‘Thubutu Kuhama’ kusaidia vijana kupata fursa mbalimbali kwa njia za kidijitali

Baadhi ya vijana walionufaika na mradi wa Daring to Shift wa DOT Tanzania wakiwa na furaha baada ya kupata mafunzo ya kuwawezesha kuendeleza mawazo yao ya biashara jamii. Mradi huu wa miaka minne utanufaisha zaidi ya vijana 8000 Tanzania nzima.

Muktasari:

  • Shirika lisilo la kiserikali DOT Tanzania likishirikiana na Serikali ya Canada kupitia Idara ya Maswala ya Nje (Global Affairs) imesema vijana wakike na kiume wameanza kunufaika na mradi wa miaka minne uliopewa jina: Thubutu Kuhama ‘Daring to Shift’

Shirika lisilo la kiserikali DOT Tanzania likishirikiana na Serikali ya Canada kupitia Idara ya Maswala ya Nje (Global Affairs) imesema vijana wakike na kiume wameanza kunufaika na mradi wa miaka minne uliopewa jina: Thubutu Kuhama ‘Daring to Shift’ ambao unakusudia kuwapatia vijana zaidi ya 8,500 ujuzi wa kidijitali, kibiashara, pamoja na kuwaunganisha na mitandao wanayohitaji ili wapate fursa za kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Mradi wa Thubutu Kuhama (D2S), ambao umezinduliwa rasmi wiki iliyipita, umeanza utekelezaji wake tangu mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2023.

Mradi huo unatekelezwa katika mikoa tisa ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Tabora, Iringa, Arusha, Tanga na Zanzibar. Thubutu Kuhama, itawanufaisha moja kwa moja vijana 285 wenye umri kati ya miaka 18 na 35, miongoni wa hao vijana 200 wakiwa wa kike.

Vijana hawa wataongoza mafunzo na mipango ya maendeleo katika jamii zao katika nguzo kuu nne za mradi yaani: kazi za kidijitali, biashara ya kidijitali, ujasiriamali jamii, na uongozi wa jamii. Hivi ndivyo vijana 285 watakavyoongoza mabadiliko chanya ya kidijitali katika jamii zao;

• Vijana 110 watafundishwa kuwa Viongozi wa Jamii na wao watafundisha vijana wengine 8,000 mafunzo ya stadi za dijitali ili kuboresha biashara zao.

• Wajasiriamali Jamii (Social Innovators) 150 watawezeshwa kuanzisha biashara zenye manufaa na ambazo zitaleta ufumbuzi wa changamoto za jamii ikiwemo ajira.

• Vijana 10 watapewa mafunzo na kuwa mabalozi wa kidijitali ambapo wao watafundisha vijana wengine 500 na kuwapatia ujuzi kidijitali kuwawawezesha kuwa vinara kwenye soko la ajira.

Mpaka mradi kumalizika vijana zaidi 8,500 watanufaika huku vijana 6,000 sawa na asilimia 70 ya wanufaika ikiwa ni wasichana na wanawake.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mradi, Mkurugenzi Mkuu wa DOT Tanzania Diana Ninsiima anasema, “Mradi wetu utagusa maeneo manne kwenye biashara, kipindi cha mlipuko wa Corona mambo mengi yalibadilika na biashara nyingi hasa zile ambazo hazikuwepo mtandaoni ziliathirika zaidi kwa hiyo tutasaidia vijana wadogo kuona na kuchangamkia fursa ambazo zipo mtandaoni ili waweze kupata kazi kwenye uchumi wa kidijitali.”

Anasema malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa ni kwa ajili ya watu na sio serikali. Kwa hiyo vijana wadogo wenye mawazo mapya ambayo yanalenga kutatua changamoto za kwenye jamii sisi tutawasaidia namna ya kuyaboresha ili yaweza kuwasadia kuwa wajasiriamali.

“Kwa sasa kiwango cha matumizi ya kidijitali kwa wanawake bado kipo chini ni kama asilimia 30 tu kwa hiyo ni shauku yetu kuona mradi huu unachangia kufikia asilimia 70. Teknolojia itawasaidia kupata fursa ya kubadilishana mawazo na wengine na kukuza vumbuzi zao ziweze kuyafikia masoko,” alisema mkurugenzi.

Naye mwakilishi wa UN Women Tanzania Hodan Addou alisema, “Tunatumia uvumbuzi na teknolojia kusaidia malengo endelevu katika kuhakikisha kuwa vijana wa kike wanakuwa sehemu ya mchakato wa maendeleo. Kuna haja ya wavumbuzi kutengeneza bidhaa ambazo zitajibu changamoto za wanawake na wasichana,”

Alisema ni jambo la busara kuhakikisha wanawake wanakuwa mstari wa mbele kwani wanakumbana na changamoto nyingi za matumizi ya kidijitali, mfano kuna baadhi ya kazi wanakosa kutokana na kukosekana kwa ujuzi wa kigijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwandamizi wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Ubalozi wa Canada Helen Fytche alisema maswala ya teknolojia kwa sasa ni muhimu ulimwenguni kwa maendeleo na ni chanzo kinachoongoza kwa fursa za kiuchumi.

“Tanzania haiwezi kubaki nyuma, Canada itaendelea kushirikiana na serikali na inakaribisha mipango kama ya DOT ambayo inalenga kuinua wanawake kwenye mswala ya kidijitali,” alisema.

Kazi za Kidijitali (Digital Jobs)

Kupitia nguzo ya kazi ya kidijitali, DOT itatoa mafunzo ya uwezeshaji kwa vijana 10 ambapo vijana hawa watawezesha vijana wengine 500 kukuza ujuzi wao wa matumizi ya teknolojia na kuwafanya vinara katika soko la ajira. Nguzo hii ni mahsusi katika kuongeza wigo wa fursa katika viwango vyote vya ujuzi wa kidijitali kuanzia ngazi za awali hadi utaalamu wa kimataifa. Programu ya kazi za kidijitali za DOT Tanzania itawapa vijana ujuzi ambao unakwenda sambamba na karne ya 21 na mahitaji ya waajiri.

Biashara ya kidigitali (Digital Business)

Kwa upande wa nguzo ya biashara ya kidijitali, mradi wa Thubutu Kuhama utasaidia vijana wenye biashara ndogo ndogo na zisizo rasmi kujirasimisha na kutumia teknolojia kuboresha biashara zao. Washiriki watajiongezea ushindani katika uelewa wa Tehama, usawa wa kijinsia, ujasirimali na ujuzi unaokwenda sambamba na karne ya 21.

Pia watapata nafasi ya kuunganishwa na mtandao wa vijana wenzao, wawezeshaji na mashirika yanayosaidia biashara. Matokeo yake vijana 8,000 wataongeza ujuzi wa kidijitali na biashara, watajiunga na mfumo ya kibiashara na kuwa wamiliki wa biashara hivyo watakuza mitaji yao na biashara zao.

Ujasiriamali Jamii (Social Entrepreneurship)

DOT inasaidia vijana 150 kutambua fursa zilizopo ndani ya changamoto zinazokumba jamii zao kila siku. Mafunzo ya Ujasiriamali jamii hulenga vijana wenye hulka ya uongozi kwa kuwasaidia kujenga mawazo yao ya biashara yanayolenga kutatua changamoto zinazozunguka jamii zao.

Changamoto hizo ni zile za kijamii, kimazingira, elimu na mifumo. Washiriki wa programu zililzo chini ya nguzo hii watajengewa ujuzi wa biashara kidijitali ikiwa ni pamoja na usawa wa kijinsia, teknolojia na ubunifu wa kijamii. Wakimaliza program, watakuwa na biashara endelevu zitakazoboresha maisha yao na jamii zao. Lengo kuu ni kuwakuza vijana kidijitali na kibiashara pamoja na kuhakikisha kuwa wameunganishwa na mfumo wa msaada wa kibiashara na wamiliki wa biashara waboreshe faida na biashara zao.

Uongozi wa Jamii (Community Leadership)

Kupitia nguzo ya Uongozi wa Jamii, DOT inasaidia vijana 110 kuwa viongozi katika jamii zao ambako wataendesha miradi ya ujuzi na maendeleo katika jamii zao.

Watajengewa ujuzi, uelewa wa kidijitali, usawa wa jinsia na ujuzi wa karne ya 21; watawezeshwa pia vifaa kuendesha shughuli zao. Watakapomaliza program hiyo, vijana watatumia ujuzi wao wa uongozi na uzoefu wa maisha halisi ya ulimwengu kupata ajira na fursa.

DOT Tanzania inakaribisha mashirika na kampuni mbalimbali kushirikiana nao katika kufanikisha mradi huu kwani inaamini utekelezaji wenye tija ni ule unaofanywa kwa ushirikiano.

Unaweza kuwasiliana na Meneja Mawasiliano na Ushirikiano Ndimbumi Msongole kupitia barua pepe: [email protected]