‘Sura’ tatu za uteuzi wa balozi Mulamula

‘Sura’ tatu za uteuzi wa balozi Mulamula

Muktasari:

  • Uteuzi wa Balozi Liberata Mulamula kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriiano wa Afrika Mashariki umetajwa kuwa na sura tatu za uzoefu, uwezo wa siasa za dunia na utendaji wake uliotukuka katika maisha ya kidiplomasia kwa miaka zaidi ya 30.


Dar es Salaam. Uteuzi wa Balozi Liberata Mulamula kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriiano wa Afrika Mashariki umetajwa kuwa na sura tatu za uzoefu, uwezo wa siasa za dunia na utendaji wake uliotukuka katika maisha ya kidiplomasia kwa miaka zaidi ya 30.

Balozi Mulamula aliteuliwa na Rais Samia Suhulu Hassan kuwa mbunge na waziri wa wizara hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi, aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Akizungumza na gazeti hili, mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia nchini, Abbas Mwalimu alisema uteuzi huzingatia wakati, malengo na matarajio ya kiongozi ndani ya kipindi chake kwamba anahitaji ushirikiano gani katika eneo la kidiplomasia kwa ajili ya kutekeleza malengo yake.

Uteuzi wa balozi Mulamula unalenga kuimarisha diplomasia ya uchumi ambayo ndio sera ya mambo ya nje ya Tanzania inayotazamwa katika biashara, uwekezaji na utalii.

“Kimsingi balozi Mulamula amekuwepo UN (Umoja wa Mataifa) muda mrefu, hivyo anafahamu siasa za dunia; kutokana na weledi wake wa diplomasia ana uwezo wa kutabiri na kutambua mabadiliko yoyote ya kimfumo na kimuundo katika dunia yanayoweza kunufaisha utekelezaji wa sera au kama kuna changamoto, ipatikane namna bora ya kuiendea ili kufikia masilahi ya Taifa,” alisema Mwalimu.

Balozi Mulamula ni nani?

Kwa mujibu wa tovuti ya Chuo Kikuu cha George Washington D.C nchini Marekani, Balozi Mulamula anatajwa kuwa mkurugenzi mwenza katika taasisi iliyojikita kwenye taaluma ya masuala ya Afrika kwa kufanya tafiti, kutoa ufadhili kwa wanafunzi, elimu na kuendesha midahalo inayohusu bara la Afrika.

Balozi Mulamula, aliyebobea katika masuala ya diplomasia kwa miaka zaidi ya 30, amewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Marekani kati ya Julai 2013 hadi Mei 2015.

Kati ya mwaka 2006 hadi 2011 alikuwa katibu mtendaji wa kwanza wa kongamano la kimataifa lililohusisha nchi 11 za Kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika kuhusu masuala ya Amani, Utulivu na Maendeleo (ICGLR).

Rais wa nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 2013 hadi Desemba 2015 akiwa na uzoefu wa kuhudumia majukumu mbalimbali aliyowakilisha Tanzania nje ya nchi kabla ya kustaafu Aprili 2016.