Serikali yaeleza msimamo wake uwanja wa Kia

Serikali yaeleza msimamo wake uwanja wa Kia

Muktasari:

  • Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema haiwezi kupunguza ukubwa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) ili lipatikane eneo kwa ajili ya makazi.

Dodoma. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema haiwezi kupunguza ukubwa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) ili lipatikane eneo kwa ajili ya makazi.

Hata hivyo, Serikali imeahidi kujenga miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuwa wanafanya biashara kuzunguka eneo la uwanja.

Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Aprili 13, 2021 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Dk Leonard Chamuriho wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe.

Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kukaa meza ya mazungumzo ili sehemu ya kiwanja hicho imegwe na kuwapa wananchi kwa ajili ya matumizi kwa maelezo kuwa ni kikubwa na baadhi ya sehemu hazitumiki kwa ajili ya shughuli za uwanja.

Waziri huyo amesema eneo la matumizi ya uwanja huo litabaki kwa ajili ya matumizi ya uwanja wa ndege na si vinginevyo.