TPDC yataja fursa kwa Watanzania mradi bomba la mafuta

Muktasari:

  • Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) limetaja fursa zaidi ya 10 zinazowahusu Watanzania moja kwa moja wakati wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima- Uganda hadi Tanzania mkoani Tanga eneo la Chongoleani.

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) limetaja fursa zaidi ya 10 zinazowahusu Watanzania moja kwa moja wakati wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima- Uganda hadi Tanzania mkoani Tanga eneo la Chongoleani.

Fursa hizo zimetajwa ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya Serikali za Uganda, Tanzania na wawekezaji kusaini mkataba wa kuanza utekelezaji wa mradi huo mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 13, 2021 mkoani  Dar es Salaam mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Dk James Mataragio amesema kampuni zitakazonufaika nchini ni pamoja na zile za huduma ya chakula na kampuni za ulinzi.

“Pia kampuni za huduma ya maradhi na hoteli, huduma za ofisi, mawasiliano, usafirishaji mabomba, stadi za mazingira, ujenzi, ugavi na ukodishaji wa vifaa vya kubeba mitambo mizito.”

“Lakini faida nyingine za mapato , kodi ya matumizi ya ardhi na kodi ya matumizi ya bandari, pia kutakuwa na gawio litakalotokana na mgawanyo wa hisa ya gharama za mradi,” amesema Dk Mataragio.

Hata hivyo,  Dk Mataragio amesema sehemu ya makubaliano yaliyokuwa na mvutano ni pamoja na hisa za ushiriki wa Tanzania katika mradi huo.

“ Tanzania tumependekeza iwe asilimia 15 ya gharama na tutatoa pesa taslimu, sasa maamuzi yatatolewa na vikao vya baraza la mawaziri hapo baadaye,”amesema akifafanua wabia wengine tayari hisa zake zimeshapitishwa.

Katika hatua nyingine, Dk Mataragio amesema kusainiwa kwa mikataba nchini Uganda kunatoa mwelekeo wa kuundwa rasmi kampuni ya EACOP itakayosimamia uendeshaji wa mradi.


“Kampuni itaundwa na kusajiliwa lakini tutaanza ujenzi rasmi baada ya kusaini mkataba mama, tunaita mkataba hodhi kati ya Tanzania na wawekezaji (HGA) ambao ndani yake una mikataba midogo midogo iliyokamilika Oktoba mwaka jana katika vikao vya Arusha,”amesema.

Mikataba minne ya HGA aliyotaja Dk Mataragio ni pamoja na mkataba wa ardhi katika maeneo ya kipaumbele, mkataba wa utwaaji wa ardhi, mkataba wa haki ya kutumia bandari na mkataba wa ubia kati ya wawekezaji (CNOOC,Total), TPDC na UNOC.