi bora wanaowataka na sio kuwa chanzo cha uhamasama kwenye jamii.
“Hivyo wito wangu kwa wadau wote wa kisiasa tukatimize wajibu wetu kikamilifu ili kuwe na uhuru na haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Nakubaliana nanyi pia kwamba vyama vya siasa vina wajibu wa kuhakikisha vinateua wagombea wazuri ili kuwapa wananchi wigo mpana wa kuchagua viongozi walio bora,” amesema Rais Samia.
Awali, akizungumzia uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma amesema Watanzania wana haki ya Kikatiba kushiriki kwenye mchakato huu wa uchaguzi iwe kwa kuomba ridhaa ya kuchaguliwa au kuchagua viongozi tunaowahitaji.
Pia, ametoa wito kwa mamlaka zinazohusiana na uchaguzi kuufanya kwa uwazi na weledi mkubwa huku wakizingatia utoaji wa haki kwa kila anayestahili ili wapatikane viongozi wanaotokana na wananchi na walio tayari kutumikia wananchi.
“Tunatoa wito kwa waislamu na wananchi wote kushiriki kikamilifu muda utakapowadia, wajitokeze kwenye hatua zote ikiwamo uboreshaji wa daftari la wapigakura na wanaoona wana sifa za kuongoza wasiache fursa hii ipite kupitia vyama vyao vya kisiasa. Tunawaasa pia wagombea na vyama vyao kuepukana na rushwa katika uchaguzi kwani inapoteza haki,” amesema Mruma.
Sera ya elimu na mafunzo
Katika salamu zake, Rais Samia pia ametumia jukwaa hilo kuzungumza kuhusu sera ya elimu na mitaala mipya akiitaka Bakwata kuimarisha shule zilizo chini ya taasisi hiyo ili ziwe mfano bora wa kuigwa katika kutekeleza sera iliyoboreshwa.
Amesema suala la elimu si la kufumbia macho. Kumekuwepo na rai mbalimbali ya hitaji la kuboresha muundo na mfumo wa elimu yetu nchini ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Amesema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la wategemezi kwenye kaya zetu kutokana na mfumo wa elimu kutowandaa wahitimu kukabiliana na changamoto na fursa za maisha baada ya masomo.
“Kwa kuzingatia uhalisia huo, Serikali iliamua kufanya mapitio makubwa ya mitalaa na sera, kazi hiyo ilikamilika mwaka jana na sera na mitaala imeanza kutumika,” amesema.
“Kupitia sera hii tumeongeza msukumo kwenye elimu ya amali na kuhamasisha elimu ujuzi, tukitarajia mhitimu ataingia kwenye shughuli za uzalishaji mali mapema zaidi lakini akiwa na stadi stahiki,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi ametoa maelekezo kwenye suala zima la maadili akiitaka Bakwata kuwalea wanafunzi kwenye mafunzo ya elimu ya dunia na ahera ili Taifa liweze kutengeneza watu wenye maadili na hofu ya Mungu.
Katika salamu zake kwenye baraza hilo, Mufti Abubakar Zubeir amemshukuru Rais Samia na Serikali yake kwa kutoa uzito kwa masomo ya dini kwa kuyapangia tahasusi.
“Tunashukuru umeyapa uzito mkubwa masomo ya dini yaliyokuwa yakieleaelea. Sasa umeyapa tahasusi maalumu na kukubali kugharamia. Masomo hayo mbali ya kujua dini yanasaidia kujenga vijana kuwa na tabia njema na maadili mema.”
Ametumia fursa hiyo kuwasihi waislamu kuendeleza na kuyalinda mafunzo waliyoyapa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.