‘Serikali itunge sheria rafiki sekta ya habari’

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile

Muktasari:

  • Baadhi ya waandishi wa habari wameiomba Serikali itunge sheria ‘rafiki’ zitakazowezesha sekta ya habari kukua na kuongeza ajira zaidi.

Dar es Salaam. Baadhi ya waandishi wa habari wameiomba Serikali itunge sheria ‘rafiki’ zitakazowezesha sekta ya habari kukua na kuongeza ajira zaidi.

Wakizungumza na Mwananchi, leo Jumatano Agosti 17, 2022 waandishi hao wamesema sheria zinazotungwa hazipaswi kuumiza sekta ya habari kwakuwa habari ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Julius Mnganga, amesema sekta ya habari ni uchumi wa mtu mmoja na Taifa hivyo zinapotungwa ni lazima zichochee ustawi wake na zisilenge kukomoa waandishi.

“Sheria ni za wananchi si za Serikali hivyo wananchi wanapozilalamikia ni mbaya hakuna sababu ya Serikali kutozifanyia marekebisho” amesema

Naye Kalunde Jamal kutoka gazeti la Mwananchi, amesema anaamini Serikali itarekebisha Sheria za huduma za habari zinazolalamikiwa kuwa na vifungu vingi vinavyokandamiza uhuru wa habari na kudumaza sekta ya habari.

“Najua siku chache zilizopita Serikali iliwaita wadau wa sekta ya habari ili watoe maoni na mapendekezo ya kuboresha sekta ya habari, ninaamini katika Bunge lijalo mambo yakwenda kuwa vizuri kwenye tasnia ya habari” amesema.

Salmin Jamal, mwandishi wa kujitegemea amesema Serikali haipaswi kuwa mdhibiti wa wanahabari bali iruhusu kuanzishwa kwa Baraza Huru la Habari ambalo ndani yake kutakuwa na bodi ya ithibati.

“Sikubaliani na uwepo wa Bodi ya Ithibati na Baraza Huru, hivi vyombo vyote vinafanya kazi inayofanana ni vema likabaki Baraza Huru liwe linafanya majukumu yote” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema anaamini kuwa Serikali itafanya marekebisho katika maeneo yote yenye matatizo na yanakwamisha ukuaji wa tasnia ya habari.

Amesema Tanzania inakosa mfumo mzuri wa kuratibu vyombo vya habari na amependekeza mfumo wa vyombo vya habari vyenyewe kujisimamia.

“Tumeomba Serikali itunge sheria ambayo itatufanya tuwe chombo kimoja cha kusimamia taaluma ya habari, tunaona sheria ilivyo hivi sasa ina vyombo vingi kwa namna vitakavyofanya kazi na vina namna itakayowaacha wengine kando” amesema

Balile amesema hata hivyo wameshafanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa Serikali walionyesha nia ya dhati ya kuboresha sekta ya habari na TEF inaamini mambo yatakwenda vizuri.