Ubunifu waongeza matumizi ya bima kwa wananchi

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa huduma za bima kwa ajili ya masomo na ile ya vikundi vya akiba na mikopo (Saccos) iliyozinduliwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na Kampuni ya Metro Life Assuarance.

Muktasari:

  • Ada bima imeanzishwa kwa lengo la kutatua changamoto kubwa inayopitiwa na familia pindi mzazi au mlezi anapofariki dunia

Dar es Salaam. Kamishina wa bima nchini Dk Baghayo Saqware amesema ubunifu unaoendelea kufanya katika sekta hiyo unakuza ushiriki wa wananchi katika huduma za kifedha.

Dk Saqware ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya bima Tanzania (tira) amesema huduma za bima zinatoa suluhu ya kuwakinga wananchi na kupoteza mali lakini pia ni njia ya uwekezaji.

Dk Saqware amesema hayo juzi katika uzinduzi wa huduma za bima kwa ajili ya masomo na ile ya vikundi vya akiba na mikopo (Saccos) iliyozinduliwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na Kampuni ya Metro Life Assuarance.

“Huduma za bima kama hizi zinakuwa na sura mbili ya kwanza ni kujikinga na ya pili ni kuwekeza. Ukiwa na bima unakuwa na uhakika wa kutopoteza mali na kurudi kwenye umasikini lakini pia unaweza kutatua changamoto nyingine za kifedha,” amesema Dk Saqware.

Akizungumzia huduma ya ada bima iliyoanzishwa na taasisi hizo amesema inakwenda kutatua changamoto kubwa inayopitiwa na familia pindi mzazi au mlezi anapofariki au kupata ulemavu wa kudumu.

Dk Saqware anawahakikisha watoa huduma za bima kuwa Tira kuwa itaendelea kuunga mkono ubunifu unaofanya na watoa huduma lakini pia kuwapa watumiaji usalama wa kifedha, utulivu, kujiamini na amani.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya TCB, Jema Msuya yeye anasisitiza kuwa lengo la kuja na mpango huo ni kutoa uendelevu wa elimu kwa watoto ikiwa wazazi watapata majanga ya kifo ama ulemavu wa kudumu na kumfanya ashindwe kulipa ada ya shule.

Mkuu wa Kitengo cha Bima kutoka TCB, Francis Kaaya akielezea kuhusu ada bima amesema hata mtoto atakapohama shule atalipiwa ada kama kawaida lakini hata ada kwa shule aliyopo ikipanda bima hiyo italipa.

"Tunaelewa umuhimu wa elimu katika kujenga kesho bora ya jamii yetu na kila mzazi anakuwa na ndoto ya kuona mtoto wake anafikia kiwango fulani cha elimu, bima hii inatoa uhakika wa hilo na inalea pia kwani mtoto atakuwa akipewa fedha ya matumizi Sh1 milioni kwa mwaka,” amesema Kaaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Metro Life Assurance, Amani Boma amesema kupitia ushirikiano wao na Benki ya TCB wanajivunia kuwaletea Watanzania huduma ya bima kadri ya mahitaji yao.

“Wote tunajua ukifikisha miaka 40 kama una familia unaanza kuwaza hili leo nikiondoka itakuwaje. Ndiyo maana tumekuja na ubunifu kama huu tunajua hii ni changamoto kwa wengi ndiyo maana tumekuja na suluhisho la Adabima,” amesema Boma.

Kuhusu bima ya Saccos amesema mchango wa huduma hizo za kifedha ni muhimu katika kuimarisha uchumi na jamii lakini zimekuwa na changamoto ya kupoteza fedha pindi mwanachama anapofariki na ndiyo maana wameleta suluhisho.