Samia atoa msimamo kuhusu madini ya Tanzanite

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri wa Madini, Doto Biteko kukutana na wawekezaji katika sekta ya madini kujadili mfumo mzuri wa kuyalinda madini ya Tanzanite.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri wa Madini, Doto Biteko kukutana na wawekezaji katika sekta ya madini kujadili mfumo mzuri wa kuyalinda madini ya Tanzanite.

Amesema Mungu aliipendelea Tanzania kwa kuipa madini ya Tanzanite hivyo kuna haja ya kufanya jitihada kuyapa hadhi inayostahili madini hayo.

Akizungumza  leo Jumapili Juni 13, 2021 mjini Mwanza baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha madini, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema namna ambavyo biashara ya Tanzanite inafanyika hairidhishi.

“Tanzanite ni madini ambayo Mungu ameipendelea Tanzania lakini sasa hivi nchi mbalimbali ukienda utayakuta. Hili ni zao pekee la madini tunaloweza kujivunia kama watanzania.”

“Kuna haja ya kukaa kuipa jina itakayoipa upekee Tanzanite yetu, kuwa na mfumo wa kuidhibiti.

Tanzanite yote itakayochimbwa nchini inunuliwe na mashirika yanayohusika,” amesema.

Rais Samia amemsisitiza Waziri Biteko na wawekezaji kuhakikisha wanaipandisha hadhi Tanzanite na kurekebisha mauzo yake kwenye soko la dunia.