‘Tumalizane’, janga jipya kwa waendesha bodaboda nchini

Muktasari:

  • Usafiri wa pikipiki maarufu ‘bodaboda’ sasa ni kimbilio la Watanzania walio wengi, bila kujali ukubwa wa kipato chao.

Dodoma. Usafiri wa pikipiki maarufu ‘bodaboda’ sasa ni kimbilio la Watanzania walio wengi, bila kujali ukubwa wa kipato chao.

Umuhimu wa usafiri wa bodaboda unaonekana pale mtumiaji anapotumia muda mfupi kufika alipokusudia, tofauti kama angetumia usafiri kama vile gari.

Katika miji mikubwa yenye msongamano, usafiri wa pikipiki unatumika kwa kiwango kikubwa kuokoa muda. Vijijini bodaboda ni mkombozi kwa kukosekana vyombo vingi vya usafiri, hasa magari.

Hata hivyo, usafiri huu licha ya faida zake chekwa, kwa waendesha vifaa hivyo, uchunguzi wa gazeti hili katika Jiji la Dodoma na maeneo mengine nchini, umebaini kuwa kundi hilo limo kwenye janga jingine jipya la kuwekwa majaribuni na baadhi ya abiria wao hasa wanawake.

Pata picha hii: ‘‘Unambeba mtu anakukumbatia, wakati mwingine anakutekenya makusudi kutengeneza mazingira, ukimfikisha kwake hataki kukupa nauli yako, anaanza kulegeza macho, mwishowe anakwambia ‘Tumalizane’,

Hapa ndipo wanapokwama baadhi ya vijana ambao kwa kuwa damu inachemka, wanajikuta wakiingia mtegoni kwa kufanya ngono, kitendo kinachowaweka hatarini kiafya.

Ndiyo. Tumalizane sasa limekuwa janga jipya kwa waendesha vyombo hivi karibuni, hasa katika Jiji la Dodoma .

Uchunguzi wa Mwananchi umegundua kuwa ukiondoa mambo manne yanayowakabili waendesha bodaboda, ambayo ni: ajali, vifo, faini za barabarani, kuporwa, sasa kuna hili la ‘Tumalizane’ ambalo linaweza kuwaweka watu wa kundi hilo katika mazingira ya kuambukiza au kuambukizwa magonjwa ukiwamo Ukimwi.


‘Tumalizane’

Mwendesha bodaboda katika kituo cha KKKT Mailimbili jijini Dodoma, Geofrey Gidion anakiri kuwa kundi lao la waendesha bodaboda liko kwenye hatari kubwa kwa sasa kutokana na ukweli kuwa wanapata vishawishi ambavyo ni vigumu kuviepuka.

“Ukimfikisha kwake hataki kukupa nauli yako, anaanza kulegeza macho, mwishowe anakwambia ‘Tumalizane’, hapo utafanyaje, wakati mwingine hata kinga huna kwa wakati huo, unafanyaje wakati damu inachemka?” anasema Gidion.

Dereva huyu anasema kuwa kauli ya Tumalizane kwa sasa imekuwa maarufu sana Dodoma na mara nyingine vijana wakikaa kijiweni wanaulizana kama wamemalizana na abiria wangapi, huku baadhi wakisifiana kuwa waliomalizana nao wengine ni warembo zaidi.

Gidioni anataja nyakati za hatari kwao kuwa ni pamoja na usiku ambapo wateja wengi ni wanawake.

‘‘Huo ndiyo muda wa majaribu zaidi kutokana na uvaaji wao, kulewa na wengine kukosa walichokitarajia kwenye sehemu za starehe,” anasema.

Mwenyekiti wa waendesha pikipiki katika kituo cha Dodoma Makulu, Ashery Kingaule anasema shida kubwa ni kwa wanawake watu wazima, kwani hulazimisha, tofauti na wasichana ambao wao hushawishiwa.

Kingale anasema vijana wengine wanaingia kwenye mtego bila kupenda wakati wa kutoa huduma hiyo na mara nyingine hutokea kwa watu wanaowaamini kwamba hawawezi kuwa na mambo ya ajabu kama hayo, wakiwamo wake za watu.

“Kwa sisi watu wazima kidogo tunajitambua, ingawa hiyo haituondolei mtego huo, lakini kwa vijana miaka 20 hadi 25, tuwe wakweli wanaumizwa sana na hiyo ‘tumalizane’, maana ndio wanaowabeba madada poa jioni kuwapeleka maeneo yao na kuwafuata usiku,” anasema Kingale.

Kuhusu wasichana, anasema kinachowaponza ni kwamba wanaonekana kuwa na gharama ndogo kwenye matumizi, kwani wanafunzi hata wakipewa Sh5,000 na chipsi zinawatosha na walio wengi hawapelekwi nyumba za kulala wageni kwa kuhofia kukamatwa hivyo wanapelekwa maeneo aliyoita ‘mageto’ ya wavulana.

Kuhusu tahadhari anasema ipo, lakini ni kidogo kwani inakuwa vigumu kila mahali kuwa na kondomu kwa hofu ya kusahau kwenye nguo zao, mwisho wake zinaweza kukutwa na wake au wapenzi wao halafu inakuwa hatari.

“Kingine hawa wanawake wanakuwa na maswali mawili tu, ‘njoo tumalizane’ na swali la pili ‘je, huniamini?’ Hapo ujue mchezo umekwisha, hili nalisema nikiwa na uhakika nalo, kwani limewahi kunikuta, nilifanyaje? usihoji,” anasisitiza.


Si Dodoma pekee

Jijini Mwanza, kiongozi wa waendesha bodaboda katika kituo cha Mjengoni kata ya Luchelele, Boniface Shayo alisema katika kituo chake ameshapokea taarifa ya baadhi ya bodaboda kushiriki ngono na abiria wao pale wanaposhindwa kulipia gharama ya usafiri huo.

Alisema visa hivyo vinajitokeza sana usiku ikilinganishwa na mchana, huku akisema baadhi ya bodaboda hujikuta wakishiriki tendo la ndoa na watu wasiowafahamu bila kutumia kinga, hali ambayo alisema ni hatari kutokana na maambukizi ya VVU

Aliwataka waendesha pikipiki nchini kutanguliza nidhamu katika kazi hiyo ili kujilinda kiafya na kufikia malengo yao.

“Ukiwauliza wanakwambia hakuna namna nyingine ya kumfanya mtu asiye na hela ya usafiri. Hii ni hatari kwa sababu mtu anaweza kupata maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa,” alisema Shayo.

Baadhi ya madereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam walilieleza Mwananchi kuwa uwepo wa tabia hiyo unachangiwa na wahusika kutokuwa na msimamo wa utafutaji

“Haya mambo yapo kila siku madereva wenzetu wa bodaboda kutembea na abiria wao wa kike, tena wengine machangudoa, ila sasa ni suala la mtu binafsi kujua kilichokuweka barabarani, wengine tuna familia zinatutegemea,” alisema Musa Assa dereva bodaboda wa Mkwajuni, Kinondoni.

Dereva mwingine wa bodaboda kutoka Mabibo (jina tunalijifadhi) alisema kuwa wakati mwingine wanashindwa kujizuia kwa sababu ya umri mdogo unaoambatana na matamanio ya mwili.

“Kwa mfano, mimi hapa nina miaka 19 na bado sijaoa, kwa hiyo wakati mwingine ikitokea, mi nafanya tu, sema sasa wakati mwingine ninajuta baada ya kufanya hivyo na tena bila kondomu,” alisema.

Paul Michael ni dereva bodaboda eneo la Magomeni, alisema kuna haja ya mamlaka husika kutoa elimu zaidi kwa vijana wa bodaboda ili kuwanusuru.

“Huu mchezo upo sana na hasa kwa wale madereva wenye umri mdogo, nafikiri wapewe elimu zaidi,” alisema Michael,

Mkoani Mbeya madereva bodaboda walieleza changamoto ya kushawishiwa kufanya ngono zisizo za lazima na wanawake ambao wamekuwa wakikodi pikipiki kama abiria nyakati za usiku na pindi wanapodaiwa fedha kuwataka kumalizana ili wasilipe nauli.

Walisema kuwa wamekuwa katika kundi lenye hatari kubwa ya kupata maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kutokana na udharura wa kufanya mapenzi pasipo maandalizi ya kutumia kinga.

Erasto Mwakalonge wa kituo cha Mabatini anasema kadhia hiyo imekuwa ikijitokeza usiku na kwamba kundi kubwa la wanawake wamekuwa wakijiuza kwenye kumbi za starehe na wanapokwama wanawavaa madereva bodaboda pale wanapopelekwa makwao na kushindwa kulipa nauli wakitanguliza hoja ya kumalizana kwa ngono.

“Kimsingi, tunakerwa sana na tabia ya baadhi ya wanawake wa namna hiyo, kwani vijana wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 20 ndio waathirika wakubwa katika hilo na wako katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa,” alisema.

Dereva wa kituo cha Stendi kuu, Raphael John alisema kuwa wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU kwa kubakwa na wanawake ambao wanajifanya abiria nyakati za usiku, ambao wamekuwa wakizagaa katika kumbi za starehe, na wengine kujifanya abiria katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani.

Alisema kutokana na changamoto hiyo wanaomba wadau, hususan Serikali kupitia wataalamu wa afya kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza pamoja na kuongeza vituo vya utoaji wa kondomu kwenye maeneo ya stendi na vituo vya daladala jijini Mbeya.

Jijini Arusha vijana wanaojihusisha na biashara ya bodaboda walieleza kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa na hasa katika mji wa Namanga.

Wanasema limekuwa kubwa kutokana na bei ya usafiri kupanda. Wanawake wanaokosa nauli wanalazimika kumalizana na madereva.

Mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda katika mji wa Namanga uliopo mpakani mwa Kenya na Tanzania, Omar Zuakuu alisema kuna wasichana ambao wamekuwa wakipenda wenyewe kufanya ngono na waendesha bodaboda kama ujira wa kupelekwa sehemu wanayotaka na wengine wamekuwa wakibakwa, hasa baada ya kulewa.

“Hili tatizo ni kubwa, kuna ongezeko la vijana wetu kuugua magonjwa ya ngono, hasa kisonono kutokana na ngono zembe na wasichana tofauti,” alisema.

John Lenana, mwendesha bodaboda katika Jiji la Arusha eneo maarufu la pikiniki ambalo kuna biashara ya wasichana wanaojiuza miili, alisema baadhi yao wamekuwa na uhusiano na wasichana ambao kila siku huwapa usafiri.

“Wengi wamekuwa na uhusiano hadi wengine kuishi pamoja maana wanawabeba kuwaleta hapa kujiuza na unakuta mara nyingine hawalipi na hapo uhusiano wa kimapenzi ndipo unapoanza,” alisema.

Alisema kuna baadhi ambao hupata magonjwa makubwa ya ngono, ikiwamo maambukizi ya VVU na baadaye kurejea makwao nje ya Arusha.

“Ukiona mwenzako anaumwa na baadaye haonekani kwa muda, tunajua tayari amerudi kijijini kwao kwa matibabu, maana huwa tunachanga na tatizo likiendelea tunamshauri kurudi nyumbani,” alisema.

Bodaboda nao tatizo

Hata hivyo, wakati waendesha bodaboda wakidai kuwekwa majaribuni na abiria wao, mwelimishaji rika, Judith Michael anataja waendesha bodaboda kama kundi hatari ambalo linapaswa kuchungwa katika kueneza maambukizi ya VVU na Ukimwi.

Judith anasema katika kazi zake za kuelimisha rika, anakutana na matukio ya wasichana kupewa mimba za utotoni, ugomvi wa kugombea wasichana na kuenea kwa maambukizi ya Ukimwi kupitia kundi hili.

“Bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwenye kundi hili, yaani vijana hawa wamejaa tamaa na kutwa nzima wao wanazungumza habari za mapenzi tu, wanaharibu watoto wa shule, wake za watu yaani ni vurugu, natamani Serikali iwatungie sheria lazima watembee na kondomu maana kutwa nzima wao wanazungumza mambo ya mapenzi,” anasema Judith.

Serikali yastuka

Mratibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi katika mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, Enrico Kawanga anasema tayari wameshaliona kundi hilo na kukiri kuwa lipo kwenye hatari kubwa ya kuambukiza au kumbukizwa VVU.

Licha ya kutotaja ukubwa wa tatizo kwa kutaja takwimu, Kawanga anasema wameweka mkakati wa kuona namna ya kumaliza tatizo hilo ambapo wameshalitambua kundi hilo na kuwa na mawasiliano na viongozi wao ili kufikia malengo ya utoaji elimu.

Anakiri kuwa kuna changamoto kubwa kwa waendesha bodaboda, kwani wamebeba siri kubwa ya maisha ya wake za watu, hivyo baadhi ya kinamama huwakubalia ili wasitoe siri.

“Tumelitambua kundi hili muhimu sana, ni kweli wako mtegoni maana baadhi ya abiria na hasa wanawake huwachukua lakini wakifika mwisho wa safari wanasema hawana nauli, hivyo wanaomba kumalizana…ndipo inapoanzia,” anasema Kwanga.

Mratibu huyo anasema kuwa wamezungumza na viongozi wa bodaboda kwenye maeneo yote, lakini wanaona haisaidii kwani viongozi wao wakitoka, vijana wanaona kama wanadanganywa kwa sababu hao viongozi wamelipwa fedha.

Kuhusu mkakati wa kujilinda wenyewe, alisema hata wakiamua kugawa kondomu za bure kwenye vijiwe vya bodaboda, haitasaidia bali wanatafuta fedha ambazo zinasaidia kuwakusanya mahali pamoja na kuwapa elimu kuliko ilivyo sasa.

Alisema klabu nyingi za bodaboda zimeanzishwa na kutambulika kutokana na kutazama wingi wa watu wanaopata maambukizi kupitia bodaboda.

Kwa mujibu wa Kawanga, waendesha bodaboda ni mawakala wakubwa na watunzi siri za wanaume na wanawake, hasa kwenye suala la mapenzi, ndiyo maana huchukuliwa kama kundi linaloweza kusikilizwa na kuhudumiwa wanachotaka, licha ya wakati mwingi huwa wanashawishika.


Takwimu za Tacaids na Ukimwi

Machi 22, 2022 Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema wanaoambukizwa VVU kwa kasi ni vijana, kwani asilimia 30 ya maambukizi mapya ni vijana wa umri wa kati ya miaka 15 hadi 24.

Dk Maboko alisema katika kundi hilo kati ya vijana 100 walioambukizwa VVU hapa nchini, 80 ni vijana wa kike, huku akieleza namna umri wa kuanza vitendo vya ngono unavyomtisha, kwani baadhi wanaonyesha kuanza vitendo hivyo wakiwa na miaka minane.


Imeandikwa na Habeli Chidawali (Dodoma), Hawa Mathias (Mbeya), Musa Juma (Arusha),